Na Mwandishi Wetu
Timu ya Taifa ya Kenya ‘Harambee Stars’ imejiondoa katika mashindano maalumu ya CECAFA yaliyopangwa kuanza leo Julai 21,2025 jijini Arusha kwa ajili ya maandalizi ya michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN- 2024).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka nchini Kenya (FKF), uamuzi huo umefanyika kutokana na mapendekezo na ushauri wa benchi la ufundi la timu hiyo, likiongozwa na Kocha Mkuu Benni McCarthy, baada ya tathmini ya kina ya hali iliyopo kwa sasa, ikiwamo kutoridhishwa na mazingira.
Kenya ilikuwa icheze leo dhidi ya Uganda lakini baada ya kujitoa, itarejea nchini Kenya na kuendelea na maandalizi ya CHAN.
Mashindano hayo maalum yalikuwa yashirikishe nchi nne za Tanzania, Uganda, Senegal na Kenya.
Michuano ya CHAN inatarajiwa kuanza Agosti 2, 2025 ambapo Tanzania itafungua dimba dhidi ya Burkina Faso kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.