Humphrey Polepole ajiuzulu

Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole, ametangaza kujiuzulu nafasi yake ya Ubalozi na nafasi nyingine za uongozi wa Umma kuanzia leo Julai 13, 2025.

Kupitia barua yake aliyoweka katika mitandao yake ya kijamii, Polepole amemwandikia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, leo Julai 13, 2025, amesema amechukua uamuzi huo kutokana na kukosekana kwa uelekeo sahihi katika uongozi wa kitaifa, kufifia kwa maadili na dhamira ya kuhudumia Wananchi.

Amesema katika kuhudumu kwake ndani na nje ya nchi, amefuatilia kwa karibu na kushuhudia kwa masikitiko makubwa mwelekeo wa uongozi usiojielekeza ipasavyo katika kusimamia haki za watu, amani na kuheshimu watu.

“Kufifia kwa dhamira ya kweli na uwajibikaji wa dhati wa kushughulikia kero na changamoto zao, na kudidimia kwa maadili ya uongozi katika ngazi mbalimbali.

“Kwa heshima na unyenyekevu, naomba kukutaarifu kuwa nimefikia uamuzi wa kujiuzulu nafasi yangu ya Uongozi wa Umma nikiwa Balozi na Mkuu wa Kituo cha Uwakilishi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Havana – Cuba, pamoja na uwakilishi wa eneo la Karibe, Amerika ya Kati na nchi rafiki za Colombia, Venezuela na Guyana.

“Uamuzi huu si mwepesi, bali umetokana na tafakari ya kina juu ya mwenendo wa uongozi katika nchi yetu, uzoefu wangu kama Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Novemba 2020 – Machi 2022), na hatimaye kama Balozi katika vituo vya Lilongwe – Malawi (Machi 2022 – Aprili 2023) na Havana – Cuba (Aprili 2023 – Julai 2025).

“Mheshimiwa Rais, nilipokea kwa heshima kubwa uteuzi na dhamana uliyonipa kuwa mwakilishi wa nchi yetu katika ngazi ya kimataifa. Niliamini na ninaendelea kuamini lilikuwepo kusudi na kazi muhimu ya kuyashika, kuyasimika, kuyasimamia, kuyaimarisha na kuyaendeleza maslahi mapana ya nchi yetu katika maeneo ya uwakilishi ulinipa dhamana ya kuyasimamia. Ni heshima kubwa na isiyopimika kuaminiwa kuwa Mwakilishi wako, Nchi yetu, Taifa letu, wananchi na Mamlaka ya nchi. Kwa hili, nasema asante.

“Hata hivyo, kwa muda wote wa kuhudumu ndani na nje ya nchi, nimefuatilia kwa karibu na kushuhudia kwa masikitiko makubwa mwelekeo wa uongozi usiojielekeza ipasavyo katika kusimamia Haki za watu, Amani na kuheshimu watu, kufifia kwa dhamira ya kweli na uwajibikaji wa dhati wa kushughulikia kero na changamoto zao, na kudidimia kwa maadili ya uongozi katika ngazi mbalimbali. Kudhoofika kwa utekelezaji wa majukumu ya msingi ya serikali kwa ajili ya ustawi wa wananchi; mambo haya yanateteresha maslahi mapana ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Haya yote yamezidi kunifanya nikose amani ya moyo na imani katika uongozi niliopo ndani yake sasa.

“Matukio ya hivi karibuni ya wazi ya kukiuka misingi, utamaduni na desturi za Chama cha Mapinduzi (CCM) – hususan katika mchakato wa uteuzi wa wagombea ndani ya Chama ambao kwa kila awamu huwa msingi wa kukihuisha Chama na fursa ya kufanya Mageuzi ambayo kwa pamoja hukipa chama sura ng’aavu mbele ya umma kabla ya uchaguzi; desturi hii ya kufanya mageuzi ndani ya chama imekuwa nguzo muhimu ya ukubalifu na ushindi wa CCM mbele ya umma. Imekuwepo kauli maarufu ya CCM isemayo “Chama kwanza mtu baadaye”, mwanzoni mwa mwaka huu, nilipoona kauli hii inafanyika vinginevyo, nimejiuliza mara kadhaa ni maslahi ya nani yanapiganiwa wakati huu, mtu, kikundi au Chama Taasisi?

“Kwa kuwa siwezi kuendelea kuwa sehemu ya uongozi usiohamasika na utii wa misingi ya katiba ya nchi na chama, haki, maadili, utu na uwajibikaji kwa wananchi, nimeamua kwa hiari yangu kujiuzulu nafasi yangu ya uongozi na utendaji serikalini.

“Nitaendelea kuwa mwana CCM wa kawaida, mzalendo na raia mwaminifu kwa Taifa na nchi yetu.

“Ninamwamini Mungu wa Mbinguni na ninahamasika na tumaini kuu kwamba siku moja nchi yetu itaongozwa kwa misingi ya haki, maadili, usimamizi thabiti wa miiko na nidhamu ya uongozi, dhamira njema, siasa safi, uongozi bora na hofu ya Mungu.

“Mheshimiwa Rais, nakushukuru kwa fursa uliyonipa, naamini historia itatoa tafsiri sahihi ya hatua hii”, ameandika Polepole.

spot_img

Latest articles

Nandy ahamasika kutangaza Nembo ya Made in Tanzania Kimataifa

Na Tatu Mohamed MSANII wa muziki wa kizazi kipya, Faustina Mfinanga (Nandy), amesema elimu aliyoipata...

Ndumbaro: Sheria 300 Zimetafsiriwa kwa Kiswahili Ili Kuimarisha Uelewa kwa Wananchi

Na Tatu Mohamed WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro, amesema kuwa hadi...

Jessica: CCM inajali uongozi wa vijana

Na Mwandishi Wetu KATIBU wa Idara ya Uhamasishaji na Chipukizi UVCCM TAIFA, Jessica Mshama...

Waziri Aweso: Tuna uhakika wa maji ya kutosha Dar na Pwani

Na Mwandishi Wetu WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso amewatoa hofu wakazi wa mikoa ya...

More like this

Nandy ahamasika kutangaza Nembo ya Made in Tanzania Kimataifa

Na Tatu Mohamed MSANII wa muziki wa kizazi kipya, Faustina Mfinanga (Nandy), amesema elimu aliyoipata...

Ndumbaro: Sheria 300 Zimetafsiriwa kwa Kiswahili Ili Kuimarisha Uelewa kwa Wananchi

Na Tatu Mohamed WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro, amesema kuwa hadi...

Jessica: CCM inajali uongozi wa vijana

Na Mwandishi Wetu KATIBU wa Idara ya Uhamasishaji na Chipukizi UVCCM TAIFA, Jessica Mshama...