Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imezindua huduma mpya ya kidijitali inayowezesha wananchi kupata taarifa kuhusu namba na kitambulisho cha Taifa kwa njia ya ujumbe mfupi wa maneno kupitia namba ya 15274.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Banda la NIDA ndani ya Maonyesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa NIDA, Godfrey Tengeneza amesema huduma hiyo inalenga kurahisisha upatikanaji wa taarifa kwa wananchi bila kulazimika kufika ofisi za mamlaka hiyo.
“Huduma hii mpya tunayokwenda kuizindua hivi karibuni, tayari imeanza kufanya kazi. Mwananchi anatuma ujumbe mfupi kwenda 15274 akiulizia taarifa za kitambulisho chake, nasi tunamjibu papo hapo. Hii ni sehemu ya maboresho tunayofanya kuhakikisha huduma zetu zinafika kwa urahisi na kwa wakati,” alisema Tengeneza.

Kwa mujibu wa Tengeneza, maboresho hayo yamepunguza muda wa upatikanaji wa namba ya kitambulisho na kitambulisho chenyewe. “Kwa sasa ndani ya siku nne baada ya kujisajili, namba ya kitambulisho inakuwa tayari. Kitambulisho chenyewe hutolewa kati ya wiki mbili hadi tatu. Mwananchi hupokea ujumbe mfupi kwenye simu yake pindi kitambulisho kinapokuwa tayari,” aliongeza.
Katika maonyesho hayo, NIDA pia inatoa huduma mbalimbali kwa wananchi ikiwemo usajili kwa ajili ya kupata kitambulisho cha Taifa, kutoa elimu kuhusu taratibu za kujaza fomu za maombi na viambatisho muhimu vinavyotakiwa, pamoja na kutoa taarifa kwa wale wanaotaka kujua kama namba au kitambulisho chao kimeshatolewa.
Banda la NIDA limevutia idadi kubwa ya wananchi, hasa kutokana na huduma ya usajili inayotolewa moja kwa moja katika maonyesho hayo.

“Tumegawa sehemu zetu kuwa mbili: moja kwa ajili ya huduma za usajili na nyingine kwa huduma nyingine zisizo za usajili. Hii imeongeza ufanisi na kurahisisha huduma kwa wananchi,” alifafanua Tengeneza.
Aidha, NIDA inatumia fursa ya maonyesho haya kutoa elimu kwa umma kuhusu shughuli mbalimbali zinazofanywa na mamlaka hiyo, ikiwa ni pamoja na umuhimu wa kuwa na kitambulisho cha Taifa katika kupata huduma mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Maonyesho ya Sabasaba hufanyika kila mwaka kwa lengo la kuwaunganisha wadau wa sekta mbalimbali na wananchi, huku NIDA ikiwahakikishia Watanzania huduma bora, za kisasa na zinazokidhi mahitaji ya wakati.