Na Tatu Mohamed
CHUO Kikuu cha Dodoma (UDOM) kimeshiriki Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) kwa kutoa elimu ya ulaji bora kwa lengo la kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza.
Akizungumza katika banda la UDOM, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Masoko wa chuo hicho, Rose Joseph, amesema ulaji sahihi ni msingi wa afya bora, hivyo elimu hiyo inalenga kuwasaidia wananchi kuboresha lishe na kuepuka maradhi kama vile shinikizo la damu na kisukari.
“Tunatoa huduma ya bure ya upimaji wa afya na ushauri wa tiba lishe kwa wananchi wote. Huduma hii inamwezesha mtu kujua vyakula sahihi kwa afya yake na muda wa kula,” amesema.

Ameongeza kuwa, UDOM inatoa huduma ya ushauri wa kisheria hasa katika mikataba ya biashara ambayo wengi wamekuwa wakidhurumiwa kutokana na kutojua sheria vizuri.
“Kwa ambao wanakesi mahakamani, UDOM ipo tayari kutoa wataalam wake kuweza kuwasaidia kwa ushauri wa kisheria,” amesema.
Pia amesema watakaotembelea Banda lao watapata fursa ya kujua mafunzo ambayo yanatolewa na Chuo hicho.
“Chuo kina zaidi ya program 90 za Shahada ya awali, na program zaidi ya 56 za masters, kwahiyo tunawakaribisha wale ambao wanataka kujiendeleza watembelee kwenye Banda letu lililopo katika Maonesho ya Sabasaba ili kufahamu zaidi.

“Tumebuni pia utaratibu wa watu kujiendeleza kwa njia ya mtandao kwahiyo ni fursa ya watu kujiendeleza wakiwa nyumbani,” ameongeza.
Amefafanua pia, kupitia mradi wa PPP Chuo kimebuni miradi saba ambayo wanatafuta wadau kuweza kuwekeza katika miradi hiyo ikiwemo ujenzi wa Hoteli ya Nyota Tano.