Na Mwandishi Wetu
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan, kesho Juni 10, 2025 anatarajia kupokea gawio na michango mingine kutoka kwa taasisi za umma na kampuni ambazo serikali ina umiliki wa hisa chache, huku matumaini ya wataalamu wa uchumi na biashara yakiwa makubwa.
Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, ambaye ndiye msimamizi mkuu wa taasisi hizo, anaungana na wataalamu hao kwa kusema kuwa kwa mwendo wa makusanyo ulivyo, anaamini gawio la mwaka huu wa fedha litakuwa la kihistoria.
Wataalamu waliozungumzia tukio la gawio kwa nyakati tofauti wameonesha imani yao kuwa makusanyo ya gawio na mapato mengine yasiyo ya kodi yataongezeka kwa kiasi kubwa ikilinganishwa na mwaka wa fedha uliopita na kwamba fedha hizo zitatumika kwa maendeleo ya Taifa.

Mwaka wa fedha uliopita (2023/24), kiasi cha Sh767.1 bilioni kilikusanywa ikiwa ni mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na gawio, mchango wa asilimia 15 ya mapato ghafi, na michango mingine.Kuna dalili njema kuwa mwaka huu, unaoisha Juni 30, makusanyo yakawa makubwa zaidi kwani hadi Juni 2 tayari takribani bilioni 900 zilikuwa zimekusanywa.
Prof Abel Kinyondo, mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anaamini kuwa makusanyo ya mwaka huu yanaweza yakafikia Sh1 trilioni kwani hakukuwa na changamoto yoyote kubwa iliyoathiri shughuli za kiuchumi.
Alishauri kuwa ni vema mapato yasiyo ya kodi yakaelekezwa kwenye maeneo ambayo yataleta tija kwa Taifa, huku akitolea mfano wa uwekezaji kwenye miradi ya maendeleo.“Lazima tuelekeze fedha hizo kwenye maeneo ambayo yatakuwa na athari chanya, vinginevyo haitakuwa na maana kiuchumi na kijamii,” alisema Prof Kinyondo.

Dkt. Daudi Ndaki, Mchumi kutoka chuo kikuu cha Mzumbe, pia alionesha shauku yake kuona pesa itakayokusanywa inatafutiwa namna ya kuikuza ili iwekezwe maeneo mengine.
Alionesha imani yake kuwa siku ya Jumanne wiki hii Rais Samia atapokea gawio zuri kutokana na kuongezeka kwa ufanisi wa taasisi za umma.“Mashirika mengi yameboresha bodi zao, sio ‘business as usual’ (hawafanyi kazi kwa mazoea tena),” alihitimisha Dk. Ndaki.
Dkt. Lutengano Mwinuka, Mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma, alishauri: “Lazima tuje na mkakati wa namna bora ya kutumia gawio.”
Alisema gawio linapaswa kutumika katika maeneo ambayo yataleta matokeo makubwa au ya kimkakati.
Aliwashauri wasimamizi wa taasisi za umma kuendelea kuongeza ufanisi ili makusanyo yaendelee kupaa.
Kauli hii inaungwa mkono na mtaalamu wa uchumi na biashara, Dk. Donath Olomi: “Mashirika ya biashara yanatakiwa yaendelee kubanwa linapokuja suala la ufanisi ili wapate faida kubwa zaidi na hatimaye kutoa gawio nono,” alisema mtaalamu huyo.
Serikali, kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina, imewekeza kiasi cha Sh86.3 trilioni katika taasisi na kampuni ambazo ina umiliki wa hisa chache 308.
Ni katika muktadha huo, serikali inataka kuona inafaidika na uwekezaji wake kupitia gawio, ambalo hutokana na faida za mashirika na taasisi za umma zinazofanya biashara.
Aidha, taasisi ambazo hazimo kwenye kundi la gawio zinatakiwa kuwasilisha asilimia 15 ya mapato yao ghafi kila mwaka kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Umma.
Pia, zipo taasisi zinazopaswa kuwasilisha mapato ya ziada kila mwisho wa mwaka wa fedha, ambapo hulazimika kuwasilisha asilimia 70 ya ziada hiyo kwa Serikali kwa mujibu wa Sheria ya Msajili wa Hazina.
Akizungumzia siku ya Gawio, Mchechu alisema kuwa Rais Samia atatoa tuzo kwa taasisi na mashirika 14 yaliyofanya vizuri katika makundi mbalimbali ya uchangiaji kwenye mfuko mkuu wa Serikali, kwa mwaka huu wa fedha 2024/2025.
Alisema kundi la kwanza kutambuliwa ni kampuni zilizo toa gawio kubwa zaidi, kundi la pili ni taasisi wachangiaji wa asilimia 15 kwenye mfuko mkuu wa serikali, kundi la tatu: taasisi na mashirika yaliyoongeza michango yao kwenye mfuko wa serikali, na kundi la nne: taasisi zinazochangia mfululizo kwa miaka 5 –2020/21 – 2024/25.
Aliendelea kueleza kuwa kundi la tano ni taasisi zilizofanyiwa mageuzi makubwa, kutoka kwenye lundo la hasara na kuanza kuchangia, na kundi la sita ni mchango wa kipekee na wa aina yake katika mfuko mkuu wa serikali.