Na Mwandishi Wetu
KESI inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, imeahirishwa hadi Juni 16, 2025 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, huku Mahakama ikimpa onyo kali kwa kutamka maneno bila ruhusa ukumbini.
Uamuzi huo umetolewa leo Juni 2, 2025 na Hakimu Mkazi Mkuu, Franco Kiswaga, wakati shauri hilo lilipotajwa.
Upande wa Jamhuri uliwakilishwa na jopo la mawakili wakiongozwa na Nassoro Katuga, huku utetezi ukiwakilishwa na Wakili Mwandamizi Mpale Mpoki.

Katika maelezo yake, Hakimu Kiswaga amesema hakuna ubishi kuwa mshtakiwa alitamka maneno ya “No reform, no election” akiwa mahakamani, kauli iliyotafsiriwa na upande wa Jamhuri kuwa ni ya kudharau Mahakama.
“Mara tu Mahakama inapokaa, inakuwa kamili kwa mujibu wa kifungu cha 6(c) hivyo hakuna aliyepaswa kuongea bila ruhusa na mshtakiwa hakupaswa kutoa kauli hiyo,” amesema Hakimu Kiswaga.
Aidha, Mahakama imesisitiza kuwa ni marufuku kwa mtu yeyote iwe ni mshtakiwa au wasikilizaji wa kawaida kuzungumza bila ruhusa ya Mahakama.
“Hatua hiyo ni muhimu kuhakikisha Mahakama inafanya kazi kwa kufuata sheria na si mihemko ya mtu binafsi,” amesisitiza Hakimu Kiswaga.
Mbele ya Hakimu Kiswaga, upande wa Jamhuri ukiwakilishwa na jopo la mawakili uliieleza Mahakama kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika, hivyo kuomba Mahakama isogeze mbele shauri hilo.

Upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Mpale Mpoki, ulihoji ni lini upelelezi huo utakamilika na kujibiwa na upande wa Jamhuri kuwa upelelezi upo katika hatua za mwisho.
Katika kesi hiyo, Lissu anadaiwa kutenda kosa hilo Aprili 3, 2025 jijini Dar es Salaam, ambapo alidaiwa kutoa maneno ya uchochezi kwa lengo la kushawishi umma kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, pamoja na kumshinikiza kiongozi mkuu wa serikali.

NJE YA MAHAKAMA
Akizungumza nje ya viunga vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Wakili wa Lissu Dkt. Rugemeleza Nshala amesema “upelelezi unaendelea faili la kesi limerudi kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ameagiza kuna vitu vipelelezwe zaidi,”.
Kuhusu hoja zilizotolewa na upande wa utetezi juu ya kukamatwa kwa mteja wao kabla ya upelelezi kukamilika Dkt. Nshala amesema upande wa mashtaka umeeleza kuwa aina ya kesi hiyo haihitaji upelelezi kukamilika ndipo mtuhumiwa akamatwe hoja ambayo mahakama iliikubali.
Ameongeza kuwa Mahakama imeelekeza upande wa mashtaka kuwa kesi itakapokuja tena tarehe 16 upande wa mashtaka ueleze hali ya kesi imefikia wapi.
Hata hivyo Dkt. Nshala ameeleza kuwa miongoni mwa mambo yaliyoleta mabishano makali ya kisheria ni pamoja na kitendo cha mteja wao tundu Lissu kuingia mahakamani hapo na kuutamka kaulimbiu ya “no reform no election” ambapo upande wa mashtaka ulihoji usahihi wa hilo jambo ambalo hakimu aliuonya upande wa utetezi kuwa jambo hilo si sahihi.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bara, John Heche, ametoa wito kwa mahakama kutafuta eneo lenye nafasi kubwa zaidi ili kuwawezesha watu wengi kuweza kushiriki kwenye kesi zinazomkabili Lissu badala ya vyumba vya mahakama ambavyo vimeonekana kuwa vidogo hali ambayo imesababisha baadhi ya wanachama na watu wengine kushindwa kuingia mahakamani huku wengine wakikumbana na kadhia ya kuzuiwa kwa nguvu na Jeshi la Polisi.”Sisi tunaiomba Mahakama twende hata Karimjee, twende uwanja wa taifa, twende hapo Mwalimu Nyerere watu wakae wasikilize kesi, ni mambo ya kutendeana haki, na haya mambo ndiyo yanafanya tunasema tutashinda nchi hii na tutabadilisha nchi hii, hatutaki mtu mwingine aonewe kama sisi tunavyoonewa”Heche ameeleza kusikitishwa na kushikiliwa kwa Lissu kwa muda mrefu bila ushahidi kupelekwa.Mwisho