Na Mwandishi Wetu
WAKULIMA wa zao la Pamba wilayani Magu wametakiwa kuzingatia sheria na taratibu za kilimo bora ili kupata pamba yenye ubora itakayoendana na thamani ya soko ya zao hilo .
Wito huo umetolewa na Balozi wa pamba nchini, Agrey Mwanri katika ziara yake inayolenga kuhamasisha na kutoa elimu ya usafi na ubora wa pamba kwa wakulima na AMCOS kwa msimu wa pamba wa 2025/2026.

Akizungumza na wakulima wa zao la pamba katika vijiji mbalimbali wilayani Magu, Mwanri amesema Ziara hiyo imetokana na kushuka kwa ubora wa pamba kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo uvunaji mbaya, utunzaji na uchafuaji wa makusudi wa pamba katika baadhi ya vituo vya kununulia pamba.
Akitoa elimu kwa wananchi walioshiriki vikao hivyo msanifu wa pamba kutoka bodi ya pamba Tanzania, Sharifa Salumu amesema ili kilimo kiwe na tija ni lazima kanuni bora zifuatwe ikiwa ni pamoja na kuandaa shamba la pamba kwa kuondoa maotea yote na kuyachoma, kupanda mbegu bora kwa kuzingatia kupanda kwa msitari na kwa vipimo vinavyoelekezwa, kupalilia kwa wakati na kunyunyizia viuwadudu kwa kufuata maelekezo.

Wakulima walioshiriki mafunzo hayo wameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwajali wakulima wa zao la pamba kwani hivi karibuni wakulima hao walipewa baskeli kwaajili ya kuwarahisishia usafiri wa kufika shambani na kutembeleana ili kuhamasisha watu wengine kulima zao hilo.

