Malezi duni yanavyochochea ndoa za utotoni

Na EBENI MITIMINGI

Ni ndani ya halmashauri ya Mlimba darubini yetu inakutana ana kwa ana na visa vya ndoa za utotoni baada ya kuwakuta mabinti wawili wanaojiendeshea maisha yao katika hali ya kupambana kufa kupona ili wao na watoto wao wapate walau mlo wa siku moja.

Mabinti hawa ambao sasa ni dhahiri maisha ya kupambana yamewakomaza mapema kuliko umri wao, wanaakisi kile kilichofichuliwa na Shirika la Umoja wa Matifa la Kuhudumia Watoto UNICEF mwaka 2022 kwamba nchini Tanzania wanawake milioni 1.3 walioolewa kabla ya kutimiza umri wa miaka 15 huku wengine milioni 6.6 wakiolewa kabla ya kutimiza umri wa miaka 18.

Maisha ya mabinti hawa ambao sasa ni wazazi ni kilelezo cha maelfu ya watoto wa kike wa Kitanzania ambao wamepokwa fursa ya maisha ya utoto yanayopasa kuwapa muda wa kujifunza, kukua na kutengeneza ndoto zao za baadaye, lakini sasa wameingia kwenye mahusiano hatarishi na hivyo kupata mimba na ndoa za utotoni.

Moja ya sababu kubwa inayotajwa kuchangia ndoa hizi, ni malezi duni. Wazazi wengi kutokana na umasikini, ujinga, mila potofu hushindwa kupata muda wa kutosha kusimamia mienendo na kuwaonesha upendo watoto wao. Kushindwa huko kwa wazazi, huwasukuma wasichana wadogo kutafuta upendo kwa kuanzisha mahusiano hatarishi ambayo mwishowe hupa ujauzito katika umri mdogo.

Ofisa Ustawi wa jamii Halmashauri ya Mlimba Mkoani Morogoro Latifa Hassan anasema familia nyingi huona ni aibu kulea mtoto aliyepata ujauzito.

“Wenyeji wa huku (Mlimba) ambao wengi ni wakulima wakishaona mtoto wao amepewa ujauzito bila kujali ni msichana wa umri mdogo huamua kumuozesha wakiamini wanaficha aibu,” anasema Hassan.

Waathirika

Darubini yetu inakutana na Prisca Majuto mkazi wa Kijiji cha Mpanga binti mwenye umri wa miaka 15 aliyekuwa na ndoto ya kuwa mwanajeshi, lakini sasa ni mama anayelea mtoto mmoja aliyemzaa katika umri mchanga kabisa. Binti huyu anatoka katika familia masikini yenye usimamizi mdogo wa wazazi. Anasimua namna malezi duni yalivyomfanya kuanzisha mahusiano hatarishi ambayo yaliharibu malengo yake ya kuwa na maisha bora.

“Wazazi wangu walihamia Mlimba (Mjini) na kuniachia nyumba nijilee mwenyewe hapa kijijini nikiwa bado nasoma shule ya msingi.

“Sikuwa na mtu mzima wa kunifundisha, kunionya wala kunisimamia ingawa chakula kilikuwepo kutokana na mavuno tunayopata shambani. Maisha yangu yalikuwa ni ya kutembelea vijiji vingine kwenye sherehe na muziki nikifurahi na mwanamume aliyeonesha kunipenda na kunipa mahitaji yangu mpaka nilipopata ujauzito.

“Mama alipopata taarifa kuwa nina ujauzito aliona namna pekee ya kuondoa aibu hiyo kwa familia ni kuniozesha. Kwa hiyo, alikuja kijijini nilipokuwa naishi peke yangu na kuniuliza akitaka kumfahamu mwanaume aliyehusika, na nilipomfahamisha akanikabidhi nikaishi naye kama mke nilee ujauzito wangu nianze maisha kama mama wa familia.” Prisca anasimulia masahibu yake.

Hata hivyo matarajio ya Prisca kwamba huenda angepata nafuu katika mahusiano hayo hayajatimia kwani licha ya kuishi kwa mwaka mmoja sasa na mwanamume huyo, lakini amekuwa akipitia changamoto kutokana na mzazi mwenzake kutafuta wanawake wengine.

“Mume wangu hanitaki, lakini nalazimika kuendelea kuishi kwake kwa sababu sitamani mwanangu akose malezi ya baba na mama kama nilivyokosa mimi na kusababisha niingie katika ndoa ya utotoni,” anasema Prisca.

Prisca aliyekuwa na ndoto ya kuwa mwanajeshi, sasa amepoteza matumaini ya nafasi yoyote kielimu ambayo ingemtimizia maono yake.

Simulizi ya Prisca inafanana na ya jirani yake Faraja Lyambo wenye umri wa miaka 14, huyu ni msichana aliyekuwa na ndoto ya kuwa muuguzi. Ndoto zake hazikutimia kwani kutokana na malezi ya mzazi mmoja alijikuta ameingia kwenye ndoa ya utotoni.

“Wazazi wangu waliachana nikiwa mdogo, nikalelewa na baba na bibi ambao hawakuwa na utamaduni wa kunipa muda wa kuzungumza nao na kufurahia upendo unaostahili kwa mtoto.

“Katika hali hiyo nilikutana na mwanamume aliyeonesha kunipenda na kila siku nikawa ninaenda mahali alipokuwa akinielekeza tukutane ili anione na kunisimulia mambo mbalimbali ya kufurahisha.

“Siku moja tukiwa kwenye mazungumzo, baba alituona na kuamuru niolewe na mwanamume huyo ili asije kunipa ujauzito kabla ya ndoa na ikawa aibu kwa familia,” anasema Faraja.

Faraja sasa ana umri wa miaka 24 akiwa na watoto wawili wa kwanza akiwa na umri wa miaka 7 na mwingine 1.5 huku akifanya biashara ya kuuza ndizi za kuchemsha katika shule moja ya sekondari kijijini kwao ili kumudu mahitaji yake na watoto wake kila siku baada ya mzazi mwenzake kutowajibika kikamilifu.

Athari za ndoa za utotoni

Muuguzi kutoka Zahanati ya Kijiji cha Ngalimila halmashauri ya Mlimba Mkoani Morogoro, Vivian Towegale, analeza shida za kiafya wanazozipata wasichana wanaoingia kwenye ndoa katika umri mdogo.

“Ni hatari sana kwa wasichana wadogo hasa wanapopata ujauzito. Wakati wa kujifungua hupitia changamoto nyingi kutokana na viungo vyao kutokuwa vimekomaa vya kutosha kuhimili shughuli ya uzazi,” anasema Towegale.

Muuguzi huyu anaongeza, kati ya wajawazito 117 waliohudumiwa katika Zahanati ya Ngalimila mwaka 2024, 17 walikuwa ni mabinti wa chini ya miaka 18.

Wasichana wadogo wanapoingia kwenye ndoa hukatisha maendeleo yao kielimu, na kwa sababu hiyo hukosa fursa ya kuwa na maisha bora kwa siku za baadaye, na kujikuta wakipitia changamoto nyingi zaidi kiuchumi kujihudumia na kuhudumia watoto wao.

Sambamba na changamoto hizo, ziko taarifa kutoka mashirika mbalimbali kama Shirika la Umoja wa Matifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) na Chama cha Waandishi wa Habari wanawake (TAMWA) kuwa ndoa za utotoni huambatana na vitendo vya ukatili ikiwamo vipigo.

Juhudi zinazofanyika kupinga ndoa za utotoni

Latifa anaeleza kuwa wanatumia vyombo vya dola kama mojawapo ya mbinu za kupambana na ndoa za utotoni.

“Tunatumia miongozo mbalimbali ya serikali kupambana na tatizo hili ikiwamo kutumia vyombo vya dola kuzuia ndoa hizi, lakini pia tuna kamati ambazo zinahusika kupokea taarifa kuhusu ndoa za utotoni zinazotarajiwa kufungwa katika maeneo yetu kisha huenda kuzuia zisifungwe na kuwatafutia usimamizi salama mabinti lengwa, anaeleza Ofisa huyo na kuongeza:

“Lakini pia ikitokea mzazi anamuombea uhamisho wa shule binti yake basi huwa tunafuatilia ili kuhakikisha kuwa huko alikoenda amepelekwa kweli shuleni na si mbinu ya ulaghai ili kumpeleka akaolewe, maana wapo wanaotumia mbinu hiyo kuozesha wasichana wadogo.”

Latifa anaongeza kuwa utoaji wa elimu katika mikusanyiko mbalimbali kwenye vijiji na hata shughuli nyingine zinazokusanya wazazi ikiwamo masuala ya kuhudumia kaya masikini (TASAF), mafunzo hutolewa kuhusu usimamizi wa malezi kuwaepusha wasichana dhidi ya ndoa za utotoni.

Ofisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Mlimba Mkoani humo, Hawa Mdoka, anasema ushirikiano kati ya mamlaka na jamii ni muhimu kwani ndiyo utamaliza tatizo la ndoa za utotoni.

“Tatizo la ndoa za utotoni haliwezi kwisha kwa mapambano ya mamlaka peke yake. Wazazi ni muhimu kujua wajibu wao wa malezi. Wakiepuka kutengana na kuwaacha watoto pasipo usimamizi bora,” anasisitiza Mdoka na kuongeza kuwa:

“Lakini pia jamii ikishiriki kikamilifu kutoa taarifa ya vitendo hivi viovu na viongozi wa dini kukemea katika nyumba za ibada tutafanikiwa kumaliza tatizo hili.”

Ukinzani wa kisheria

Ndoa za utotoni ni ukatili dhidi ya watoto ulipaswa kuchukuliwa hatua kali za kisheria ili kukomesha wanaoendekeza tabia hiyo, hata hivyo kuna ukinzani wa kisheria unatoa mwanya kwa wahusika kutoshughulikiwa kikamilifu.

Wakati sheria ya mtoto namba 21 ya mwaka 2009 inawataka wazazi kutimiza wajibu wao wa malezi kwa watoto wao ikilenga ulinzi dhidi ya kupokwa haki za msingi kama elimu, afya, chakula, malazi na kucheza, sheria ya ndoa ya mwaka 1971 inampa ruhusa mzazi kumuozesha mtoto wa miaka 15 hivyo kukosa haki yake ya kulelewa kama mtoto kwa wazazi wake.

Ukinzani huu wa kisheria umepunguza ukali dhidi ya wanaotekeleza vitendo vya ndoa za utotoni na matokeo yake maelfu ya wasichana wadogo hushindwa kutimiza ndoto zao kielimu kwa maisha yao ya baadaye.

spot_img

Latest articles

Timu ya Taifa kriketi ya wanawake kusaka tiketi ya kucheza Kombe la Dunia

Na Mwandishi Wetu Timu ya Taifa ya wanawake ya mchezo wa kriketi ya Tanzania inatarajiwa...

Ratiba ya Ligi Kuu msimu wa 2025/26 hadharani, Dabi ya Kariakoo Des 13

Na Winfrida Mtoi Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara(TPLB) leo  Agosti 29, 2025,  imetangaza ratiba...

Gari, Pikipiki, dhahabu, simu janja zaongeza msisimko katika mnada wa Piku

Na Mwandishi Wetu JUKWAA la kidigitali la PIKU linalojulikana kwa kuendesha minada ya kipekee...

TACTIC yaimarisha huduma za usafiri na usafirishaji Manispaa ya Sumbawanga

Na Mwandishi Wetu MRADI wa Uendelezaji Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC) unaelezwa kuimarisha huduma...

More like this

Timu ya Taifa kriketi ya wanawake kusaka tiketi ya kucheza Kombe la Dunia

Na Mwandishi Wetu Timu ya Taifa ya wanawake ya mchezo wa kriketi ya Tanzania inatarajiwa...

Ratiba ya Ligi Kuu msimu wa 2025/26 hadharani, Dabi ya Kariakoo Des 13

Na Winfrida Mtoi Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara(TPLB) leo  Agosti 29, 2025,  imetangaza ratiba...

Gari, Pikipiki, dhahabu, simu janja zaongeza msisimko katika mnada wa Piku

Na Mwandishi Wetu JUKWAA la kidigitali la PIKU linalojulikana kwa kuendesha minada ya kipekee...