Na Tatu Mohamed, Mwanza
MKURUGENZI Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC), David Kafulila amesema uchumi wa nchi hauwezi kujengwa bila kuzishirikisha sekta binafsi.
Kafulila ameyasema hayo leo Aprili 16, 2025 katika Mdahalo wa kitaifa wa ulioandaliwa na Media Brains kwa kushirikiana na PPPC wenye Mada Kuu ya Ubia wa Sekta ya umma na Sekta Binafsi katika Muktadha wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Amesema Dunia nzima inafanya ubia na masuala hayo yamekuwa ni ajenda kubwa kwenye mijadala ya uchumi duniani.

“Duniani kote imekuwa ni ngumu kwa Serikali hizi kutekeleza matarajio ya wananchi kwa kutumia kodi na mikopo… na ushahidi wake ni takwimu za hali ya uchumi wa Dunia. Ambapo uchumi wa Dunia kufika mwaka jana Novemba ulikuwa takribani Trilioni 115 lakini deni la serikali zote duniani ilikuwa takribani Trilioni 102.
“Deni la Dunia yote kwa maana ya serikali, sekta binafsi, na Kaya ilikuwa ni zaidi ya Dola Trilioni 315…tafsiri yake ni kwamba uchumi wa Dunia unaendeshwa kwa mikopo,” amesema.

Kafulila amefafanua kuwa, uchumi wa Dunia zaidi ya asilimia 90 ni mikopo ambapo kwenye upande wa Afrika mikopo ya serikali kwa uchumi ni takribani asilimia 67 na kwa Tanzania ni asilimia 47.
“Unaweza ukaona pamoja na maneno kwamba deni la serikali linaongezeka lakini utaona Tanzania kuna utofauti mkubwa, na hii ni kielelezo kuwa Serikali ya awamu ya sita inasimamia vizuri hali ya uchumi.
“Tunapokwenda kutengeneza dira hii tunatamani Watanzania watafakari ni aina gani ya uchumi wanaoufikiria ni kipi kitaweza kufikisha huko. Tunafikiri kwamba kwa miaka 25 ijayo tuwe na uchumi ambao ni sawa na Nchi 15 kubwa duniani… tafsiri ni lazima tuongeze ushiriki wa sekta binafsi kufikia hayo matarajio,” amesema na kuongeza:

“Uchumi wenyewe ni takribani dola Bilioni 85, kwahiyo ukifikiria kujenga uchumi wa Dola Trilioni 1 unafikiria kuongeza takribani mara 12. Hatuwezi kufikia huku kama hatuwezi kubadilika kwa kile tunachokifanya,” amesema Kafulila.
Amebainisha kuwa Mdahalo huo ni sehemu ya kujenga uelewa kwa wananchi kuhusu masuala ya ubia na kuweza kutafakari kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

“Hii ni fursa kubwa ya kujadili namna ambavyo tunataka kuwa na uchumi wa nchi yetu kwenda mwaka 2050. Lazima kufungua uchumi kwa kuongeza ubia sekta za ndani na nje kushiriki katika kujenga uchumi na serikali ipo tayari kushirikiana na sekta binafsi katika kuimarisha uchumi wa nchi,” ameongeza.