Na Mwandishi Wetu
Kikosi Maalumu cha Kuzuia Magendo Zanzibar (KMKM), kimempandisha cheo mchezaji wetu Ibrahim Hamad “Ibra Bacca” kutoka Koplo na kuwa Sajenti kutokana na kuonesha kiwango bora Uwanjani.
Akizungumza baada ya kupandishwa cheo hicho, amesema anakishukuru kikosi chake kutokana na sapoti wanayoitoa kwake kila sehemu anayopita na kuahidi kuendelea kuitumikia nchi yake.
“Sina budi kushukuru kikosi changu kwa kuweza kunisapoti kwa kila hatua. Nitaendelea kuipambania nchi yangu,” amesema Sajenti Ibrahim Bacca ambaye wazazi wake pia ni askari.
Beki huyo alisajiliwa na Yanga msimu wa 2022/2023 kutoka KMKM ambacho ni kikosi cha ulinzi cha Zanzibar ambacho kina jukumu la kulinda mipaka ya bahari dhidi ya magendo, uvuvi haramu, na vitendo vingine vya kihalifu. Pia, KMKM husaidia katika operesheni za uokoaji baharini na usalama wa majini.