Mwanzoni mwa wiki hii iliibuka habari kubwa iliyotokana na tamko la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Sululu Hassan, kwamba Tanzania ilikuwa inaingia mkataba wa kuuziana umeme na Kenya. Kwamba maandalizi ya mkataba huo yalikuwa katika hatua za mwisho. Mkataba huo unahusu Kenya kuiuzia Tanzania umeme kwa ajili ya mikoa ya kaskazini mwa Tanzania. Hii ni mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara.
Habari hii ilizua mijadala mikubwa kwenye mitandao ya kijamii. Sababu kubwa ya mjadala huo ni kile kilichokuwa kinahojiwa. Je, baada ya taifa kutangaziwa kwamba Bwawa la Mwalimu Nyerere lenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115 kuwa lilikuwa limekamilika kwa karibia asilimia 99 na ushei, kwa nini tununue umeme nje? Kukamilika kwa bwawa hili kulikuwa kunahitimisha ahadi za serikali kwamba nchi itakuwa na umeme wa kutosha kwa matumizi ya humu ndani, lakini pia ziada ya kuuza nje. Kwa hiyo Watanzania walijua kuwa sasa taifa lao litakuwa linauza umeme nje na siyo kununua. Hii ndiyo imekuwa chanzo cha mijadala hiyo.
Hata hivyo, serikali haikukaa kimya baada ya kuona mjadala huo. Makatibu wakuu wawili, wa Nishati, Felchesmi Mramba na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa ambaye pia ni msemaji mkuu wa serikali, walitoa taarifa ya ufafanuzi juu ya uamuzi wa serikali kununua umeme kutoka Kenya. Kimsingi umeme huo ijapokuwa unanunuliwa kutoka Kenya, ni umeme unaozalishwa Ethiopia, ambayo ilifanikiwa kujenga Bwawa kubwa la umeme kuliko yote barani Afrika, Grand Renaissance Dam, lenye uwezo wa kuzalisha Gigawati 5.15. Bwawa hili ni la nane kwa ukubwa duniani.
Katika maelezo ya serikali sababu kubwa inayosukuma kununuliwa kwa umeme kutoka Kenya ni kuongeza nguvu kwenye gridi kwa upande wa kaskazini. Kwamba kutokana na masafa marefu ya kusafirisha umeme (transmission) zaidi ya km 700 kutoka kwenye vyanzo ambavyo viko kusini mwa ukanda huo, husababisha upotevu mkubwa wa umeme. Upotevu huu, kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Msigwa unasababisha hasara ya walau Sh. bilioni 32 kwa mwaka. Mramba alitoa ufafanuzi akisema kwamba gridi ya taifa ya umeme kwa upande wa kaskazini, ni dhaifu sana. Kuna shida kubwa ya umeme kuwa mdogo (low voltage) na kwamba mipango ni kununua umeme kutoka Kenya kupitia Namanga kiasi cha megawati 100, ambao utasaidia kuboresha hali ya nguvu ya umeme kwa ukanda huo.
Ni vigumu kupinga masuala ya kitaalam yanapokuwa yanatolewa kwa mfano na mtu kama Mramba. Huyu ni injinia wa umeme. Amekaa na kukulia Tanesco mpaka kuwa Mkurugenzi Mkuu. Anaujua umeme. Anaijua Tanesco. Anaijua gridi ya taifa ya umeme kama kiganja chake. Anapozungumza mtu wa aina hiyo kuhusu shida ya upatikanaji wa umeme wa kuaminika kanda ya mikoa ya kaskazini, huwezi kumkatalia tu au kumbishia tu. Kwa maana hiyo, inawezekana mkataba wa kununua umeme kutoka Kenya, ambao kimsingi ni kutokana na nguvu ya Ethiopia unaelezeka, ni suluhisho sahihi.
Hata hivyo, inatupasa kujitafakari kwa kina kama taifa juu ya mifumo yetu ya kusafirisha umeme. Kwa kauli ya Mramba mwenyewe, gridi ya taifa kwa upande wa kaskazini ni dhaifu sana. Sasa haieleweki ni dhaifu kwa sababu ya umeme mdogo, au ni dhaifu kwa sababu ya uchakavu na uwezo mdogo wa mfumo kwa ujumla wake. Yawezekana kwamba umeme mdogo ndiyo chanzo, na kwamba masafa ya kuusafirisha zaidi ya km 700 ndiyo chanzo kikuu cha udhaifu huo.
Hapa kuna sababu ya kujifikirisha kidogo. Kenya ambao watakuwa wanatupa umeme wa megawati 100 wanapata uwezo huo kwa sababu upo umeme unaingizwa kwenye gridi yao kutokea Ethiopia. Kwa maneno mengine, gridi ya Kenya haiwezi kuwa na nguvu kubwa ya kutoa hizo megawati 100 kwa Tanzania, kama haitakuwa na nguvu ya kupokea na kuusafirisha umeme huo kwenye mfumo wa gridi yao. Yaani Kenya bila Ethiopia hawana ziada ya megawati 100 za kuuzia Tanzania.
Kinachosumbua akilini ni kitu kimoja, je, hatuna uwezo wa kuimarisha mfumo wetu wa gridi ili kupunguza upotevu wa umeme? Kama upotevu ni mkubwa kiasi cha kuzidi gharama za kununua umeme nje ya nchi, hili ni suala linalohitaji tafakari ya kina zaidi. Kwamba km 700 ni changamoto kubwa katika upotevu wa umeme hivyo nafuu ni kununua umeme? Yaani hatuwezi kukabiliana na udhaifu wa gridi? Dunia inajua kwamba Marekani inapokea umeme mwingi sana kutoka Canada. Ni wangapi tumejiuliza ni umbali gani umeme ule unasafirishwa? Canada wanasafirisha umeme kwenda Marekani kwa umbali wa km 1,522.
Umeme wa Canada ni biashara kubwa wanayofanya na Marekani. Ni biashara ya matrilioni ya Dola za Marekani kila mwaka. Canada wakizima umeme unaokwenda Marekani ni hakika watakuwa katika hali mbaya kwa sababu asilimia kubwa ya umeme unaotumika Marekani unatoka Canada. Kwa mwaka 2023 Canada waliiuzia Marekani umeme wa megawati milioni 35.8. Umeme huu unapita masafa hayo hapo juu, zaidi ya km 1,500. Sisi km 700 zimekuwa za hasara, ngumu, haiwezekani kutatua changamoto ya upotevu, dawa ni kununua umeme!
Mramba katika kauli yake kwa umma, alisema kanda ya kaskazini ambayo kwa jiografia ya Tanesco ni pamoja na mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Mara na Mwanza, ina uhitaji wa megawati 300. Kwa maana hiyo, megawati 100 zitakazoingizwa kwenye gridi kwa upande wa kaskazini, zitaamsha gridi hiyo, hivyo kuonda tatizo sugu la low voltage.
Tujikumbushe kitu kimoja muhimu hapa. Sekta ya nishati ya umeme nchini inajulikana kwa figisufigisu nyingi ambazo mwisho wa yote ni uwapo wa upigaji mkubwa sana katika miradi mingi ya umeme. Hakuna ambaye hakumbuki shughuli ya IPTL ambayo ilitafuna taifa hili kwa zaidi ya miongo miwili. Hakuna ambaye hakumbuki mikataba ya kuuzia Tanesco umeme (Power Purchases Agreement) ambayo iliinyonya ‘damu’ ya kutosha Tanesco. Bado kuna suala la bomba la gesi asilia lililojengwa kwa mabilioni ya fedha, lakini pia tunaambiwa kuna mambo hayajakaa sawa kwa gharama ya gesi kwa Tanesco. Mizigo yote hii ya mikataba ya kuuzia Tanesco umeme huwa inabebwa na watumiaji wa umeme huo, wananchi. Watanzania.
Ni vema kutambua kwamba walau kwa sasa Tanesco imeachana na mikataba karibia yote ya kuuziwa umeme. Tanesco imesimama peke yake, ukiacha habari ya gesi ambayo siyo mali yake, lakini pa kubwa sana ile mikataba iliyokuwa imeikongorowa Tanesco imeondoka. Ikumbukwe kwamba mikataba yote hiyo ilikuwa halali kwa sababu ilifungwa kihalali kwa sheria za Tanzania na za Kimataifa, lakini haikuipa Tanesco fursa ya kupumua. Ilikuwa ni mizigo.
Mawazo ya wengi kwa kitambo sasa yamejengwa kwenye dhana na sasa uhalisia kwamba madhali Bwawa la Mwalimu Nyerere limekamilika, ya nini sasa kuingia kwenye mipango na mikataba ya kununua umeme? Kwa nini tusiimarishe uwezo wa gridi ya taifa? Kukimbilia kununua umeme inawezekana kabisa tunakwenda kufungua ‘jini kutoka kwenye chupa’. Tunajua serikali ya awamu ya tano, ilifikisha mwisho mikataba yote ya kuuzia Tanesco umeme. Sasa nini kinatuvuta huko?
Nionavyo mimi, dhana kwamba kuna umbali mrefu sana kutoka vyanzo vya umeme mpaka mikoa ya kaskazini, ni dhaifu mno. Nafikiri uimarishaji wa gridi ya taifa ili kupunguza upotevu wa umeme njiani, ndiyo ingekuwa suluhu ya jambo hili.
Kama hatutafanyia kazi udhaifu wa gridi, ina maana kwamba hata tutakapoamua kuuza umeme Zambia kwa mfano, itakuwa kazi ngumu kwa sababu utakuwa wa bei ya juu sana kwa sababu hatuna uwezo wa kuusafirisha umeme wetu kwa masafa marefu. Kwanza hatuwezi kukaa hapa na kuaminishana eti kutoka Bwawa la Mwalimu Nyerere mpaka Tunduma mpakani na Zambia ni karibu; au kutoka Bwawa la Mwalimu Nyerere mpaka Malawi ni karibu. Hakuna kokote ambako ni karibu.
Hakuna siku serikali imesema mkataba fulani wa kuzalisha au kuuziana umeme inaokwenda kuingia ni mbaya, lakini matokeo mara nyingi yamekuwa kinyume chake. Aliyegongwa na nyoka akiona unyasi hushtuka!