KUNA kila dalili kwamba taifa letu kidogokidogo linakumbwa na hali ya kutokuaminiana. Hali hii ni kama inazidi kuongezeka kila uchao. Yapo matukio mengi ambayo yametokea nchini, hasa ya kupotea au kuuawa kwa watu, ambao maelezo yanayotolewa ama yanaibua hisia hasi kutokana na jinsi yanavyopokewa.
Katika dunia tunayoishi leo, mitandao ya kijamii ni nyenzo mojawapo ya mawasiliano. Ni nyenzo ambayo kwa sasa imeshika kasi kubwa sana katika kupashana habari. Nyenzo hizi zimekuwa pia ni mojawapo ya kipimo cha kutaka kujua hisia za jamii juu ya jambo linalotokea. Mitandao ya kijamii siyo tu inatoa fursa kwa jamii kuwasiliana kwa uhuru bila hofu ya kutishwa, bali pia imefungua milango ya kuamsha uwajibikaji.
Katika muktadha huu, Jumatatu wiki hii, taarifa juu ya kupotea na hatimaye kupatikana kwa mwili wa Mfanyabiashara wa Jijini Dar es Salaam, Daisle Simon Ulomi, zilizagaa katika mitandao ya kijamii. Habari za awali za kupotea kwa Ulomi zilikuwa zimetolewa na familia yake kwamba alikuwa hajaonekana nyumbani kwake tangu Desemba 11, 2024 yaani Jumatano ya wiki iliyopita. Baada ya kelele nyingi na maombi ya wanafamilia ya kutaka msaada wa kupatikana kwa Ulomi kutanda sana kwenye makundi ya mitandao ya kijamii, Jumatatu, Desemba 16, 2024 ndipo zilipatikana taarifa kwamba mwili wake ulikuwa umepelekwa kwenye chumba cha maiti cha Hosipitali ya Mwananyamala ukiwa unatokea kituo cha afya cha Makuburi.
Taarifa za ziada zinasema kwamba Ulomi alipata ajali ya bodaboda. Hata hivyo, hakuna taarifa za kina zinazoshikamanisha simulizi yenye mtiririko ili kusaidia kujua kwa undani alipata ajali akiwa na nani, alipelekwa na nani kituo cha afya cha Makuburi, kuna pengo kubwa la taarifa juu ya kifo chake.
Tukio la kupotea na hatimaye kukutwa kwa mwili wa Ulomi ukiwa chumba cha maiti, linaongeza mfululizo wa matukio ambayo hayajapata majibu ya kupotea na kuuawa kwa raia wa nchi hii katika mazingira ya kutatanisha. Kwa mfano, hadi leo hakuna taarifa za kipolisi za uchunguzi juu ya kuuawa kwa aliyekuwa kiongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Ali Kibao, aliyekamatwa na watu waliodhaniwa kuwa ni askari na kisha siku moja baadaye mwili wake ukakutwa umetupwa huku uso wake ukiwa umeharibiwa vibaya kwa tindikali.
Rais Samia Suluhu Hassan alitoa salamu za rambirambi kwa viongozi wa Chadema na kutaka kufanyika kwa uchunguzi wa mauaji hayo, lakini hadi sasa tangu Septemba hakuna taarifa zozote za kina zimetolewa kuhabarisha umma ni nini hasa kilimsibu Kibao na wahusika wa mauaji hayo ni akina nani.
Katika mfululizo wa matukio ya kutekwa, kupotea na kuuawa kwa watu, ambayo yamekuwa mengi katika siku za hivi karibuni, vyombo vya usalama ambavyo vinapaswa kutoa majibu ya kukidhi kwa wananchi juu ya madhila haya, ama vimekuwa vikitoa maelezo ambayo yanaacha maswali mengi, au pangine hakuna maelezo kabisa yanatolewa. Kwa mfano, hadi leo umma haujaelezwa waliko Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (BAVICHA) wilaya ya Temeke, Deusdedith Soka. Anayedaiwa kutekwa pamoja na Jacob Mlay na Frank Mbise, watatu hawa wanadaiwa kukamatwa baada ya kuitwa kwenda kituo cha polisi Temeke kufuatilia pikipiki ya Soka iliyokuwa imeibwa. Pia mpaka leo, vyombo vya usalama havijatoa maelezo yoyote ya kukidhi kiu ya wananchi kujua waliko watu zaidi ya 80 ambao waliorodheshwa na Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) ambao ama wametekwa, wamepotea au kuuawa.
Matukio haya ambayo kila uchao yanaibua maswali mengi magumu juu ya usalama wa wananchi, yanapokosa majibu ya kina, basi kidogokidogo wananchi wanazidi kuongeza shaka yao juu ya kila wanachoelezwa hasa kinapokuwa kinaonekana kuwa na mapengo mengi. Wiki iliyopita katika safu hii nilitafakari tukio la wananchi kushambulia gari lililodaiwa ni la wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambalo lilisababisha kifo cha mmoja wa watumishi hao, Amani Simbayao. Nilisema isije kuwa wananchi wameanza kuchoka kusikia maelezo yasiyokidhi kiu yao juu ya matukio ya kihalifu yanayotokea katika maeneo yao na hivyo sasa wameamua kujihami kwa kuwa imani yao kwa walinzi wa usalama inazidi kuporomoka.
Leo tena umma unapewa maelezo ya kifo cha Ulomi katika mazingira ambayo yanazidi kuongeza wasiwasi na shaka kwao. Nilipata kueleza katika safu hii huko nyuma kwamba amani ya taifa letu ni matokeo ya kazi kubwa ya kujenga jamii inayojali haki za watu, inayoheshimu utu wa watu, lakini la muhimu zaidi inayojengea kila mmoja matumaini chanya juu ya kesho yake.
Kadri siku zinavyokwenda hasa hasa tangu mwaka 2016 tumeona tukiotesha mizizi ya kumomonyoa matumaini haya. Ingawa tangu mwaka 2021 hali ilianza kutengamaa, tukaanza kuona nuru, katika siku za hivi karibuni wimbi jingine kubwa la kupotea na kuuawa kwa watu katika mazingira tatanishi, limeturejesha tena nyuma. Nyuma kabisa. Kuna dalili kwamba nchini sasa kuna magenge yanayojiendeshea mambo yao watakavyo kana kwamba wako juu ya sheria. Tunaona kutokujali kwa kiwango cha juu kabisa kwa walinzi wa amani hasa umma unapopiga yowe juu ya uhalifu wa kupotezwa au kutekwa kwa watu.
Kinachosumbua zaidi ni kuona kwamba kila tukio la kutekwa, kukamatwa na hata kuuawa kwa raia linapotokea, wahusika wenye wajibu wa kuwapa wananchi majibu ya sababu za hali hii na wahusika ni akina nani, ni kama hawasumbuki kwa kuwa wanajipiga kifua wakisema ‘watapiga kelele siku chache, halafu watanyamaza.’ Hali hii imefisha kabisa uwajibikaji, lakini wakati huo huo inakuza hali ya kutokuaminiana katika jamii.
Tunakumbuka Rais Samia alipoingia madarakani alisema amevunja vikosi kazi vyote, na akaagiza kila taasisi iliyoundwa kisheria itekeleze wajibu wake kama unavyofafanuliwa kwenye sheria zilizoziunda. Umma hauna hata chembe ya kutokumuamini Rais wao, ni kiongozi wao. Hii ilikuwa ni kauli ya matumaini. Sasa ni kitambo kimepita, swali kuu la kujiuliza ni nani huyo ambayo ana ubavu wa kupuuza maelekezo ya Rais? Ni kwa nini polisi wanakana kuhusika na matukio haya hata pale wanaodaiwa kuendesha utekaji na ukamataji ni watu wanakuja wakiwa na zana za wanausalama, wakiwa na magari yao, silaha zao na hata pingu? Ni nani mwingine amepewa mamlaka ya kushughulika na raia katika kusimamia utekelea wa sheria katika kudumisha usalama? Nawaza kwa sauti, hivi vikosi kazi (task forces) zimerejea kwa mlango wa nyuma?