ALHAMISI iliyopita yaani Desemba 5, mwaka huu wa 2024 lilitokea tukio baya la kuhuzunisha la wananchi kushambulia watu wanaodaiwa kuwa ni wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ambao walikuwa kwenye msako eneo la Tegeta jijini Dar es Salaam.
Katika tukio hilo la kusikitisha, inadaiwa wafanyakazi hao wakiwa kwenye gari lao walimlazimisha raia mmoja kusimama baada ya kuzuia gari lake kwa mbele. Raia huyo alikataa kushuka kwenye gari lake kwa kile alichodai kwamba hakuamini kwamba waliokuwa wanataka kumkamata walikuwa ni wafanyakazi wa TRA.
Kadhia hiyo iliishia kwa wananchi kuwashambulia wafanyakazi hao kwa silaha mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuharibu gari lao wakiwatuhumu kuwa ni watu ‘wasiojulikana’. Mashambulizi yalikuwa mabaya kiasi kwamba yalisababisha kifo cha mfanyakazi mmoja wa TRA ambaye alitambuliwa kwa jina la Amani Simbayao. Alikufa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili. Mungu ampe pumziko la milele.
Hili ni tukio baya kwa hali yoyote ile. Polisi nao wamesema kwamba wamekamata watu kadhaa kuhusiana na tukio hili. Pengine, sheria itachukuwa mkondo wake ili haki ipatikane kwa kila mmoja anayedaiwa kuhusika katika kadhia hii.
Hata hivyo, Watanzania kwa ujumla wetu tunapaswa kujiuliza maswali muhimu, kwa nini wananchi wameamua kujichukulia sheria mikononi mwao hata katika mazingira kama haya yaliyowakuta wafanyakazi wa TRA? Ni nini hasa kinawasukuma watu kuamua kujihami wenyewe? Ni kwa nini hawataki kwa mfano kuwaita polisi kuja kwenye tukio ambalo wanahisi kuna uhalifu unatendeka na badala yake wanaamua kujichukulia sheria mkononi?
Hakuna ubishi kwamba Watanzania kwa ujumla wao ni watu wa amani. Ni watu wanaosikiliza vyombo vya mamlaka. Ni watiifu, tena utii wao hauna masharti. Ndiyo maana kwa mfano polisi wakisema ni marufuku kuandamana, kweli watu wanatii. Hawandamani. Polisi wakisema jambo fulani lisifanyike, watu wanatii bila kuuliza. Watanzania kwa hulka siyo watu wagomvi, siyo watu wa kuzuia vyombo vya mamlaka kutimiza wajibu wao. Watanzania wanaaminiana na kuishi kwa amani na kila mmoja.
Pamoja na hulka hii ya Watanzania ambayo kwa hakika imejengwa kwa miaka mingi sana kiasi cha kuitwa ni utamaduni na tunu za taifa hili, kidogo kidogo kuna dalili na viashiria kwamba wamechoka kuendelea kuwa kama walivyo. Swali la kujuliza ni kitu gani hicho kinawasukuma kuanza kuhama katika utamaduni wao wa kuishi kwa kuaminiana na kwa amani?
Kwa sasa ndani ya nchi ipo hofu imejengeka juu ya kutekwa, kujeruhiwa na hata kuuawa kwa watu. Watekaji hawa hawajulikani ni akina nani. Wapo wanaokuja kwa sura ya askari polisi, wapo wanaokuja katika sura ya kiraia, lakini wakiwa wamejihami kwa silala na nyenzo nyingine za kudhibiti wahalifu.
Kwa mfano, aliyekuwa kiongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Ali Kibao, alikamatwa akiwa ndani ya basi la Tashriff akisafiri kwenda Tanga katika maeneo ya Tegeta. Waliomkamata wanadaiwa kuwa walikuwa na silaha ambazo hutumiwa na vyombo vya ulinzi vya ndani ya nchi. Watu hao walimfunga pingu Kibao wakashuka naye kutoka kwenye basi hilo, kisha wakaondoka naye. Walifanya hivyo baada ya kulizuia basi hilo mbele na nyuma, kama lilivyofanywa gari la Tegeta juzi. Siku moja baadaye mwili wa Kibao uliokotwa eneo la Ununio ukiwa umeharibiwa sana usoni kwa kumwagiwa tindikali.
Yapo matukio mengi ya watu kupotea. Kwa mfano Septemba mwaka huu wapo watu wengine waliopotea au kutekwa, hawa ni Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (BAVICHA) wilaya ya Temeke, Deusdedith Soka. Anadaiwa kutekwa pamoja na Jacob Mlay na Frank Mbise, watatu hawa wanadaiwa walikamatwa baada ya kuitwa kwenda kituo cha polisi Temeke kufuatilia pikipiki ya Soka iliyokuwa imeibwa.
Mwingine ambaye ametekwa na kuteswa kisha akatelekezwa ufukweni jijiini Dar es Salaam, ni Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana wa ACT-Wazalendo, Abdul Nondo. Nondo alikamatwa akiwa kituo cha mabasi cha Magufuli, Mbezi Luis alfajiri ya Desemba mosi mwaka huu, muda mfupi baada ya kushuka kwenye basi akitoka safarini mkoani Kigoma ambako alishiriki uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka huu.
Katika matukio yote haya polisi wamenyooshewa kidole cha lawama kwamba wanahusika na utekaji. Hata hivyo, Polisi wamekanusha kuhusika.
Ingawa polisi wamekanusha kuhusika na matukio haya, imekuwa ni vigumu kuelewa kama kweli wanafuatilia matukio haya kwa kutumia ujuzi na maarifa ya upelelezi wa kazi yao, ili wahalifu ambao wanazua taharuki katika jamii wadhibitiwe.
Wiki iliyopita polisi walitoa taarifa ya kukamatwa kwa watu wanne wanaodaiwa kuhusika katika jaribio la kutaka kumteka mfanyabiashara wa jijini Dar es Salaam, Deogratious Tarimo Novemba 11, 2024 eneo la Kiluvya. Watu hawa walikamatwa siku 23 baada ya tukio hilo kutokea ambalo picha za video zilisambaa katika mitandao ya kijamii zikiwaonyesha watu hao wakipambana kumwingiza kwa nguvu Tarimo kwenye gari dogo aina ya Toyota Raum, bila mafanikio.
Katika safu hii Septemba 9, 2024 niliandika uchambuzi uliobeba kichwa kisemacho “Samia hawa hawako nawe”. Ndani ya tafakari hiyo nilitaja viongozi wawili Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni na Inspeka Jenerali wa Polisi (IGP), Camilius Wambura, nikihoji kama wanawajibika vipi katika nafazi zao hasa baada ya kuwapo kwa taarifa za watu kutekwa na kuuawa. Nilifanya rejea ya orodha iliyokuwa imetolewa na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) ya watu waliokuwa wametekwa na kupotea.
Licha ya orodha ya TLS iliyotolewa Agosti 8 mwaka huu wa 2024 juu ya kutekwa na kupotea kwa watu hao wakiwa na orodha ya watu 83, Jeshi la Polisi ni kama halikusumbuliwa wala kutikiswa na taarifa hizo. Siyo Masauni ambaye sasa amehamishiwa Ofisi ya Makamu wa Rais kusimamia Mazingira, wala IGP Wambura aliyeonyesha kusumbuliwa na orodha hiyo.
Matukio haya kwa kweli ni vigumu sana kusadiki kuwa yanafanywa na raia tu wa hivi hivi. Na kama yanafanywa na raia wa hivi hivi tu, halafu inakuwa ni vigumu kwa vyombo vya usalama kujua ni akina nani wanaharibu nchi; Wanaharibu utulivu na amani ya nchi; Wanashusha hadhi ya serikali mbele ya wananchi na hata jumuiya ya kimataifa, inaleta shida kubwa kusadiki.
Hali hii inawafanya wananchi waanze kujiuliza maswali magumu kama serikali yao inaweza kuwa imepoteza uwezo wa kuwalinda. Wanajiuliza watu wanaopanga na kuendesha uhalifu mkubwa wa kiwango hiki na wasijulikane, wamepata wapi ujuzi wa kuvizidi maarifa vyombo vya usalama, kama Jeshi la Polisi?
Kama mawazo ya wananchi ni hayo, basi matukio ya wananchi kujichukuliwa sheria mkononi kwa kisingizio cha kujilinda yanaweza kuwa mengi na athari zake ni mbaya kama tukio la Tegeta ambalo mfanyakazi wa TRA ameuawa.
Ni vema kila mwenye dhamana ya kulinda usalama wa raia na mali zao afahamu kwa yakini kabisa, kwamba endapo wananchi watafikia hatua ya kuamini kwamba sasa jukumu la kujilinda dhidi ya hatari zozote ni lao, kwa kuwa labda vyombo vyenye mamlaka hayo ama vinaonekana kuvuta sana miguu kuwajibika, au inaonekana kana kwamba huenda vidole vingi sana vya lawama juu ya matendo ya utekaji na utesaji vinaelekezwa kwa vyombo hivyo, tunaweza kuanza kuona taifa tofauti kabisa na hili ambalo tumeishi kwa miaka 63 sasa. Tunaomba polisi wasitufikishwa huko.