Na Jesse Kwayu
WAZIRI Mkuu Mstaafu ambaye pia ni Jaji mstaafu, Joseph Warioba amesema ana wasiwasi kwamba amani ya Tanzania inaweza kutetereka kama hatua hazitachukuliwa kushughulikia matatizo yanayokabili mchakato wa uchaguzi Tanzania, huku akimuomba Rais Samia Suluhu Hassan achukue hatua kutatua matatizo yanayokabili uchaguzi nchini.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari leo Desemba 4,2024 jijini Dar es Salaam, Jaji Warioba amesema kuwa kwa bahati mbaya mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2024, yamejirudia matatizo yale yale ambayo yalishuhudiwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2019 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Amesema matatizo hayo yanatokana na serikali ya awamu ya tano, ambayo kwa mara ya kwanza ndiyo ilihusika kupoka haki za wananchi za kuchaguliwa kwa kutumia wasimamizi wa uchaguzi.
Ameeleza kuwa uzoefu ambao Rais Samia ameonyesha kushughulikia changamoto mbalimbali alizokutana nazo tangu aingie madarakani kama kurejesha mikutano ya vyama vya siasa, maandamano, kufungulia vyombo vya habari na kuendeleza mazungumzo kuhusu hali ya kisiasa, anaweza kabisha kutatua tatizo hili ambalo liliasisiwa wakati wa uchaguzi wa 2019 na 2020.
Jaji Warioba alitumia fursa hiyo kueleza histioria ya michakato ya uchaguzi zilizofanyika nchini tangu mwaka 1958 hadi sasa, na kueleza kwamba katika chaguzi zote zilifanyika huko nyuma, serikali ilikuwa inafanya tathmini ya changamoto zilizotokea na kuzifanyia kazi ili kulinda haki ya wananchi ya kuchagua na kuchaguliwa.
Amesema katika chaguzi zote serikali ilikuwa inasimamia haki za wananchi katika uchaguzi ila mwaka 2019 ndipo hali ilibadilika na serikali ikawa sasa ndiyo inasababisha wananchi kupoteza haki zao katika uchaguzi.
Katika mchakato wa uchaguzi, Jaji Warioba amesema kwamba taratibu ziliwekwa kwa anayegombea kuwa na fursa ya kuweka pingamizi kwa mgombea mwingine kama kuna ukiukaji wa taratibu, lakini sasa hali imebadilika kwani wale wanaopasa kulinda haki za wananchi kwa maana ya wasimamizi wa uchaguzi ndio wanaengua wagombea.
“Wagombea wanaenguliwa na wasimamizi siyo kwa sababu ya pingamizi za wagombea wenzao. Wanaenguliwa na wale waliotakiwa kulinda hazi za wananchi. Hawaenguliwi kwa hoja za msingi za haki za kikatiba na kisheria,” alisema.
Amefafanua kwamba baada ya kuwako kwa mijadala mingi ya kina baada ya matatizo ya uchaguzi wa 2019 na 2020 na kupitishwa kwa sheria ya uchaguzi, wananchi walikuwa na mategemeo ya kuona mabadiliko, hata hivyo, mwaka huu yametokea tena yale yale yaliyopita na chanzo chake ni wasimamizi wa uchaguzi.
“Kama tusipodhibiti hali hii ya kushindwa kulinda haki za wananchi tunaendelea kujenga mazingira ya kuleta vurugu ambazo zitaathiri amani nchini,” ameonya.
Hadi sasa anaamini maelezo ya serikiali juu ya matatizo yaliyotokea kwenye mchakato wa uchaguzi hayajitoshelezi na ni dhahiri wananchi hawawezi kuelewa inakuwaje upande mmoja tu ndiyo unakosea kujaza fomu za kugombea na mwingine ukipatia.
Ameeleza kwamba haiwezekani mgombea wa nafasi ya uenyekiti wa kijiji au mitaa akawa na uwezo wa kujaza kura bandia kwenye sanduku la kura, kazi hiyo inafanywa na wasimamizi wa uchaguzi.
Warioba amekitenga Chama Cha Mapinduzi na ukiukaji huu mkubwa wa uchaguzi akisisitiza kwamba: “Haya siyo matatizo ya CCM. Ni ya serikali.” Pia aliongeza kuwa aliyepewa kazi ya kusimamia uchaguzi uliopita hajatimiza wajibu wake, kwani hata pale Katibu Mkuu wa CCM alipoiomba serikali kuvumilia makosa madogo madogo ambayo yalitumika kuwaengua wagombea akiwa amekwisha kuwailiana na Mwenyekiti wa CCM ambaye pia ni Rais Samia Suluhu Hassan, tatizo halikutatuliwa.
“CCM kupitia Katibu Mkuu Nchimbi imeonyesha kutokukubaliana na kuenguliwa kwa wagombea, kura bandia, mauji na matumizi ya vyombo vya dola katika uchaguzi. Ametoa matamko na tumemsikia tatizo ni aliyepewa kazi ya kusimamia uchaguzi huu,” amesema.
Ingawa kisheria mwenye dhamana na Wizara ya Tawala za Miko ana Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ni Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, kwa kuwa TAMISEMI iko ofisi ya Rais, mamlaka ya kuendesha uchaguzi huo yamekasimiwa kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI ambaye ni Mohammed Mchengerwa. Mchengerwa amekuwa akisema kwamba uchaguzi ni suala la kisheria, kanuni na taratibu. Kauli ambayo Jaji Warioba anapingana naye kwa kuwa hoja kuu ni haki ya wananchi kikatiba.
Kadhalika ameonya juu ya matumizi ya vyombo vya ulinzi na usalama katika siasa, hasa Jeshi la Polisi. Alitoa angalizo kuwa polisi kama raia wana mataminio yao pia, hivyo kuwatumbukiza kwenye siasa wanaweza kusababisha kugawanyika jambo ambalo ni la hatari kwa usalama wa raia. “Serikali ndiyo inaingiza polisi katika siasa.”
Amelimwagia sifa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwamba ndiyo taasisi pekee imebaki yenye uaminifu, uadilifu, uzalendo na nidhamu ambayo haili kwa urefu wa kamba yake.
Ameonya kwamba kama hatua hazitachukuliwa sasa kutatua changamoto hizi ambazo zimejitokeza katika uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka huu, haoni kukiwa na mabadiliko yoyote kwenye uchaguzi mkuu mwakani kwani matatizo yatakuwa ni yale yale.
Katika kutafuta suluhu ya hali iliyoko sasa amesema anatambua kuwa uhusiano wa vyama vya siasa na serikali siyo mzuri, watu wamekata tamaa, chuki na uadui umeingia katika kuendesha siasa na kwa bahati mbaya watu hawaaminiani tena. Ameviomba vyama vya siasa kuweka mbele maslahi ya taifa na siyo ya kisiasa ili kupata ufumbuzi wa tatizo linalokabili taifa kwa sasa.
Amekumbusha kuwa CCM ina Baraza la Wazee ambalo linaundwa na wenyeviti na makamu wenyeviti wastaafu, huku akiwataja kwa majina, amesema wana uwezo mkubwa sana wa kusaidia kutatua changamoto ambayo iko mbele ya taifa kwa sasa.
Hata hivyo, Jaji Warioba amesema miongoni mwa suluhu ambazo hazina budi kutafutwa ni pamoja na mabadiliko ya katiba, ambayo mwanzoni Rais alionyesha nia ya kuendelea nayo, lakini baadaye ikaibuliwa hoja ya elimu ya katiba kwanza, jambo ambalo hajaona likifanyika mpaka sasa.
“Naona kama hakuna utashi wa kisiasa kuhusu mabadiliko ya katiba,” amesema huku akisisitiza kwamba kwa nyakati tulizo nazo hakuna namna ya kukwepa mabadiliko ya katiba kwani ni hitaji la lazima la kisiasa baada ya miaka zaidi 30 ndani ya mfumo wa vyama vingi vya siasa.