Na Winfrida Mtoi
Timu ya taifa ya kriketi ya wanaume ya Tanzania imeendelea kujiweka katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa wa mashindano ya kundi A ya Afrika kuwania kufuzu Kombe la Dunia la T20 baada ushindi wa wiketi tisa dhidi ya Cameroon.
Katika mchezo huo uliopigwa jana Septemba 24,2024 kwenye viwanja vya Gymkhana jijini Dar es Salaam, Cameroon ilianza kupiga mpira na kuishia kupata mikimbio 37 katika ova 12.1 huku wapiga mpira wote wa kikosi hicho wakitolewa.
Cameroon haikufanikiwa kuhimili mbinu za Tanzania wakati wachezaji wa kikosi hicho wakirusha mpira na hatimaye kushuhudia wapiga mpira wote wa Cameroon wakitoka mapema.
Abdoulaye Aminou alimaliza akiwa mpiga mpira mwenye mikimbio mingi katika kikosi cha Cameroon baada ya kupata mikimbio 11.
Alexis Balla alimudu kupata mikimbio sita na kuwa mchezaji mingine aliyetoa mchango katika idadi ya mikimbio ya kikosi hicho.
Warusha mpira wa Tanzania waliwachachafya vilivyo wapiga mpira wa Cameroon na kuwanyima fursa ya kupata mikimbio mingi.
Chipukizi Laksh Snehal aling’ara wakati kikosi cha Tanzania kikirusha mpira, ambapo alimaliza akiwa na wiketi nne.
Mchezo mzuri ulioonyeshwa na kinda huyo, wakati wa zamu ya timu yake kurusha mpira, ulimfanya achaguliwe kuwa mchezaji bora wa mechi hiyo.
Warusha mpira wengine Kassim Nassor, Sanjay Bom, na Harsheed Chohan, walizidi kuinyanyasa Cameroon, wakipata mikimbio miwili kila mmoja.
Tanzania haikupata tabu kuvuka idadi ndogo ya mikimbio ambayo Cameroon ilipata, ikimaliza zamu ya kupiga mpira mapema na kupata ushindi huo.
Timu hiyo, ikiongozwa na nahodha Abhik Patwa, ilipata mikimbio 38 huku ikipoteza wiketi moja katika ova tatu tu.
Chipukizi mwingine wa kikosi hicho Mohamed Omary alikuwa na mchezo mzuri wakati wa zamu ya kupiga mpira kwani alipata mikimbio 13 bila kutolewa.
Wapiga mpira wazoefu wa timu ya Tanzania- Patwa na Zafar Khan, waliihakikishia ushindi baada ya kupata mikimbio 12 kila mmoja.
Matokeo hayo yameifanya Tanzania kuendeleza wimbi la ushindi, ikiongoza michuano hiyo ikiwa na pointi sita.
Malawi, ambayo pia inafanya vizuri kwenye michuano hiyo, iko katika nafasi ya pili ikiwa pia ina pointi sita, ikitofautiana na Tanzania kwa uwiano wa mikimbio.
Ghana iko katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi nne,ikipata ushindi katika mechi mbili na kupoteza moja.
Cameroon inakamata nafasi ya nne baada ya kupata pointi mbili, zilizotokana na ushindi wa wiketi sita dhidi ya Mali katika mechi iliyochezwa Jumapili.
Timu za Lesotho na Mali hazijapata ushindi wowote mpaka sasa na hivyo kujikuta zikiwa katika nafasi mbili za mwisho.
Lesotho inashika nafasi ya tano wakati Mali inashika mkia.
Akizungumzia mafanikio hayo, Nahodha Msaidizi wa wa timu ya Tanzania, Kassim Nassor amesema walifanya maandalizi mazuri ya michuano hiyo na wapinzani wao walikuwa wazuri ila waliwazidi uzoefu.
“Nafasi ya kufuzu iko vizuri, tunategemea hizi mechi za kesho(leo) na keshokutwa. Mashindano yapo nyumbani hakuna sababu ya sisi kukosa kombe,” amesema Kassim.