HISTORIA ya maisha ya binadamu imeshuhudia pasi na shaka yoyote kwamba kujenga jambo lolote ni kazi ngumu inayohitaji juhudi na bidii katika kujituma. Kinyume chake, kubomoa ni kazi nyepesi sana. Jaribu kufikiria jengo kubwa la ghorofa ambalo huchukua miaka kadhaa ya kazi ngumu, kujituma na gharama kubwa kuikamilisha, lakini kwa kutumia bomu moja tu jengo kubwa la ghorofa ndani ya sekunde chache laweza kugeuka kuwa kifusi. Kujenga ni kazi ngumu, kubomoa ni kazi rahisi sana.
Tanzania ni taifa lililopata uhuru Desemba 9, 1961 sasa tunakaribia kushehereka miaka 63 ya uhuru. Huu ni umri wa kutosha, hata kwa mtumishi aliyeajiriwa ni umri wa zaidi ya kustaafu. Umri wa kustaafu kwa mujibu wa sheria nchini ni miaka 60. Katika umri huu wa miaka 63 ni hakika kazi kubwa na ngumu imefanyika. Kujenga taifa lenye umoja na mshikamano, kukuza amani, kulinda haki za kila mmoja, usawa wa kila mmoja mbele ya sheria, hivi ni vitu muhimu sana kwa ustawi wa watu hata kama hiviongezi sahani ya ugali mezani kwa mtu.
Kazi hii ambayo imefanywa kwa jasho na damu ya Watanzania, ilifika mahali ukawa ndiyo utamaduni wa nchi yetu – tunu yetu. Kwamba kila raia anajisikia huru kukaa, kwenda na kufanya lolote ilimradi havunji sheria. Kila mmoja alijiona kuwa ana haki ya uhai wake kulindwa na kutetewa na vyombo vilivyoundwa kisheria kufanya kazi hiyo.
Pamoja na utamaduni huu ambao ulijengwa kwa takribani miongo mitano na ushei, ilipofika mwaka 2016 kidogo kidogo umma ukashuhudia mambo ambayo kwa Tanzania yalikuwa ni simulizi kutoka mataifa mengine. Kutekwa, kuteswa na kuuawa watu bila kufuata taratibu za kisheria ambazo zimeainishwa katika mfumo wa utawala wa nchi hii.
Kidogokidogo hali hiyo ilianza mwaka 2016 kwa kile kilichopewa jina la watu wasiojulikana kuendesha matendo hayo maovu kinyume kabisa cha utaratibu wa utawala bora uliokuwa umeimarishwa kisheria katika nchi hii. Sehemu ya Tatu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungono wa Tanzania kuanzia ibara ya 12 hadi ibara ya 32, haki mbalimbali za binadamu zinazolindwa na katiba zimeainishwa.
Miongoni mwa haki hizo ni pamoja na haki ya usawa – kama usawa wa binadamu, usawa mbele ya sheria; haki ya kuishi – kama haki ya kuwa hai, haki ya uhuru wa mtu binafsi, haki ya faragha na usalama wa mtu, uhuru wa mtu kwenda atakako; haki ya uhuru wa mawazo – kama uhuru wa maoni, uhuru wa mtu kuamini dini atakayo, uhuru wa mtu kushirikiana na wengine na uhuru wa kushiriki shughuli za umma. Orodha ya haki hizi ni ndefu na imehakikishwa kikatiba.
Kwa kiasi kikubwa kabla ya 2016 haki hizi ziliheshimiwa, kulindwa na kuenziwa. Ni baada ya mwaka 2016 ghafla tukaona mwelekeo mpya wa utawala wa taifa letu. Mara watu wakaanza kutekwa na kupotezwa, mara watu wakatekwa wakateswa na kutelekezwa porini; kwa mara ya kwanza taifa likajazwa hofu, watu wakapoteza matumaini. Kile ambacho kilijengwa kwa jasho na damu kwa miaka 55 kikapigwa bomu kisha kikabomolewa. Ukajengeka utawala wa kiimla, utawala usiofuata sheria, mauaji ya watu wasiojulikana, pwani ya bahari ya Dar es Salaam ikawa ni dampo ya miili ya binadamu iliyofungwa kwenye viroba.
Hakuna hata kiongozi mmoja alitaka kusikia kelele na wito wa kufanyika kwa uchunguzi wa miili iliyokuwa inaokotwa kwenye pwani ya Dar es Salaam kila uchao. Hakuna kiongozi alijisumbua na miili hiyo. Miili ya binadamu ikapata hadhi kama mizoga ya wanyama. Hakuna aliyejali. Wapo waliokuwa wanatembea mitaani kwa mbwembwe kubwa wakijiona kwamba wako juu ya sheria hata pale kidole cha lawama kilipoelekezwa kwao.
Mwaka 2021 Machi, awamu mpya ya uongozi ikaingia madarakani. Umma ukahakikishiwa kwamba nchi imeingia katika mapambazuko mapya. Utekeji, utesaji na mauaji yakasita. Mwaka 2021, 2022 na 2023, kukawa na mwamko mpya. Hoja ya maridhiano ikapalizwa kila mahali. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, akaibuka na falsafa ya R Nne – Maridhiano (Reconciliation); Ustahimilivu (Resilience); Mageuzi (Reforms); Ujenzi mpya (Rebuild). Hizi R4 zikawa ndiyo dira ya Rais katika uongozi wake wa awamu ya sita. Hakutaka kushambulia moja kwa moja awamu ya tano. Hata hivyo, hotuba zake zikaonyesha anatamani nchi kurudi katika utamaduni wake- nchi ya amani, nchi ya utawala wa sheria, nchi ya kulinda haki za raia, nchi ya dola kufanya kazi yake iliyopewa na katiba.
Huenda Rais Samia alikuwa na nia njema sana ya kurejesha nchi katika utamaduni wake, katika ujenzi wake wa miaka 55 ya uhuru. Zipo hatua kadhaa zilizoonekana zikipigwa. Kubwa kwa ndogo.
Hata hivyo, kadri Rais anavyokuwa anajaribu kurejesha nchi kwenye ‘reli’ yake, ndivyo pia juhudi za chini chini za kumrejesha kwenye utawala wa kiimla zililivyoshika kasi. Matokeo yake ni hapa tulipofikishwa sasa. Sasa ni vigumu kujua kwa dhati kama kweli bado Rais amesimama na R4 na kama wapo wanaumuunga mkono ndani ya serikali yake.
Agosti 9 mwaka huu, mwezi mmoja sasa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kilitoa orodha ya watu zaidi ya 80 ambao ama wametekwa, kupotea au kuawa tangu mwaka 2016; TLS iliitaka serikali kufanya uchunguzi wa watu hao na kueleza umma wako wapi. Agosti 22 mwaka huu, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wakaibuka na orodha yao pamoja na kukubaliana na ile ya TLS, lakini wao wakaenda mbele zaidi kwa kuwaleta hadharani ndugu na jamaa ya watu waliotekwa, kuuawa au kuteswa kama mashuhuda wa hali ilivyo nchini.
Nchi ikiwa katika mtanziko huo, Agosti 18 mwaka huu ikatolewa taarifa nyingine kwamba viongozi wawili na mwanachama mmoja wa Chadema wilayani Temeke wametekwa na hawajulikani waliko. Viongozi hao walitajwa kuwa ni Mwenyekiti wa Vijana Wilaya ya Temeke, Deusdedit Soka na Katibu wa Wilaya, Jacob Mlay na mwanachama Frank Mbise.
Nchi ikiwa inasubiri majibu ya vyombo vya usalama kuhusu waliko Watanzania hawa, Septemba 6 mwaka huu zikazagaa habari kwamba Mjumbe Sektretariati ya Chadema Makao Makuu, Ally Mohamed Kibao, ametekwa, akapigwa pingu alipokuwa ndani ya basi la Tashrif akisafiri kwenda Tanga. Waliomkamata walikuwa na bunduki zinazotumiwa na majeshi ya Tanzania. Aidha, walifanikiwa kumteka Kibao baada ya kuzuia basi hilo mbele na nyuma kwa kutumia magari mawili yanayosadikiwa kuwa ni ya polisi. Mwili wa Kibao uliokotwa siku moja baadaye huko Ununio Dar es Salaam ukiwa umeharibiwa sana. Uso wake umeharibiwa kwa kumwagiwa tindikali.
Rais Samia ametuma salamu za rambirambi kufuatia mauaji hayo kwa familia na Chadema kwa kumpoteza kiongozi huyo. Aidha ameviagiza vyombo vya uchunguzi kumpelekea taarifa ya kina kuhusu tukio hilo baya na mengine ya namna hiyo kwa haraka. Amesisitiza Tanzania ni nchi ya kidemokrasia na kila raia ana haki ya kuishi na kwamba serikali anayoiongoza haivumilii vitendo vya kikatili vya namna hiyo.
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla, naye alitoa salamu za rambirambi za CCM kwa Chadema na familia ya Marehemu Kibao.
Pamoja na kila linaloweza kuelezwa, leo ni dhahiri wapo watu wamefanikiwa kumuondoa Rais Samia kwenye njia yake ya uongozi aliyoamua kuifuata. Wamefanikiwa kwa kurejesha taifa kwenye umwagaji wa damu. Wamefanikiwa kwa kuichafua na kuisiriba serikali yake kwa tope zito lenye harufu mbaya. Wamefanikiwa kumzingira na kumuacha peke yake na falsafa yake ya R4. Wamefanikiwa kurejesha nchi kwenye mfumo wa uovu, uhuni na chuki ambao uliasisiwa na kupaliliwa kidogo kidogo kuanzia mwaka 2016 na ilipofika 2021 ukawa umestawi vema.
Watanzania wote wana kila sababu ya kusimama na kusema kwa kauli moja, hapana, hapana, hapana, hatuwezi kuruhusu nchi yetu irejeshwe tena kwenye uchafu wa 2016 – Machi 2021. Tujiulize Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni na Inspekta Jenerali wa Polisi, Camilius Wambura tangu kengele iliyopigwa na TLS Agosti 9, mwaka huu kuhusu ujahili wa kuteka, kutesa na kuua watu walichukua hatua gani? Hivi wanajisikia vipi nchi inavyogaragazwa kwenye tope la kiwango hiki?


