NA EBENI MITIMINGI, MEDIA BRAIN
Taasisi tatu za umma kwa niaba ya Serikali ya Tanzania zimesaini makubaliano na Kampuni ya ESSA ya Indonesia kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa kiwanda cha mbolea aina ya urea, mradi utakaogharimu Sh.trilioni 3.24 za Kitanzania.
Taasisi zilizosaini makubaliano hayo mbele ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Prof.Kitila Mkumbo ni Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC).
Katika hafla ya kusaini makubaliano hayo iliyofanyika Jijini Dar es salaam Jumatano Julai 31, 2024, imebainishwa kuwa mradi huo utakapokamilika unatazamwa kama suluhisho la upatikanaji wa mbolea nchini kwani kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani milioni moja kwa mwaka.
Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Kilimo, hadi Aprili, 2024 upatikanaji wa mbolea nchini ulifikia tani 1,052,218.4 sawa na asilimia 123.95 ya makadirio ya mahitaji ya mbolea tani 848,884.
Hata hivyo kati ya hizo uzalishaji wa ndani ni tani 114,223 tu, sawa na asilimia 10.8. Kiasi kilichobaki cha tani 611,651.4 ziliingizwa kutoka nje ya nchi na tani 326,344 ni bakaa ya msimu wa 2022/2023.
Kujitosheleza kwa mbolea ni moja ya malengo ya Agenda ya 2030 inayotekelezwa na Serikali kupitia Wizara ya Kilimo ikilenga kuiwezesha sekta ya kilimo kukua kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030.
Profesa Mkumbo anasema licha ya kuwapo kwa mpango wa kiwanda hicho kuanza kazi ifikapo 2029, amezungumza na uongozi wa Kampuni ya ESSA kuharakisha utekelezaji ili kukiwezesha kukamilika mapema, na kwamba wahusika wamepokea ombi hilo.
“Mradi huu utatusaidia mambo mengi maana ikumbukwe kwamba asilimia 65 ya malighafi za viwanda vyetu zinategemewa kutokana na kilimo, hivyo hatua ya uzalishaji wa mbolea nchini itaongeza tija si tu katika kilimo, bali katika maendeleo ya viwanda vyetu,” anasema waziri huyo na kuongeza kuwa mradi huo ni matokeo ya ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan Januari mwaka huu nchini Indonesia.
Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Joel Laurent amesema kiwanda hicho kitamsaidia mkulima wa Tanzania kupata mbolea kwa bei nafuu na kuongeza tija kwenye uzalishaji huku akiweka wazi kuwa kumekuwa na ongezeko la matumizi ya mbolea katika siku za karibuni.
“Kiwanda kimekuja wakati mwafaka maana matumizi ya mbolea yanaongezeka, mwaka 2022/2023 matumizi yalikuwa karibu tani laki tano, msimu uliofuata 2023/2024 yakaongezeka na kwenda zaidi ya tani laki nane na kadri tunavyoendelea yanaweza kufika tani milioni moja,” anasema Laurent.
Anaongeza kuwa kiwanda hicho kitaiwezesha serikali kuokoa mabilioni ya fedha zinazotumika kuagiza mbolea kutoka nje ya nchi ambayo ni takriban asilimia 87 ya mahitaji pamoja na fedha zinazotumika katika mpango wa mbolea ya ruzuku kwa wakulima.
Kwa upande wake mwakilishi mkazi wa Kampuni ya ESSA, Abdallah Kitete anasema wataanza ujenzi wa kiwanda hicho mkoani Mtwara, mara tu watakapokabidhiwa gesi na maeneo ya kufanyia kazi na Shirika la Petroli nchini (TPDC).
Anasema ujenzi wa kiwanda hicho utafanyika kwa awamu tatu hadi kitakapokamilika na kwamba mahitaji yao ni kupata kiasi cha gesi ambacho ni mita za ujazo trillioni 70 kwa siku kwa miaka 20 mfululizo. “TPDC wamekubali kutupatia kiasi hicho cha gesi maana wanasema wana kiasi kikubwa cha rasilimali hiyo,”anasema Kitete.
Kitete anongeza kuwa kiasi cha tani milioni moja watakachoanza kuzalisha ni zaidi ya mahitaji ya nchi ambayo ni tani 850,000, hivyo kiasi kinachobaki ambacho ni tani 150,000 kitauzwa nje ya nchi na kuliingizia taifa mapato ya nje.