Kidata aligusa maslahi ya deep state?

MEI mwaka jana wafanyabiashara katika eneo la Kariakoo ambalo limepewa hadhi ya soko la Kimataifa waligoma. Mgomo wao ulitokana na kutokuridhishwa na mwenendo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) dhidi yao. Kwamba TRA walikuwa wakiwabambika kodi, kuwabugudhi na kimsingi walikuwa kero kwao kiasi cha kuwafanya washindwe kufanya kazi zao kwa uhuru. Vitendo ambavyo walidai vimevuruga biashara zao kiasi cha kuwakimbiza wateja wao, hasa wanaotoka nje ya nchi.

Katika mgomo huo kwanza aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla alikwenda kuwasikiliza ili kuwashawishi wafungue maduka yao, hakufanikiwa. Mgomo uliendelea na hatimaye ilimlazimu Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa, kwenda kuonana na wafanyabiashara hao mara mbili katika mikutano iliyoibua mambo mengi dhidi ya TRA.

Kwa bahati njema, ingawa katika mkutano wa awali na Waziri Mkuu hawakukubali kufungua maduka yao, mara ya pili baada ya mkutano wao uliodumu kwa saa kadhaa huku watendaji wanaohusika na kodi wakijibu maswali ya wafanyabiashara, maduka yalifunguliwa. Uamuzi wa kufungua maduka ulifikiwa kwa kuwa wafanyabiashara waliamini kwamba baada ya kuundwa kwa kamati iliyowajumuisha wao na serikali, basi kero zao zingelipatiwa ufumbuzi.

Hata hivyo, mwaka mmoja na ushei Kariakoo ile ile ‘imevimba’ tena. Wafayabiashara waligoma na safari hii mgomo wao ulipanuka zaidi kutoka Dar es Salaam na kuambukiza mikoa mingine saba. Nako wafanyabishara walifunga maduka.

Kwamba ni akina nani hao ambao wana nguvu kubwa ya kuweza kumsumbua Kamishna Mkuu wa TRA kiasi kwamba pona yake iwe ni kuondolewa tu kwenye nafasi hiyo? Hawa wana nguvu gani, kiasi kwamba hata kama Rais kweli ameridhishwa na utendaji wa Kidata, hawezi kumhakikishia ulinzi ili aendelee na kazi yake, isipokuwa salama yake ni kumuondoa hapo? Yaani Rais mwenye mamlaka yote ya dola, Rais ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama hana njia ya kumlinda mteule wake anayechapa kazi sawasawa kwa sababu tu anaandamwa na wasiopenda uwajibikaji wa mteule huyo? Kweli?

Jesse Kwayu

Wafanyabiashara hao walikuwa na malalamiko dhidi ya TRA. Walikuwa wanalalamika kwamba ukaguzi wa Risiti za Kielekroniki (EFD) na hesabu za kodi (return) uliokuwa ukifanywa na TRA ulikuwa unawaathiri kibiashara na kukimbiza wateja wao kutoka nje. Serikali kupitia Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, alitangaza kusimamishwa kwa ukaguzi huo wakati ukiandaliwa utaratibu mzuri wa utekelezaji wa suala hilo. Hata hivyo, maduka hayakufunguliwa mara moja.

Akimuapisha Kamishna Mkuu wa TRA mpya, Yusuph Mwenda, katika Ikulu ndogo ya Tunguu Zanzibar, Rais Samia Suluhu Hassan, bila kuhusianisha moja kwa moja uamuzi wa kumuondoa aliyekuwa Kamishna Mkuu TRA, Alphayo Kidata na sekeseke la wafanyabiashara eneo la Kariakoo, alisema tu aliamua kumuondoa TRA ili kumwepusha na mashambulizi ingawa kimsingi alikuwa anafanya kazi nzuri ya kukusanya mapato ya serikali. Kidata sasa amehamishiwa Ikulu kama mshauri wa Rais.

Rais wa Jamhuri ya Muungani wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inampa Rais mamlaka ya kumteua amtakaye kufanya kazi yoyote atakayo. Hakuna sheria inayoweza kutumiwa kuuliza kwa nini amemteua fulani au kumuondoa fulani katika nafasi yoyote. Hata ni mamlaka yasiyohojiwa. Ni mamlaka ya kikatiba.

Hata hivyo, uamuzi wa Rais wa kueleza mwenyewe bila kushurutishwa sababu za kumuondoa Kidata TRA na kumpa nafasi nyingine, kwamba ni kutokana na kuandamwa na kwamba aliona asisubiri mpaka ‘adate’ imeibua maswali mengi kwa yeyote anayesumbua ubongo wake kufikiri.

Kwamba ni akina nani hao ambao wana nguvu kubwa ya kuweza kumsumbua Kamishna Mkuu wa TRA kiasi kwamba pona yake iwe ni kuondolewa tu kwenye nafasi hiyo? Hawa wana nguvu gani, kiasi kwamba hata kama Rais kweli ameridhishwa na utendaji wa Kidata, hawezi kumhakikishia ulinzi ili aendelee na kazi yake, isipokuwa salama yake ni kumuondoa hapo? Yaani Rais mwenye mamlaka yote ya dola, Rais ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama hana njia ya kumlinda mteule wake anayechapa kazi sawasawa kwa sababu tu anaandamwa na wasiopenda uwajibikaji wa mteule huyo? Kweli?

Sina tatizo na aliyeteuliwa kurithi mikoba ya Kidata, sina sababu ya kumdhania kwamba hatafanya kazi nzuri, kwa sababu zipo taarifa zake nyingi zinazomshuhudia kuwa ni mtu makini na mchapa kazi. Kwa hivyo, ni wajibu wetu kama Watanzania kumtakia kila la kheri katika kazi yake mpya.

Ila, kwa uamuzi wa kumuondosha Kidata kama Rais alivyoamua kutueleza kwa wazi kwamba sababu ni kumlinda dhidi ya ‘watesi wake’ basi ajue tu ameamua kufungua ‘pandora box’ dhidi ya wateule wake wengi. Mteule yeyote anayeapa mbele ya Rais kwa kiapo cha utii na uchapa kazi, sharti alindwe kwa nguvu zote alimradi anatekeleza wajibu wake kwa mujibu wa sheria. Kama hawezi kuhakikishiwa ulinzi tutarajie majeruhi wengi mbele ya safari.

Safu hii inajukana kama Nyuma ya Pazia, kwa kuegemea jina hili, uamuzi wa Rais unaweza kuchukuliwa kwamba kuna mambo mengine makubwa yapo nyuma ya pazia ambayo umma haujui. Kwamba katika utendaji kazi serikalini yamkini kuna watu wasiogusika.

Ukiwagusa, kuna uwezekano wa wewe uliyewagusa hata kama uko sahihi kisheria na kikanuni, utakwenda na maji. Mwandishi George Orwell katika kitabu cha Animal Farm, kitabu cha siku nyingi- kilichapishwa mara ya kwanza mwaka 1945, kinatukumbusha habari ya watu wengine kuwa na haki zaidi ya wengine hata kama binadamu wote ni sawa.

Swali linalosumbua sasa ni hili, hawa wenye haki zaidi ya wengine katika nchi hii ni kina nani hasa ambao kimsingi wanaweza hata kumfanya mteule mchapaka kazi wa Rais akose ulinzi, isipokuwa tu salama yake ni kuondelewa kwenye nafasi yake? Na je, akishakuondolewa, ina maana hao ambao hawakumtaka watakuwa wameshinda? Watakuwa sasa hawana kipingamizi kuhusu mambo yao ambayo huenda Kidata alikuwa kizingiti kwao? Je, wataacha kuendelea na vita yao dhidi ya wateule wengine wachapa kazi? Je, hawa wana nafasi gani katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania? Je, hii ndiyo ile dhana ya ‘deep state’?

Wakati tukimtakia kila la kheri Mwenda, Kamishna Mkuu mpya wa TRA, ni wakati pia wa kutambua kwamba kazi ya kutumikia taifa ni wito wa kujitoa na kujikana, wale ambao wanaonyesha wazi kuwa na ujasiri wa kusimama katika kulinda na kutekeleza sheria ni vema wakalindwa ili kuwatia moyo.

Pia kwa kufanya hivyo tutasaidia kujenga uwajibikaji na kuvunja nguvu za magenge yanayojipanga kukwepa sheria, taratibu na kanuni za kuendesha taasisi za umma katika kuwatumika Watanzania, ambao wengi hawana hata uwezo wa kuepuka kulipa kila senti ya kodi inayolipwa kupitia bidhaa na huduma nyingine zitolewazo nchini.

spot_img

Latest articles

Soma Ripoti ya UHIFADHI WA UHAI: UKIUKWAJI WA HAKI ZA BINADAMU NDANI YA SEKTA YA UHIFADHI TANZANIA

Na Mwandishi Wetu, Media Brains Utafiti mpya umebaini kwamba mamlaka za serikali zimekuwa kichocheo kikuu...

RAIS DKT. SAMIA ATOA MAAGIZO KWA BASHE, NFRA KUNUNUA MAHINDI KWA WAKULIMA TSH 700 KWA KILO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassanamemuagiza Waziri wa Kilimo...

Upi upepo unaoweza kufika Tanzania,wa Wiliam Ruto au Paul Kagame?

KUNA upepo wa aina mbili unavuma katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mmoja...

Watu wawili wafariki, 16 wajeruhiwa katika ajali ya basi Songwe

Na Mwandishi Wetu, Media Brains Watu wawili wamefariki dunia na wengine 16 kujeruhiwa baada ya...

More like this

Soma Ripoti ya UHIFADHI WA UHAI: UKIUKWAJI WA HAKI ZA BINADAMU NDANI YA SEKTA YA UHIFADHI TANZANIA

Na Mwandishi Wetu, Media Brains Utafiti mpya umebaini kwamba mamlaka za serikali zimekuwa kichocheo kikuu...

RAIS DKT. SAMIA ATOA MAAGIZO KWA BASHE, NFRA KUNUNUA MAHINDI KWA WAKULIMA TSH 700 KWA KILO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassanamemuagiza Waziri wa Kilimo...

Upi upepo unaoweza kufika Tanzania,wa Wiliam Ruto au Paul Kagame?

KUNA upepo wa aina mbili unavuma katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mmoja...