WIKI iliyopita imekuwa ya harakati nyingi katika ukanda wa Afrika Mashariki. Kubwa ya yote ni kizazi kinachojulikana kama Generation Z kuingia barabarani nchini Kenya ili kuilazimisha serikali ya nchi hiyo kusikiliza kilio chao kuhusu ongezeko kubwa la kodi kupitia muswada wa fedha wa mwaka 2024 uliopendekezwa na serikali na kupitishwa na Bunge.
Kwa waliozoea siasa za Kenya siyo tu wamebaki vinywa wazi kwamba sasa nyakati zimebadilika na kwamba wanaoongoza maandamano siyo tena wanasiasa wakongwe waliozoeleka, bali ni vijana wenye umri wa miaka kati ya 11- 26. Hawa walizaliwa kati ya mwaka 1995 na mwaka 2010. Hawa wameleta mtikisiko mkubwa sana Kenya. Mtikisiko huu unataka kufanana na ule uliovuma kati ya miaka ya 2010 hadi 2013 ambao ulipewa jina la Arab Spring. Moto uliwaka katika nchi za Tunisia, Misri, Libya, Yemen na Syria.
Ukiacha Tunisia na Misri ambako kwa kiasi kikubwa umma ulijimwaga barabarani kwa amani na utilivu na hatimaye kusababisha kuondoka madarakani kwa marais wa nchi hizo, Libya, Syria na Yemen mtikisiko huo umeacha maafa makubwa yasiyoelezeka mpaka sasa.
Nchini Kenya, kwa kiwango kikubwa maandamano yamekuwa ya amani, ijapokuwa kuna vifo vimetokea. Hadi Jumapili idadi ya vifo vilivyokuwa vimeshuhudiwa ni kati ya watu 19 – 24, kulingana na vyanzo mbalimbali vya habari. Mtikisiko wa Kenya umebadili kabisa siasa za taifa hilo.
Dunia imeshuhudia Rais William Ruto, maarufu kwa jina la Hustler, akitoa hutuba mbili tofauti kabla ya kukutana na waandishi wa habari Ikulu kwa mahojiano maalumu juu ya hali iliyojitokeza nchini humo.
Katika hutuba za Rais Ruto alieleza uamuzi wake wa kukataa kusaini muswada wa fedha wa mwaka 2024 ili sasa uwe sheria baada ya kupitishwa na wabunge wengi wa chama chake. Kwa sasa muswada huo umerejeshwa bungeni kwa hatua zaidi, ama za kuubadili au vinginevyo. Bado mambo yamesimama kama yalivyo.
Maandamano ya wiki iliyopita nchini Kenya hayakuwa yakiongozwa na mwanasiasa yeyote, hayakuongozwa na kiongozi yeyote wa kikabila, wala hayakuongozwa na chama chochote cha siasa. Ni vijana walijiunga wenyewe kwa kile walichokuwa wanasema ‘Hapana Kwa Muswada wa Fedha wa mwaka 2024’. Vijana hawa waliwasiliana wenyewe kwa wenyewe kwa njia ya mitandao ya kijamii na kujaa kama utitiri karibu katika miji yote mikubwa ya Kenya. Walijaa Nairobi, Nakuru, Eldoret, Kisumu, Nyeri, Kitengela na miji mingine mikubwa ya nchi hiyo. Nchi ilisimama.
Akihojiwa na jopo la waandishi wa habari nchini humo, Rais Ruto mbali ya kukataa kukubali kwamba serikali yake ndiyo chanzo cha hali iliyotokea nchini humo, alisema kuwa tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana halijazalishwa na serikali yake. Alisema kuwa hali hiyo inajulikana kwa miaka mingi, na hadhari nyingi zimekwisha kutolewa kwamba kama hali hiyo haitashughulikiwa ni bomu linaloweza kulipuka wakati wowote.
Kenya kama ilivyo kwa nchi nyingi za Afrika zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara, zinafanana kwa changamoto ya idadi ya watu. Kwa mfano wakati idadi ya watu wenye umri kati ya miaka 0-14 kwa Kenya ni asilimia 37 ya idadi yote ya watu inayokaliwa kuwa ni milioni 56.2, kwa Tanzania ambayo ina idadi ya watu milioni 61 walioko kati ya umri wa miaka 0-14 ni sawa na asilimia 40.8 ya watu wote. Kwa watu wenye umri chini ya miaka 35 Tanzania ni asilimia 77.8 ya watu wote, wakati Kenya walioko chini ya miaka 35 ni sawa na asilimia 80 ya wakazi wote wa nchi hiyo. Kwa maneno mengine sura ya idadi ya watu Tanzania na Kenya haitofautiani sana, na kimsingi ndiyo sura halisi ya nchi nyingi kusini mwa Jangwa la Sahara.
Kwa hali hiyo, kinachowakumba vijana wa Kenya kwa kiasi kiubwa kinawakumba pia vijana wa Tanzania, kama ilivyo wa Uganda au Rwanda au Burundi au Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Suala la ukosefu wa ajira kwa nchi za ukanda huu, au tusema Afrika kwa ujumla ni kilio kinachofanana. Mamilioni ya vijana mwaka baada ya mwaka wanamwagwa mitaani wakiwa wanatoka masomoni katika ngazi mbalimbali, kuanzia sekondari, vyuo vya kati hadi vyuo vikuu. Wote ni wageni wa ‘kutembeza bahasha za kaki’ zenye barua na wasifu wao wakitafuta ajira ambazo siyo zimekuwa adimu sana, bali pia zinapatikana kwa kujuana sana. Kwa kifupi ajira hakuna.
Maisha ya watu wetu katika nchi hizi yanafanana sana. Vijana wanaambiwa wajiajiri. Wajitafutie ajira. Wanaambiwa wawe wabunifu. Wanaoongoza kwa kutoa ushauri huo ni waliokalia ofisi za umma ama za kuchaguliwa, kuteuliwa au kupeana. Ukisikia ushauri huo unatoka kwa watu wanaolipwa mshahara na kodi za wananchi, wanaotumia magari ya kifahari ambayo yamenunuliwa na yanaendeshwa kwa kodi za wananchi, na wao mwaka baada ya mwaka wanajirundikia maslahi manono wao na wenza wao.
Kilichogomba Kenya ni muswada wa fedha wa mwaka 2024 ambao umejaa kodi zinazoumiza watu wa kipato cha chini. Kodi kwenye mkate, mafuta ya kula, mawasiliano ya simu na mambo kama hayo ambayo kwa ujumla wake yanakwenda kufanya maisha ya wahangaikaji, wasaka unga wa kila siku kuishi maisha ya shida na adha kubwa zaidi. Rais Ruto awali hakuwaza kwamba hali ya ‘uasi’ wa umma wa Gen-Z ungeliweza kuisimamisha nchi kwa kiwango hicho. Ndiyo maana aliamua ‘kuwapotezea’ mpaka walipoamua kumuonyesha kwamba hata bunge lake linaweza kufurumushwa.
Kuna somo tumepata kutoka kwa majirani wetu Wakenya. Kwamba shida za vijana wa Kenya na Watanzania zinafanana. Kwamba adha ya kijana wa Kenya ni ile ile ya kijana wa Kitanzania. Hakuna ajira, kukata tamaa, kupuuzwa, kudanganywa mwaka baada ya mwaka na wenye madaraka, kushuhudia upendeleo machoni pao juu fursa zinazojitokeza ambazo zinagawanywa kwa mtindo wa upendeleo mkubwa wa kujuana. Matumizi mabaya ya rasilimali za taifa kwa walioaminiwa kuzisimamia.
Si jambo la kustaajabisha kuona kundi hili la vijana likiwa sasa limeaminishwa kwamba shughuli ya kuendesha bodaboda ndiyo ajira, kwamba umachinga wa kutembea na bidhaa juani, kwenye mvua mwaka baada ya mwaka ndiyo ajira. Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenye ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2020-2025 inasema itatengeneza ajira milioni 8. Hizi ni fursa na nafasi nyingi. Ni sawa na kusema kwamba kila mwaka zinatengenezwa ajira milioni 1.6. Kimsingi hizi ni ajira nyingi. Kwa sasa inakadiriwa kuwa kiasi cha vijana milioni moja wanamwagwa mitaani kutoka ngazi mbalimbali za elimu kila mwaka. Kama kweli, malengo ya CCM yatatimia, au kama yanatimia basi hali tunayoshuhudia katika miji mingi ya nchi hii, vijana wanaohangaikia ajira isingelikuwapo.
Ni kwa kutafakari hali hii na kutupia jicho Kenya tunapaswa kujiuliza kwamba je, Tanzania haina Gen-Z wake? Nao wanaweza kufanya nini katika hali hii ya kukata tamaa na kujiona walimeachwa pembezoni mwa meza ya kufaidi matunda ya uhuru na uchumi wa nchi yao? Tunahitaji tafakari na hatua za maana sasa kwani ugonjwa wa Gen-Z wa Kenya unaambukiza kwa kasi kuliko hata ilivyokuwa Arab Spring ya miaka ya 2010.