Watawala wetu wametumbukia kwenye ulevi wa uvivu wa kufikiri

Inajulikana wazi kuwa mabasi ya mwendokasi DART yanatoa huduma kwenye barabara kuu ya Morogoro kutoka Kibaha/Mbezi/Kimara kwenda Posta, Kariakoo -Gerazani, na Muhimbili, lakini pia kuna mabasi mengine yanafika mpaka Morocco kupitia barabara ya Kawawa hadi makutano na Bagamoyo.

Ukitafakari hali ya usafiri huu unabaki na mshangao mkubwa kwamba hivi sisi tunaweza kufanya nini? Kwamba mabilioni ya shilingi yametumika kujenga mtandao wa barabara za mwendokasi, barabara yote kuanzia Kibaha Mpaka mjini kati – Posta Mpya, kipande cha kuingia hadi Kariakoo Gerezani, kisha daladala zote zikafukuzwa njia ya Posta – Ubungo- Kimara -Mbezi na Kariakoo – Ubungo – Kimara- Mbezi, ili kutoa fursa ya biashara ya ukiritimba kwa DART, yenye barabara zake bila kuingiliwa, lakini imeshindikana kabisa kuendesha shughuli hiyo kwa ufanisi uliotarajiwa. Yaani pamoja na ukirimba wote huo- barabara na abiria DART imeshindwa!

Tumesikia amepatikana mwekezaji kutoka nje ambaye atakuja kuendesha biashara ya usafiri wa abiria Dar es Salaam kupitia barabara za DART. Nimesikia na kuona watu wakishangilia. Wanashangilia anakuja mwekezaji kuendesha shughuli ya daladala! Tunashangulia.

Mwaka 1996 kulikuwa na malumbano makubwa nchini juu ya uamuzi wa kubinafsishwa kwa iliyokuwa ikiitwa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC). Leo ni miaka 28 tangu uamuzi ule ufikiwe ambao ulizaa iliyokuwa ikiitwa benki ya makabwela- NMB na NBC 1996. Kilio kilichokuwapo wakati huo kilikuwa ni hiki, kwamba NBC imeshindwa kujiendesha, inapata hasara, imekuwa kubwa sana kiasi cha kukosa ufanisi. Lakini, pia kulikuwa na taarifa kwamba katika kipindi kile ambacho yalikuwa yanafanyika mageuzi makubwa ya kiuchumi nchini, Tanzania ilikuwa inavutia wawekezaji kutoka nje baada ya kuachana na sera za kijamaa chini ya Azimio la Arusha. Sasa uchumi wa soko ulikuwa unataka mazingira sawa kwa wawekezaji kuja kuingia katika sekta ya fedha-benki.

Itakumbukwa aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Dk. Idris Rashid wakati anajenga hoja kuhusu udhaifu wa NBC, alisema kuwa madeni ya NBC yangekusanywa wakati huo kwa noti za Sh. 1,000, basi kama zingelipangwa moja juu ya nyingine zingefika juu ya kilele cha Mlima Kilimanjaro. Hiyo ilikuwa ni lugha ya picha iliyokuwa inawasilisha ujumbe kwamba, NBC ilikuwa ‘mfu’ kifedha na kwa maana hiyo isingeliweza kuendelea kama ilivyokuwa.

Leo miaka 28 baadaye umma unajua NBC iliyobinafsishwa ili kujengewa uwezo mkubwa zaidi huku MNB ikiachwa hoi, picha ya sekta ya benki inashuhudia vipi juu ya dhana ile. Kwamba hakuna kinachowezekana kwa mikono yetu wenyewe? NMB imewezaje? 

Mwaka jana tuliona taharuki kubwa juu ya DP World kupewa mkataba wa kuendesha Bandari ya Dar es Salaam, sababu kubwa iliyojengewa hoja ni ‘sisi Watanzania’ kushindwa kuendesha bandari hiyo kwa ufanisi ulikusudiwa. Matokeo yake bandari haiingizi mapato ya kutosha kulingana na uwezo ambao upo ndani ya soko linalozunguka Tanzania. Yawezekana yote haya ni kweli.

Hata hivyo, swali kuu la kujiuliza ni hili, miaka 61 baada ya uhuru tunazidi kujenga uwezo wa kujiendesha wenyewe kama nchi, au ndiyo siku baada ya siku tunakuwa tegemezi?

Yaani leo Tanzania ina vyuo vikuu 49, kati ya hivyo 19 ni vya umma na 30 ni vya binafsi. Vyuo vya kati hapo navyo ni karibia idadi sawa na vyuo vikuu, yaani viko 47. Vyuo vyote hivi mwaka baada ya mwaka vinafyatua maelfu na maelfu ya wahitimu kwenye fani mbalimbali. Siyo uhandisi mitambo, ujenzi, kemikali, jiolojia, umeme na eletroniki na nyingine nyingi; pia kwenye uhasibu, utawala, biashara, sayansi ya siasa, sosholojia; kuna usanifu wa kila aina, nafasi hii hapa haitoshi kueleza viwango vya elimu vya watu wetu na aina za maarifa yanachotwa kwenye vyuo hivi.

Pamoja na haya yote, bado hatuwezi! Hatuwezi siyo tu kujitegemea kwa kuwapa watu wetu uwezo wa kuendesha mambo yatu, bali tunalalamika usiku na mchana kutafuta watu wa kuja kutufundisha hata jinsi ya kufanya usafi, jinsi ya kuendesha daladala, jinsi ya kufunga hesabu za biashara, kila kitu.

Tunapeleka watoto wetu shule, vyuo na elimu nyingine za juu ili wakakue, ili wakapoteze muda. Tuwazunga tunawajengea uwezo, lakini kiuhalisia tumeshindwa. Tena tumeshindwa vibaya.

Ukitafakari kwa kina unatagundua kuwa ni hakika mifumo yetu imeshindwa kutatua changamoto za maisha ya watu wetu. Tumeshindwa kuwahakikishia watoto wa taifa hili kwamba wanaweza kumudu changamoto za maisha kwa kutatua kero zetu hata zile za chini kabisa.

Wakati hali ikiwa hivi, tunashuhudia mwaka baada ya mwaka maisha ya ukwasi uliopitiliza ya watu walioaminiwa na umma na kukabidhiwa madaraka ya dola. Wanaishi maisha ya kufuru kwa kodi za umma. Maisha ya viongozi waliochanguliwa hayafanani kwa vyovyote na hali ya maisha ya Watanzania kwa ujumla. Ni kama maisha ya makundi mawili tofauti katika nchi mbili tofauti.

Mfumo huu wa maisha unatoa fursa kwa waliokalia ofisi za umma kuona kwamba wao ni wateule, wenye haki na ruhusa ya kufanya lolote kwa maslahi yao, lakini siyo kutatua kero za taifa hili.

Yaani miaka 61 ya uhuru hatuna Watanzania wanaoweza kuendesha biashara ya ‘daladala’ ya DART? Yaani umri huo ambao ni wa mtu aliyekwisha kufanya kazi mpaka akastaafu kwa mujibu wa sheria, bado tunajenga barabara nzuri kama za DART, lakini hatuwezi kabisa kuendesha mabasi ya kusafirisha abiria ambao wala siyo wa kutafuta. Wamejaa wa kumwagika! Hatuwezi.

Kwa sasa hivi Dar es Salaam inachimbuliwa usiku na mchana kujenga barabara. Sitaki kuingia kwenye mjadala wa vyanzo vya mapato vya ujenzi wa barabara hizo, ila ukweli ni mmoja barabara nyingi za mwendo kasi zinajengwa. Sasa hivi mkandarasi yuko kazini barababara ya mwendokasi Mwenge-Ubungo barabara ya Sam Nujoma; mkandarasi yuko kazini barabara ya Bagamoyo Mwenge- Tegeta; mkandarasi yuko kazini Chang’ombe- Magomeni; Barabara ya Nyerere kutoka Gongolamboto kuja mpaka mjini kati nayo iko kwenye ujenzi; kazi za ujenzi zinazofayika ni nyingi mno. Lakini, ajabu ni kwamba hata zile barabara ambazo tayari zimekamilika, kama kuanzia Kariakoo – (Barabara ya Kilwa) Rangi Tatu kwenda mpaka Mbagala ambayo kimsingi imekwisha kukamilika na hata ya Kimara mpaka Kibaha katika barabara ya Morogoro, hazitumiki.

Sababu kubwa ukiuliza unaambiwa anasubiriwa mwekezaji mpya. Yaani tunakiri kwamba tunaweza kununua magari ya kifahari kwenye ofisi za serikali, ambayo mengine yanakaribia milioni 500 kwa ajili ya waziri mmoja, lakini hatuwezi kununua mabasi na kutayasimiamia kwa ufanisi.

Yaani sisi tumekuwa watu wepesi mpaka tunashangaza. Hatujui vipaumbele vyetu, hatuwezi hata kuona hali ya watu wetu inavyozidi kudidimia siku baada ya siku, hatutaki kabisa kukosa usingizi tukitafuta majawabu ya matatizo ya watu wetu. Hatutaki kujenga uwezo wetu wa kujitegemea. Tunatafuta njia ya mkato, leta mwekezaji wa kuendesha ‘daladala za DART’ baada ya hapo, vijana wa Kitanzania wapambane na hali yao kuendesha bodaboda. Tunahitaji mtu wa kuelewa kwamba tumetumbukia kwenye aibu kubwa, na kwa dhamira ya kweli kabisa apanie kuliondoa taifa hili katika ulevi wa uvivu wa kufikiri.

spot_img

Latest articles

Soma Ripoti ya UHIFADHI WA UHAI: UKIUKWAJI WA HAKI ZA BINADAMU NDANI YA SEKTA YA UHIFADHI TANZANIA

Na Mwandishi Wetu, Media Brains Utafiti mpya umebaini kwamba mamlaka za serikali zimekuwa kichocheo kikuu...

RAIS DKT. SAMIA ATOA MAAGIZO KWA BASHE, NFRA KUNUNUA MAHINDI KWA WAKULIMA TSH 700 KWA KILO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassanamemuagiza Waziri wa Kilimo...

Upi upepo unaoweza kufika Tanzania,wa Wiliam Ruto au Paul Kagame?

KUNA upepo wa aina mbili unavuma katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mmoja...

Watu wawili wafariki, 16 wajeruhiwa katika ajali ya basi Songwe

Na Mwandishi Wetu, Media Brains Watu wawili wamefariki dunia na wengine 16 kujeruhiwa baada ya...

More like this

Soma Ripoti ya UHIFADHI WA UHAI: UKIUKWAJI WA HAKI ZA BINADAMU NDANI YA SEKTA YA UHIFADHI TANZANIA

Na Mwandishi Wetu, Media Brains Utafiti mpya umebaini kwamba mamlaka za serikali zimekuwa kichocheo kikuu...

RAIS DKT. SAMIA ATOA MAAGIZO KWA BASHE, NFRA KUNUNUA MAHINDI KWA WAKULIMA TSH 700 KWA KILO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassanamemuagiza Waziri wa Kilimo...

Upi upepo unaoweza kufika Tanzania,wa Wiliam Ruto au Paul Kagame?

KUNA upepo wa aina mbili unavuma katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mmoja...