Tanesco imebweteka, itoke kwenye boksi la raha

TAIFA bado lingali katika mgawo wa umeme kwa takribani miezi miwili sasa ambao Shirika la Umeme (Tanesco) limekataa kuuita kuwa ni mgawo. Badala yake wanadai ni ratiba ya kupatikana kwa umeme. Mgawo huu au upatikanaji wa umeme wa safari hii una nafuu kidogo kuliko ambao umepata kuwapo miaka ya nyuma.

Kuna maeneo yanapata umeme karibia muda wote wa siku kwa wiki (24/7), wapo wanaguswa na mgawo huo walau kwa saa 12 kwa wiki, lakini pia wapo wa saa 18 kwa wiki. Mgawo huu ni kwa uzoefu wa jiji la Dar es Salaam.

Wakati tukiendelea kugawiana umeme, sababu zikitajwa ni pamoja na ukarabati wa mifumo, lakini pia kukiwa na taarifa kwamba hali ya ujazo wa maji katika mabwawa ya kuzalisha umeme siyo nzuri, imeelezwa kwamba karibu asilimia 64 ya umeme wote unaozalishwa kwa sasa unatokana na nishati ya gesi asilia. Mitambo ya kuzalisha umeme kutokana na gesi asilia imejengwa jijini Dar es Salaam. Ipo iliyoko Ubungo ya Wartsila na ipo iliyoko Kinyerezi. Kwa maneno mengine kama gesi asilia isingelikuwa ipo au kama ingelikuwa haijafika Dar es Salaam na kuwa chanzo cha kuzalisha nishati ya umeme, hali ya taifa letu ingelikuwa mbaya zaidi kwa sasa.

Itakumbukwa kwamba ilikwisha kuwapo kwa mitambo ya mafuta mazito ya kuzalisha umeme. Makampuni binafsi kadhaa yaliingia mkataba na Tanesco kati ya mwaka 1994 hadi miaka ya 2015 katika kuzalisha nishati hiyo kwa mikataba ya mfumo uliojulikana kama Power Purchase Agreement (PPA).

Kumekuwa na ripoti nyingi, ikiwamo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) jinsi mikataba hii imeumiza Tanesco kiasi cha kujikuta ikibeba mizigo mikubwa na mizito ya madeni kutokana na umeme iliyokuwa ikinunua kutoka kwa kampuni hizi kuwa wa ghali mno. Hata sasa, Tanesco bado inadaiwa mabilioni ya shilingi na kampuni hizi, nyingine zikiwa zimefungasha virago nchini.

Baadhi ya mitambo inayotumika kupokea gesi asilia iliyoko Kinyerezi jijini Dar es Salaam.

Wakati tunatafakari mgawo wa umeme, hasa kutokana na changamoto ya umeme unaozalishwa kutokana na nguvu ya maji (hydroelectricity), ambao umezidi kupungua mwaka baada ya mwaka kutokana na kuzidi kuadimika kwa maji, tulipaswa kutafakari zaidi njia mbadala za kuzalisha nishati hii kwa kutumia vyanzo ambavyo ni rafiki na ambavyo haviishi (renewable sources).

Kwa mfano, yapo maeneo mengi ya nchi yetu ambako kuna upepo mkali sana ambao ungeliweza kabisa kujengwa mitambo ya kuzalisha umeme (windmills), maeneo haya yamekuwa yanatajwa mara kwa mara na vyombo vya serikali kwamba itasimikwa mitambo ya kuzalisha umeme, lakini matendo halisi ya kazi hiyo hayaonekani kuwa dhahiri. Maeneo haya ni pamoja na Singida, Makambako, Same na mengine mengi.

Tukiachana na upepo, Tanzania iko kwenye ukanda wa Kitropiki. Inapata jua karibia mwaka mzima. Jua ni chanzo kikubwa sana cha kuzalisha umeme. Chanzo hiki ukiaacha gharama za usimikaji wa miundombinu ya kufua umeme wake, ni cha uhakika na rahisi.

Ni jua la Mungu. Halina cha kupanda kwa bei katika soko la dunia kama tunavyoambiwa kwenye mafuta, halina cha wazalishaji kupunguza uzalishaji kama ilivyo kwa Jumuiya ya Mataifa yanayozalisha petroli kwa wingi duniani (OPEC), jua ni baraka ya Maulana, Muumba wa vyote. Kwa bahati mbaya kama taifa umeme wa jua haujatiliwa mkazo vya kutosha.

Kwa mfano, katika juhudi zile zile tunazowahimiza watu wetu kuhakikisha kwamba wanapojenga majengo mbalimbali, iwe makazi yao, shule, hospitali na majengo mengine yoyote binafsi au ya umma waweke miundombinu ya kuvuna maji ya mvua, vivyo hivyo tungehamasisha uwekaji/ufungaji wa miundombinu ya kupata umeme utokanao na jua. Kwa kufanya hivyo, Tanesco ingeliweza kupunguziwa mzigo mkubwa sana wa kusambaza umeme katika makazi.

Hata hivyo, Tanesco ingeliweza kabisa kuwa mbia katika mpango huo. Tunaambiwa kuwa vitaa vya umeme wa jua aghalabu ni vya bei ya juu, katika hali hii serikali ingeweza kutafuta namna ya nafuu ya bei – kuondoa kodi- ili kusaidia matumizi ya umeme wa jua kwa watu wengi zaidi hivyo kusaidia katika kulinda na kutunza mazingira kwa kuwa nishati hii ni rafiki wa mazingira.

Miaka kama sita hivi iliyopita ilipata fursa ya kutembelea Morocco. Kijiografia nchi hii imo katika jangwa la Sahara, sehemu kubwa pia ya ardhi yake imemezwa na jangwa hilo. Kwa kutambua kiwango cha juu kabisa cha jua wanachopata karibu mwaka mzima, taifa hilo la kaskazini mwa Afrika, limeingia katika mkakati wa kuwekeza kwa kiwango kikubwa kwenye matumizi ya umeme wa jua.

Mathalan, katika mji wa Marrakesh kuna chuo kikuu cha tekinolojia cha Mfalme Mohammed wa VI ambako kimejikita katika kukumbatia na kuendeleza tekinolojia ya kidijitali wakilenga kunuifaika na mapinduzi ya nne ya viwanda. Nishati kubwa inayoendesha mitambo chuoni hapo inatokana na ‘shamba la paneli za joto jua’ ambazo huzalisha umeme mwingi wa kukiwezesha kuendesha mitambo mbalimbali chuoni hapo. Ni chuo kinachokumbatia vijana wengi wanaojikita katika ubunifu wakiwa wamejaa utundu wa kujaribu vitu vipya katika ugunduzi.

Miongoni mwa matatizo makubwa ya taifa la Tanzania kwa sasa ni ukosefu wa ajira. Vijana wengi kwa mamilioni mwaka baada ya mwaka wanamwagwa mitaani kutoka shuleni na vyuoni. Wengi wamejikuta wakihangaika kusaka ajira ambazo zinazidi kuadimika mwaka baada ya mwaka. Ni hakika ujenzi wa mifumo ya umeme jua, siyo tu utatatua uhaba wa umeme nchini na kushusha gharama ya nishati hiyo nchini, bali pia utatoa fursa pana na kubwa ya ajira kwa vijana wa taifa hili.

Katika hali kama hiyo, mtu anaweza kujihoji, kama kwa takribani miaka 50 Tanesco haijaweza kutafuna mfupa wa mgawo wa umeme, ni kwa nini haioni kuna sababu ya kupanua wigo wake wa kusaka vyanzo vya nishati ya umeme kama umeme wa jua na upepo?

Ni wakati sasa umefika Tanesco na hususan wizara ya Nishati kutambua kwamba nchi yetu kukaa katika ukanda wa Kitropiki ikipata jua la utosini mwaka mzima, siyo jambo la bahati mbaya. Ni fursa ambayo inapaswa kutumika vema. Siku hizi ukipita katika maduka ya kuuza vifaa vya kieletroniki na umeme kama majokofu, redio, televisheni, glopu na vingine vipo ambavyo vinaendeshwa kwa umeme wa jua. Hizi ni fursa.

Hii ni neema ya Muumba, lakini ni bahati mbaya sana kama taifa tumeendelea kung’ang’ana na taratibu na mbinu zile zile za miaka zaidi ya 50 iliyopita kukabiliana na changamoto ya kupatikana kwa umeme wa uhakika nchini.

Suala la mgawo wa umeme limekuwa ni sehemu ya utamaduni wetu sasa. Hivi karibuni kwenye mitandao ya kijamii kulikuwa na tangazo linalodaiwa kuwa ni la Tanesco la mwaka 1975 likiwataarifu wateja wake katika Jiji la Dar es Salaam kuwa kutakuwa na mgawo wa umeme katika eneo la kitovu cha jiji hilo ikiwamo Ikulu.

Soma pia; https://themediabrains.com/2023/10/08/rwanda-mbaya-ya-1995-leo-inatuduwaza/

Kwa maelezo mengine, tangu mwaka 1975 Tanesco wamekuwa na utaratibu wa mgawo wa umeme. Katika hali kama hiyo, mtu anaweza kujihoji, kama kwa takribani miaka 50 Tanesco haijaweza kutafuna mfupa wa mgawo wa umeme, ni kwa nini haioni kuna sababu ya kupanua wigo wake wa kusaka vyanzo vya nishati ya umeme kama umeme wa jua na upepo? Ni wakati sasa wa kuitaka Tanesco itoke kwenye boksi lake la starehe ikalete umeme mbadala.

spot_img

Latest articles

Hivi vikosi kazi vimerejea kwa mlango wa nyuma?

KUNA kila dalili kwamba taifa letu kidogokidogo linakumbwa na hali ya kutokuaminiana. Hali hii...

Chondechonde Polisi msisababishe wananchi wakate tamaa

ALHAMISI iliyopita yaani Desemba 5, mwaka huu wa 2024 lilitokea tukio baya la kuhuzunisha...

Ufaransa yaipatia Tanzania Sh bilioni 323.4

Na Mwandishi Wetu Serikali ya Tanzania na Shirika la Maendeleo La Ufaransa (AFD) wamesaini mikataba...

TANZANIA YAWEKA REKODI MKUTANO WA WAHASIBU WAKUU AFRIKA

Na Mwandishi Wetu Tanzania imeweka rekodi ya Mkutano wa Pili wa Wahasibu Wakuu wa Serikali...

More like this

Hivi vikosi kazi vimerejea kwa mlango wa nyuma?

KUNA kila dalili kwamba taifa letu kidogokidogo linakumbwa na hali ya kutokuaminiana. Hali hii...

Chondechonde Polisi msisababishe wananchi wakate tamaa

ALHAMISI iliyopita yaani Desemba 5, mwaka huu wa 2024 lilitokea tukio baya la kuhuzunisha...

Ufaransa yaipatia Tanzania Sh bilioni 323.4

Na Mwandishi Wetu Serikali ya Tanzania na Shirika la Maendeleo La Ufaransa (AFD) wamesaini mikataba...