Hasira za wabunge zinakumbusha kauli ya CAG Profesa Mussa Assad

NJAMA ni maafikiano au mapatano ya kufanya jambo baya dhidi ya mtu au watu wengine. Aghalabu neno hili huendana na jingine ‘kula njama’ na mara nyingi hufungamanishwa na mipango ya kutenda uhalifu pia.

Ni vigumu hata hivyo kundi kubwa la watu wengi kula njama. Ni vigumu kwa sababu kula njama inapaswa kufanyika kwa usiri mkubwa, ili mlengwa asigundue. Au watu wengine wasigundue na kusababisha njama hiyo kutokutelekezwa.

Njama, aghalabu hulenga kuwanuifaisha wapangaji wake. Kama ni kwenda kutekeleza uhalifu ili kunufaika ama na mali gharama au na hali itakayowasababisha faida yoyote kinyume cha sheria na hata maadili. Njama siyo kitu kizuri.

Nililikumbuka neno hili wiki iliyopita nilipokuwa nafuatilia mjadala bungeni wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali za mwaka 2021/2022. Kwa yeyote aliyesikiliza mjadala huo bungeni, hakika aliona nyuso nyingi za wabunge wenye uchungu. Wabunge waliokuwa wamekasirishwa na kile kilichomo kwenye ripoti ya CAG. Kwa kifupi wabunge walisema “wizi, rushwa na ufisadi” ndivyo vimejaa kwenye ripoti hiyo.

Wapo waliokwenda mbali zaidi na kusema kwa kuwa sasa imekuwa ni kawaida, mwaka baada ya mwaka matrilioni ya shilingi yanaibwa, katika miradi ya maendeleo na hakuna uwajibikaji, sasa ni wakati wa kuanzisha sheria ya kunyonga wezi wa mali ya umma.

Kama ni mgeni Tanzania unaweza kuingia kwenye mtego wa kuwasifu wabunge kwa kile walichokuwa wanakisema. Kukasirishwa na wizi wa mali ya umma. Kwamba wanakiri mwaka baada ya mwaka ripoti ya CAG inaibua ubadhirifu mkubwa kwenye matumizi ya fedha za umma. Miradi kujengwa chini ya kiwango, fedha kuibwa na kila aina ya matendo yanayoashiria kwamba hakuna anayejali kukomesha hali hiyo.

Katika kusikiliza wabunge hao nikakumbuka ghadhabu za Spika aliyejiuzulu, Job Ndugai, dhidi ya CAG aliyeondoshwa madarakani kihuni, Profesa Mussa Assad kutokana na kauli yake “bunge ni dhaifu.” Profesa Assad alitoa kauli hiyo akihojiwa na chombo kimoja cha habari huko nje, akionyesha kwamba CAG kazi yake ni kukagua hesabu, kufanya uchambuzi na kuwasilisha kwa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, ambaye huiwasilishwa ripoti hiyo bungeni kwa hatua za udhibiti na uwajibikaji.

Kwa maana kwamba Bunge ndilo linapitisha bajeti ya serikali, ndilo linapitisha sheria ya kutoza kodi na ndilo lenye mamlaka ya kuisimamia serikali katika kutekeleza hayo ambayo wamepewa. Yaani kupanga bajeti, kukusanya kodi, kutumia fedha za kodi kwa kuzingatia ruhusa iliyotolewa kisheria na Bunge.

Ibara ya 63 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatamka bayana kazi za Bunge kuwa ni pamoja na: “Sehemu ya pili ya Bunge itakuwa ndicho chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano ambacho kitakuwa na MADARAKA, kwa niaba ya wananchi, KUISIMAMIA na kuishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa Katiba hii.”

Kama hizo ndiyo miongoni mwa kazi za Bunge, je, kosa la Assad lilikuwa ni nini kama kile alichokisema ndicho hata sasa bado kinaendelea, kwamba inawasilishwa ripoti ya CAG ikonyesha ukiukaji mkubwa wa matumizi ya fedha umma, lakini mwaka baada ya mwaka hali hiyo inajirudia na kujirudia. Ukisikiliza wabunge, bila hata kutaja majina yao, wameonyesha kabisa kukata tamaa juu ya hali hii.

Mwenendo usiobadilika wa matumizi mabaya ya fedha za umma, lakini watuhumiwa ama wapo ofisi zile zile au wamehamishwa kwenda kwingine. Wametajwa baadhi ya wakurugenzi wa halmashauri ambao kazi yao ni upigaji, na wapo na wanaendelea kupiga mwaka baada ya mwaka.

Ni dhahiri, kwamba uendelea kwa hali ya kushindwa kokomesha hali hii ya matumizi mabaya ya fedha za umma kwa mabilioni, kunaacha sura mbaya kwa Bunge kwamba ama halitaki kuiwajibisha serikali au linalinda serikali na udhaifu unaoibuliwa kila wakati katika mawanda ya ripoti ya CAG. Hali hiyo pia inaibua hoja nyingine muhimu, je, Bunge nalo kwa kushindwa kufanya hivyo licha kukaa vikao na vikao, vya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAC) na Kamati Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC)?

Kwamba baada ya kazi za kupitia ripoti ya CAG kwa PAC, LAC na POAC na kuwasilishwa kwa taarifa kwenye Bunge zima, mjadala mkali kama huo kufanyika, vyote hivi ni gharama ya muda na fedha. Ni matumizi pia ya fedha za walipa kodi. Swali la kujiuliza ni hili, ni mpaka lini hali hii itaendelea bila kuwapo kwa uwajibikaji ambao kwa kweli utasababisha watumishi wa umma kuziogopa fedha za wananchi?

Kuna wakati pale bungeni inajitokeza hali kama vile serikali ndani ya Bunge, kwa maana mawaziri wana hadhi kubwa zaidi kuliko wabunge wa kawaida, na kwa maana hiyo ni kama vile serikali imewameza/wafunika wabunge wambao siyo mawaziri.

Na ni kwa sababu hiyo utaona baadhi ya wabunge tena wengi kazi yao ni kujipanga kama vile ni mawaziri watarajiwa. Hali hii ya kutamani kuwa serikalini pengine inasababisha wabunge, ambao kimsingi ni wengi kuliko mawaziri, kushindwa kujipanga kwa hoja, kuwasilisha hoja za maandishi na maazimo ili kuisukuma serikali. Lakini kilichopo ni kama vile serikali inavuta miguu katika kutekeleza kile wabunge wanazungumza.

Ni katika sura hiyo mtu anashindwa kuhitimisha hali hii ya kuendelea kwa ubadhirifu ule ule miaka na miaka kwamba inaweza tu kukoma kama kutakuwa na Bunge jeuri, lenye meno, lenye wabunge jasiri ambao wanaweza kuiwajibisha serikali. Bila kuwa na Bunge linaloogopwa na mawaziri na siyo kinyume chake ni kwa nini tusikumbuke maneno ya Profesa Mussa Assad, juu ya hadhi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania? Au ni kwa nini tusitafakari maneno ‘kula njama’.

spot_img

Latest articles

Soma Ripoti ya UHIFADHI WA UHAI: UKIUKWAJI WA HAKI ZA BINADAMU NDANI YA SEKTA YA UHIFADHI TANZANIA

Na Mwandishi Wetu, Media Brains Utafiti mpya umebaini kwamba mamlaka za serikali zimekuwa kichocheo kikuu...

RAIS DKT. SAMIA ATOA MAAGIZO KWA BASHE, NFRA KUNUNUA MAHINDI KWA WAKULIMA TSH 700 KWA KILO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassanamemuagiza Waziri wa Kilimo...

Upi upepo unaoweza kufika Tanzania,wa Wiliam Ruto au Paul Kagame?

KUNA upepo wa aina mbili unavuma katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mmoja...

Watu wawili wafariki, 16 wajeruhiwa katika ajali ya basi Songwe

Na Mwandishi Wetu, Media Brains Watu wawili wamefariki dunia na wengine 16 kujeruhiwa baada ya...

More like this

Soma Ripoti ya UHIFADHI WA UHAI: UKIUKWAJI WA HAKI ZA BINADAMU NDANI YA SEKTA YA UHIFADHI TANZANIA

Na Mwandishi Wetu, Media Brains Utafiti mpya umebaini kwamba mamlaka za serikali zimekuwa kichocheo kikuu...

RAIS DKT. SAMIA ATOA MAAGIZO KWA BASHE, NFRA KUNUNUA MAHINDI KWA WAKULIMA TSH 700 KWA KILO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassanamemuagiza Waziri wa Kilimo...

Upi upepo unaoweza kufika Tanzania,wa Wiliam Ruto au Paul Kagame?

KUNA upepo wa aina mbili unavuma katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mmoja...