Na Winfrida Mtoi, Media Brains
BODI ya Mikopo ya Elimu ya Juu nchini (HESLB) inadai Sh.758 bilioni zinazopaswa kurejeshwa kutoka kwa wanufaika wa mikopo hiyo kati ya mwaka 2005 na Septemba 2023.
Kiasi hicho cha fedha ambacho bado kiko mikononi mwa wanufaika wa mikopo tangu mwaka 2005, ni kikubwa (kwa Sh. 104 bilioni) zaidi ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya mikopo yote ya wananfuzi katika mwaka wa fedha 2022/23 ambazo zilikuwa Sh. 654 bilioni.
Kadhalika kiasi hicho ni chini kidogo (kwa Sh.28 bilioni) ya fedha ambazo zimetengwa kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi 220,376 watakaofadhiliwa katika mwaka huu wa fedha wa 2023/24, ambazo zinafikia Sh. 786 bilioni.
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru amesema jijini Dar es Salaam katika mkutano wa Wahariri wa vyombo vya habari kuwa kati ya 2005 na Septemba 2023 bodi hiyo imeishakukusanya Sh.1.34 trilioni sawa na asilimia 64 ya Sh. 2.1 trilioni zinazopaswa kurejeshwa kutoka kwa wanafuaika 235,498.
Badru anasema HESLB inaendelea kuchukua hatua kwa wale ambao wameshindwa kurejesha mikopo kupitia kampeini walioianzisha na kupewa jina la ‘fichua’ inayowashikisha wananchi kutoa taarifa kwa hiari yao kuhusu wanaokwepa kulipa mikopo waliyotumia kwa ajili ya kusoma elimu ya vyuo vikuu.
“Tunaendelea kuboresha huduma za urejeshaji mikopo kidigitali ili kurahisisha wanufaika kulipa popote na kiasi chochote kwa urahisi,” amesema.
Badru amesema kutokana na maboresho ya mifumo ukusanyaji, marejesho yamekuwa yakiongozeka kwani katika kipindi cha miaka mitatu wamefanikiwa kukusanya sh. 530 bilioni sawa na asilimia 93 ya lengo la kukuanya sh.565 bilioni.
Amefafanua kuwa kwa miaka mitatu 2020/2021 hadi 2022/2023 HESLB imekusanya Sh. 530 bilioni saw ana asilimia 93 ya malengo waliokuwa wamejiwekea ya kukusanya kiasi cha Sh. 565 bilioni. “Mwaka 2020/21tulivuka lengo kwa kukusanya bilioni 181tukazidi malengo tuiokuwa tumejiwekea kwa asilimia 101 na mwaka 2021/22 makusanyo ni bilioni 180.7 sawa na asilimia 95 ya lengo.
Anaeleza kuwa makusanyo hayo yametokana na wanufaika kulipa kwa mkupuo baada ya kuondolewa kwa tozo ya adhabu na malengo yao mwaka 2023/24 ni kukusanya bilioni 230.
Aidha anataja changamoto ambazo zilikuwa kikwazo cha ukusanyaji madeni kuwa ni athari za ugonjwa wa UVIKO 19 na wanufaika waliopo sekta binafsi na zisizo rasmi kukosa utayari wa kujitokeza kulipa madeni yao.
Kuhusu ongezeko la idadi ya wanufaika katika miaka iliyopita minne, Badru anasema 2020/21 walikuwa 149,506, wakati 2021/22 ni 177,892, mwaka 2022/23 ni 198,105, huku 2023/2024 wakifikia 220,376.
Kuhusu bajeti amesema imeongezeka kwa asilimia 63, kutoka bilioni 464 mwaka 2020/21 hadi kufikia bilioni 786 mwaka 2023/24 na kwamba pamoja na serikali kutega kiasi kikubwa cha fedha,
bado Serikali inahitaji kuongeza mtaji ili kuiwezesha taasisi kufanya kazi kubwa zaidi.
Kwa mujibu wa Badru wanafunzi waliopewa mikopo mwaka huu wanajumuisha wale wa mwaka wa kwanza 75,000 na wanafunzi 145,376 wanaoendelea.
Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati ya Utenaji wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena, amesema ipo haja kwa Serikali kupitia HESLB kutoa mikopo kwa wanaosomea fani ya uandishi wa habari kama ilivyo kwa kada na fani nyingine.