Tuihami demokrasia kwa udi na uvumba

Katika miaka ya hivi karibuni dunia imeshuhudia wimbi jipya la viongozi watamanio mkono wa chuma. Hili ni lile linalopingana hata na mifumo asili ya demokrasia. Kwa mfano wapo wasioamini tena katika chaguzi kiasi cha kuhamasisha umma kuingia mitaani kupinga kile kinachoitwa matokeo ya chaguzi huru na haki.

Kwa mfano, Rais Donald Trump wa Marekani mwaka 2020 alifanya vituko ambavyo havijawahi kufanywa na kiongozi mwingine wa ngazi yake katika taifa hilo linaloaminiwa kuwa kitovu cha demokrasia.

Trump alihamasisha ‘wahuni’ kuvamia Bunge la nchi hiyo kwa kile alichodai kukataa matokeo ya uchaguzi ambayo mpinzani wake(Rais wa sasa), Joe Biden alitangazwa mshindi. Trump alidai kuwa katika uchaguzi huo kulikuwa na hila na aliibiwa kura. Madai yake yote alishindwa kuyathibitisha mahakamani. Aibu kubwa!

Wakati dunia ikihangaika na majanga kama vita vya Urusi na Ukraine na hapa juzi baina ya Israel na Hamas, kile kilichoanza kujichomoza fungu la miaka ya 2015-2020, kwamba sasa mataifa yanatamani viongozi wa mkono wa chuma na siyo taasisi za utawala bora na demokrasia, ndicho kinaonekana kuendelea kusumbua mataifa mengi kwa sasa.

Ni kiu hii ya kutaka mtu na siyo taasisi ndicho kilishangaza ulimwengu mwaka 2016 Trump alipomshinda Hilary Clinton, hata baada ya mchakato wa ndani ya Chama cha Republican wa kumtafuta mgombea kuonyesha wazi kuwa Trump hakuwa mtu wa kusikiliza au kuheshimu taasisi za utawala, badala yake yeye ndiye angelikuwa taasisi.

Ni katika hali hiyo, Marekani kati ya 2016-2020 walipita katika tanuru la moto kutokana na mfumo wa utawa wa Trump. Haishangazi kwamba hata baada ya aibu iliyopata Marekani kwa Trump kuhamasisha uvamizi wa Bunge na ubabe wake wa kupuuza taasisi za utawala, bado Wamarekani wanatamani awe rais wao mwakani katika uchaguzi mkuu.

Rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump. Picha|REUTERS/Sam Wolfe

Trump hayuko peke yake, katika mfumo huo wa matamanio ya kiongozi madhubuti – mkono wa chuma, Uingereza nayo mwaka 2019 ilijikuta ikimpata, Boris Johnson kama Waziri Mkuu hadi 2022, alipolazimishwa kubwaga manyanga.

Utaratibu huo ndiyo umeendelea kumweka madarakani Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki, ambaye anaamini katika mfumo wa mkono wa chuma na siyo wa kitaasisi. Matamanio haya ya watu dhidi ya taasisi na mifumo, yamezidi kuota mizizi katika mataifa mengi kwa sasa kiasi kwamba sasa nguvu kubwa ya rasilimali fedha na muda wa kazi vinaelekezwa kijenga watu badala ya taasisi.

Tanzania kati ya mwaka 2015 – 2020 nasi tulijikuta katika mkwamo wa kutamani kujenga mtu badala ya taasisi na mifumo. Sote tunakumbuka vema jinsi nchi na vyote vilivyomo viligeuzwa kuwa kama mali ya mtu mmoja.

Tanzania kati ya mwaka 2015 – 2020 nasi tulijikuta katika mkwamo wa kutamani kujenga mtu badala ya taasisi na mifumo. Sote tunakumbuka vema jinsi nchi na vyote vilivyomo viligeuzwa kuwa kama mali ya mtu mmoja. Ni wakati kila kitu kilianza kutajwa kwa jina la rais aliyeko madarakani. Katika kampeni za uchaguzi ungetafakari baadhi ya mabango, ungepata picha inayoonyesha kuwa John Magufuli alikuwa kama mgombea binafsi kwa maana ya aina ya mabango yake.

Watu wa timu yake ya kampeni waliendesha harakati zao kama vile wako nje ya chama, kumjenga mtu na siyo chama. Taasisi – CCM ilionekana kuwa mzigo, lakini urahisi ukaonekana kumbeba mgombea kwa jina – Magufuli.

Hayati John Magufuli.

Na katika kuendeleza wimbi hilo la kutamani mtu dhidi ya taasisi, fedha za umma za walipa kodi ghafla zikageuka na kuanza kuwa za Rais John Magufuli, serikali ikageuka na kuwa serikali ya Rais Magufuli, kila kitu, sasa kikawa ni cha Rais.

Ugonjwa huo wa kutukuza mtu kuna wakati hata Rais Mstaafu Benjamin Mkapa ulimkera na kutaka serikali itambuliwe kuwa ni ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Akilenga kusahihisha makosa ya wenzake ndani ya chama hicho ambao waliona kuwa kitu cha maana ni kujenga mtu na siyo taasisi.

Ni katika wimbi hilo la kutaka kujenga mtu (personality) badala ya taasisi hata sasa tungali tunaona watu wakisema kwa kijiamini sana kwamba fedha za maendeleo zinazotolewa na serikali ni za Rais. Fedha za Mama. Utamsikia Waziri akisimama bungeni na kumshukuru Rais kwa kutoa fedha. Wanasahau kuwa hizi ni fedha za serikali, zilizopatikana kwa kutoza kodi, fedha za umma, mali ya wananchi, ghafla zinakuwa za mtu mmoja.

Kwamba tunakuwa na viongozi wasahaulifu kiasi cha kusahau kwamba kila pesa ambayo serikali inapata inatokana na jasho la wananchi wake. Kwamba ni katika shughuli za kiuchumi za wananchi, kwenye kilimo, viwandani, kwenye biashara ndiko kodi na tozo mbalimbali zinapatikana na hivyo serikali kupata mapato ya kuendesha shughuli kwa ajili ya kuwahudumia wananchi husika. Hizi asilani haziwezi kuwa fedha za mtu.

Kwa nini juhudi hizi za kutamani sana kujenga mtu dhidi ya taasisi zimekuwa kwa kasi kubwa? Na ni kwa nini hata wale walioaminiwa na kupewa wajibu wa kuwasilisha bungeni muswada wa fedha kuhusu kodi bado wanaendeleza ‘ukasuku’ kuwa fedha za umma ni mali ya Rais? Hizi ni juhudi za watu kujijengea uhalali wa kuwa karibu na watawala, ni juhudi za kutaka kumpotosha kiongozi mkuu asahau nafasi yake na kujikuta akiitikia mapambio ambayo kimsingi yanamwaribia upeo wa kutekeleza wajibu wake.

Ninafahamu mawanda ya katiba ya Jamhuri ya Tanzania na madaraka ambayo amepewa Rais, lakini hakuna kokote ambako katiba hiyo inasema Rais atakuwa na fedha zake. Hakuna kokote ambako imesemwa Rais anaweza tu kuanzisha bajeti na kodi bila kupitia bungeni.

Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

Kwa maana hiyo, pamoja na uhalali na haki ya kuheshimiwa na kuenziwa kwa kiongozi mkuu wa dola, yaani Rais, kama vile kumtaja katika mafanikio ya utendaji wa serikali yake na mambo yanayofanana na hayo, utaratibu huu mpya wa kutaka kujenga Rais Mfalme ambao unazidi kuota mizizi duniani, ni ishara tosha kwamba sasa kiu ya watu wengi ni kutaka Rais mwenye mkono wa chuma anayetenda yeye kuliko ujenzi wa taasisi za kiutawala za kidemokrasia ambazo zitampa kila mmoja haki na wajibu sawa mbele ya sheria.

Tujikumbushe tu, dunia hii ilipata kuangamizwa katika vita kuu vya dunia mara mbili, kikubwa ni tabia ya kutamani viongozi wa mkono wa chuma dhidi ya ujenzi wa taasisi za kidemokrasia zenye ushawishi na zinazoweza kumdhibiti yeyote kwa haki. Ni jambo la kuogofya kama Tanzania na mataifa mengine ulimwenguni leo tunajiwinda kutamani kuwa na viongozi wa mkono wa chuma badala ya kujibidiisha kujenga taasisi imara za kiutawala na kidemokrasia ambazo zitahaikisha haki na usawa kwa watu wote. Ni wakati wa kuhami demokrasia yetu kwa udi na uvumba.

spot_img

Latest articles

YAPO MATAMANIO YA UCHAGUZI WA 2019 KUJIRUDIA 2024?

KUNA uhusiano wowote kati ya mafanikio ya kiuchumi kwa nchi yoyote na kukua kwa...

Dabi ya Kariakoo Wanawake, kitaumana kesho

Na Winfrida Mtoi Mechi ya Dabi ya Kariakoo ya Ligi ya Wanawake Tanzania Bara,...

Baraza la Mawaziri sasa Kidigital- Majaliwa

Na Mwandishi Wetu Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kuwa matumizi ya mfumo wa kielektroniki...

SOMO KUTOKA KWA WATSWANA, WAFUATA NYAYO ZA WAZAMBIA KUING’ARISHA SADC

KUNA habari njema tena kutoka ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)....

More like this

YAPO MATAMANIO YA UCHAGUZI WA 2019 KUJIRUDIA 2024?

KUNA uhusiano wowote kati ya mafanikio ya kiuchumi kwa nchi yoyote na kukua kwa...

Dabi ya Kariakoo Wanawake, kitaumana kesho

Na Winfrida Mtoi Mechi ya Dabi ya Kariakoo ya Ligi ya Wanawake Tanzania Bara,...

Baraza la Mawaziri sasa Kidigital- Majaliwa

Na Mwandishi Wetu Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kuwa matumizi ya mfumo wa kielektroniki...