Nikiri kwa dhati kabisa Rais wa Tanzania ana mamlaka yasiyohojiwa juu ya uteuzi wa wasaidizi wake katika nafasi mbalimbali za utumishi serikalini. Mamlaka haya chimbuko lake ni Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hasa ibara za 36 na 37. Hatahojiwa kwa kutekeleza matakwa ya ibara hizi.
Kwa maana hiyo, wote wanaoteuliwa na Rais kushika madaraka mbalimbali ya kiutumishi katika utumishi wa umma, wanapewa fursa hizo na Rais. Ni kama vile Rais anawamegea sehemu kidogo ya madaraka yake katika kutekeleza majukumu mabalimbali ya umma. Na ni Rais huyo huyo mwenye haki na wajibu wa kuwaacha waendelee kutekeleza majukumu aliyowapa, au akiamua kuwaondoa ni hiari yake. Halazimishwi kusema ni kwa nini amewaondoa kama vile ambavyo pia halazimishwi kusema ni kwa nini amemteua yeyote.
Hata hivyo, pamoja na madaraka hayo ya kikatiba ya Rais, ni kwa miujiza tu itawezekana Rais kuwafahamu watu wote anaowateua. Kwa mfano, Tanzania Bara ina mikoa 26, wilaya 139 na halmashauri 185. Wakuu wa maeneo hayo wote wanateuliwa na Rais. Wapo wakuu wa taasisi za serikali zinazojitegemea, wako wakuu wa mashirika ya umma, wako mawaziri na manaibu wao, wapo makatibu wakuu na manaibu wao, wapo mabalozi, wapo majaji wote. Kwa kifupi orodha hii ni ndefu sana, na haiyumkini mtu mmoja awafahamu wote hawa anaowateua hata kama Katiba inatamka hivyo. Huu ni ubinadamu, kiongozi mkuu wa nchi hata kama angelitaka kuwafahamu wote hawa kabla ya kuwateua, isingewezekana.
Sasa katika kutekeleza majukumu haya, Rais ana vyombo vya kumshauri, ingawa pia halazimiki kufuata ushauri wao, katika kufanya teuzi hizi. Katika mfumo unaofanya kazi sawasawa, majina ambayo yanafikishwa kwa Rais kwa ajili ya uteuzi, ni lazima yawe yamepepetwa sawasawa. Kwamba ni watu wa namna gani wanapendekezwa kuteuliwa katika nafasi hizo, na kwa kweli wawe ni watu wenye uwezo katika kumudu majukumu ambayo wanakwenda kukabidhiwa. Serikali ni taasisi kubwa, ina vyombo vingi vya kuweza kusaidia kufanyika kwa upepetaji wa watu hao.
Kwa hali hiyo, haitarajiwi kwa mfano, leo mchana fulani atangazwe kuteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa, halafu usiku taarifa itoke kwamba uteuzi huo umetenguliwa. Ni kweli ni haki ya mamlaka ya uteuzi kuteua na kutengua. Lakini, katika mazingira ya namna hiyo linaibuka swali kubwa, hivi kabla ya kuteuliwa upepetaji ulifanyika kwa kiasi gani, na vyombo husika vilijiridhisha vipi kabla ya hilo jina kufika mezani kwa mteuaji?
Tumeona katika siku za hivi karibuni kasi kubwa ya kuteua na kutengua, ingawa Watanzania hawapewi maelezo ya sababu za utenguaji, kwa kuwa mteuaji halazimiki kusema, kuna hali ya maswali magumu inaibuka miongoni mwa jamii, kwamba hivi siku hizi teuzi zinafanyika kirahisi rahisi tu bila kupepeta vya kutosha?
Zamani, katika elimu ya msingi somo la uraia ilikuwa ni pamoja na kujua majina ya viongozi wa nchi. Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Mawaziri, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na wengine wanaoangukia katika kundi hilo. Leo hii, ni vigumu kuwajua viongozi hao na nafasi zao, ukiacha tu watatu pale juu, Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu. Wengine kasi ya kuhamishwa na kutenguliwa ni kubwa. Yawezekana ni kwa mema.
Kwa mfano, Rais sasa yuko madarakani miaka miwili na miezi mitatu, lakini rekodi zinaonyesha alishafanya uteuzi mkubwa mara mbili wa wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa. Lakini kama hiyo haitoshi, hata hao waliopo wamekwisha kuhamishwa vya kutosha, kutoka hapa kupelekwa kule. Inawezekana ni katika kujenga. Pia inawezekana ni katika kuimarisha uwajibikaji na nidhamu, lakini ni vema pia ikakumbukwa kwamba kila anayepewa wajibu wa kutekeleza mahali popote pa kazi kuna muda wa kujipanga, kuelewa vema eneo lake, kufahamu mepesi na magumu, kuwajuwa watu, kujua yupi ni yupi na yupi si yupi, ili kujipanga kwa utekelezaji wa majukumu. Sasa kama kila wakati katika kipindi kifupi kuna panguapangua, mtiririko na kasi ya utendaji si unavurugika?
Najua wapo watakaosema kwamba serikali ni taasisi na kwa maana hiyo hata akiondoka nani mambo yataendelea tu kama kawaida. Wana haki ya kusema hayo, na kweli serikali ni taasisi kubwa. Lakini, sote tujiulize kama utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan ni sawa na ule wa mtangulizi wake? Kwa maneno mengine personality matters a lot.
Naomba ieleweke wazi kuwa sina nia hata chembe ya kuhoji maamuzi ya Rais katika kupanga safu yake, lakini nina sukumwa ndani kwangu kuuliza na kudadisi kama yale majina yanayofikishwa mbele yake kwa ajili ya uteuzi yanakuwa yamefanyiwa upepetaji wa kutosha ili hakika pumba, makapi, na mbegu zilizovunjikavunjika zisiwemo katika ungo mkubwa uliojaa mbegu bora ambazo ziko tayari kwenda kupandwa shambani? Vyombo vya kupepeta vinaweza kuwa chanzo kikubwa kinachosababisha hii hamisha hamisha na utenguaji huu kwa kuwa kilichopelekwa mbele ya mamlaka ya uteuzi hakikustahili kufika huko.
Kwangu mimi kama kuna sehemu serikali inapaswa kutupia jicho ni katika vyombo hivi vya kupepeta, viangaliwe, visukwe upya, vizingatie kile kinachoitwa kwa Kimombo appointment by meritocracy.