Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), imejizatiti kuendana na mabadiliko ya teknolojia duniani, ikiwemo matumizi ya Akili Mnemba (AI), ili kuendelea kuimarisha usalama na ufanisi wa usimamizi wa anga nchini.
Kauli hiyo imetolewa Januari 23,2026 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Salim Msangi, wakati akifungua Mkutano wa Mwaka wa 45 wa Chama cha Waongoza Ndege Tanzania (TATCA).

Akifungua mkutano huo, Msangi amesema “TCAA itaendelea kutenga bajeti ya kila mwaka kwa ajili ya mafunzo ya wataalam wa anga ili kuhakikisha wanaendana na mabadiliko ya teknolojia ikiwemo matumizi ya Akili Mnemba (AI)na kuendelea kudumisha viwango vya juu vya usalama”.
Msangi ameongeza kuwa mamlaka hiyo tayari imefanikiwa kufunga mifumo ya kisasa ya mawasiliano katika vituo vya TCAA vilivyopo katika viwanja 15 vya ndege nchini, na kuongeza kuwa hatua hiyo itakayoongeza ufanisi wa mawasiliano kati ya marubani na waongoza ndege.

Amesema anga la Tanzania limeendelea kuwa salama na la kuaminika, hali iliyochangia ongezeko la ndege zinazopita katika anga la nchi, kutokana na uwepo wa mifumo imara ya mawasiliano na uongozaji wa ndege.

Sambamba na ufunguzi huo, Msangi pia aliwapatia tuzo maalum waongozaji ndege wastaafu wawili ikiwa ni kutambua mchango wao mkubwa katika kuimarisha usalama wa usafiri wa anga na maendeleo ya taaluma ya uongozaji ndege nchini.

Kwa upande wake, rais wa (TATCA), Merkiory Ndaboya, amesema mkutano wa 45 wa mwaka wa chama hicho ni jukwaa muhimu kwa wataalam wa anga katika kujadili changamoto zinazoikabili sekta hiyo na kuweka mikakati ya pamoja ya kuimarisha ufanisi.

Ndaboya amepongeza hatua zinazochukuliwa na TCAA katika kuimarisha mifumo ya kisasa ya anga na kusema chama hicho kitaendelea kushirikiana na mamlaka hiyo kwa lengo la kuboresha usalama na huduma za anga nchini.
Mkutano wa 45 wa TATCA unafanyika chini ya kaulimbiu ya “Ajira na Mafunzo kwa Usimamizi Endelevu wa Anga”, ukikusanya wataalam wa anga kutoka ndani na nje ya nchi.


