Na Tatu Mohamed
SERIKALI inatarajia kuanzisha kituo Maalum cha kuhudumia na kuwezesha wawekezaji vijana(Youth Investors Resource Centre) nchini ikiwa ni mkakati wa kupunguza wimbi la ukosefu wa ajira na kuongeza fursa za uwekezaji kwa vijana.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo leo Disemba 8,2025 Jijini Dar es salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari lengo likiwa kutoa mwelekeo wa kisera na kiutendaji wa Serikali kupitia Wizara ya Mipango na Uwekezaji kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Amefafanua kuwa, katika kipindi cha miaka mitano ijayo, seriakali itaanzisha programu maalum ya kuwezesha wawekezaji vijana kubuni na kuanzisha uwekezaji wa viwanda nchini kote.
Amebainisha kwa kuanzia, watatenga maeneo ambayo vijana waliomaliza vyuo vikuu na vyuo vya ufundi watapewa ili kuweza kuwekeza kwenye viwanda.
“Programu hiyo itahusisha mafunzo, uwezeshaji wa kupewa ardhi, kuunganishwa na wauzaji wa mitambo na malighafi (machinery and raw materials), na pia kuunganisha na benki ambazo zina ushirikiano na TISEZA ikiwemo Benki ya Azania, TCB, na CRDB,” amesema.

Ameongeza pia watatenga maeneo maalum kwa uwekezaji utakaofanywa na vijana Dodoma Nala lenye Ekari 100), Pwani eneo la Kwala lenye Ekari 20, Mara kule Bunda lenye Ekari 100), Ruvuma Songea lenye Ekari 100 na Bagamoyo Pwani kuna Ekari 20,”amesema.
Amesema programu hiyo itaizinduliwa pamoja na Kituo Cha Kuwezesha Vijana kabla ya mwisho wa mwaka huu.
Prof Mkumbo ameongeza kuwa serikali inakusudia kusogeza huduma za Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi kufikia kila Mkoa ifikapo mwaka 2028.

“Kila Mkoa utakuwa na kituo maalum cha kutangaza na kuwezesha wawekezaji sambamba na agizo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan la kusogeza huduma kwa wananchi wote.
“Tutashirikiana na wenzetu wa TAMISEMI kuratibu na kuwezesha huduma hizi kuwafikia wote nchini,” amesema.
Amesema kwa kushirikiana na sekta binafsi, kutajengwa miundombinu ya uwekezaji wa viwanda nchi nzima.


