Na Mwandishi Wetu
MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, ametoa wito kwa wakulima wanaotumia maji ya Mto Ruvu kwa shughuli za kilimo kusitisha matumizi hayo kwa muda hadi pale mvua zitakapoanza kunyesha kwa wingi ili kutoathiri shughuli za uzalishaji na usambazaji wa maji kwa wananchi wa Dar Es Salaam na Pwani.
Kunenge ametoa wito huo wakati alipofanya ziara katika mitambo ya uzalishaji maji ya Ruvu Chini na Ruvu Juu kwa lengo la kukagua Hali ya uzalishaji maji na upatikanaji wa maji katika chanzo cha mto Ruvu.

“Mabadiliko ya hali ya hewa hususani kuongezeka kwa joto yamesababisha kupungua kwa kiwango cha maji, hususan katika eneo la Ruvu Chini, halii hii pia imesababishwa na shughuli za kilimo zisizo rasmi kando kando ya mto kwa watu kulima bila vibali” ameeleza Kunenge.
Kunenge ameongeza kuwa ,uzalishaji wa maji katika mtambo wa Ruvu Chini umepungua, japokuwa si kwa kiwango kikubwa, huku Ruvu Juu ikiendelea kuwa na kiwango cha maji cha kuridhisha.

“Nitoe wito kwa watumiaji wa maji, hususani wanaofanya Kilimo kusitisha matumizi hayo kwa muda mpaka pale mvua zitakapoanza Tena na maji kuongezeka mtoni, kwasasa maji haya yabaki Kwa matumizi ya binadamu tu, lakini pia tutafatilia wale wanaofanya kilimo kwa kutumia maji ya mto huu bila vibali na kusababisha changamoto katika mto” amesema Kunenge.
Vile vile Kunenge amesema, kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa Bwawa la Kidunda kutasaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya upungufu wa maji, kwani bwawa hilo litaruhusu uhifadhi wa maji ya kutosha bila kutegemea mvua za msimu.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya maji Mhandisi Mwajuma Waziri amewataka Bonde la maji Wami-Ruvu kwa kushirikiana na DAWASA kufanya jitihada za haraka na upesi kuboresha maeneo yenye changamoto katika mto Ruvu yanayopelekea maji kupotea na kupunguza wingi wa maji mtoni ili wananchi wananchi waendelee kupata huduma ya maji yenye uhakika.



