Na Mwandishi Wetu
Mahakama ya Wilaya ya Ilemela imewaachia huru watuhumiwa 57 kati 61 wa kesi ya uhaini waliokuwa wakishikiliwa kufuatia maandamano na matukio ya vurugu za baada ya uchaguzi yalitokea kuanzia Oktoba 29, 2025.
Uamuzi wa kufuta mashtaka hayo umetolewa leo Novemba 24,2025 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Stella Kiama, katika Mahakama ya Wilaya ya Ilemela iliyopo kwenye Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki, Buswelu.
Hatua hiyo imetokana na upande wa mashtaka, kupitia Wakili wa Serikali Mwandamizi, Safi Amani, kuwasilisha ombi la Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) la kutokuwa na nia ya kuendelea na mashtaka dhidi ya watuhumiwa hao waliokuwa wanakabiliwa na tuhuma mbalimbali.
Shauri hilo namba 26641/2025 limeletwa kwa ajili ya kutajwa kwa mara ya pili mahakamani hapo leo ambapo kwa mara ya kwanza lilitajwa Novemba 24, 2025.
Vijana hao ni miongoni mwa wale waliokuwa wamekamatwa na Jeshi la Polisi na baadaye kufikishwa Mahakamani wakidaiwa kuhusika kwa namna moja au nyingine kwenye maandamano yaliyozaa vurugu zilizopelekea uharibifu wa mali, majeruhi na vifo.


