Na Mwandishi Wetu
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ametangaza uteuzi Mawaziri 20, watakaunda Baraza jipya litakalosimamia utekelezaji wa sera za Serikali ya Awamu ya Nane katika kipindi cha pili cha uongozi wake.
Akizungumza leo Novemba 13, 2025, Ikulu Zanzibar, Rais Dk. Mwinyi amesema Serikali katika awamu hii itakuwa na wizara 20 badala ya 18 zilizokuwepo awali, ili kuongeza ufanisi wa utendaji Serikalini.
Amesema baraza hilo limeundwa ili kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi, kukuza uchumi wa Zanzibar na kusimamia maendeleo katika sekta mbalimbali.
Ameeleza kuwa uteuzi huo umezingatia uwiano wa kijinsia, uwakilishi wa Unguja na Pemba, pamoja na uzoefu wa viongozi katika sekta zao husika.

Aidha amesema kuwa nafasi za Wizara nne zikiwemo Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Afya, Utalii na Mambo ya Kale, pamoja na Biashara na Maendeleo ya Viwanda , zitaachwa wazi kwa muda hadi Serikali ikamilishe makubaliano na Chama cha ACT Wazalendo katika kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Chama cha ACT Wazalendo kimekidhi vigezo vya kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa kushirikiana na Chama cha Mapinduzi (CCM) na sasa kitakuwa na Makamu wa Kwanza wa Rais pamoja na mawaziri wanne.

Baadhi ya Mawaziri walioteuliwa ni:
Saada Mkuya – Waziri Ofisi ya Rais Ikulu
Haroun Ali Suleiman – Waziri wa Katiba, Sheria Utumishi wa Umma na Utawala Bora
Idrisa Kitwana – Waziri wa Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu
Rahma Kassim Ali -Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi.
Suleiman Masoud Makame – Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo
Shaaban Ali Othman –Waziri wa Vijana, Ajira na Uwezeshaji, Masoud Ali Mohamed Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi
Nadir Abdullatif Alwardy – Waziri wa Maji, Nishati na Madini
Anna Athanas Paul – Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
Mudrick Ramadhani Soraga- Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu
Riziki Pemba Juma –Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo
Hamza Hassan Juma –Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar.


