Na Tatu Mohamed
SERIKALI imesema itaendelea kuhakikisha vijana wa Kitanzania wanapata elimu na mafunzo ya ufundi stadi yenye umahiri, ubunifu na ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira la sasa na la baadaye, ili kuchochea maendeleo ya viwanda na uchumi wa taifa.
Kauli hiyo imetolewa leo Oktoba 17, 2025 jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, wakati akifungua mkutano wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) uliowakutanisha wamiliki wa viwanda, waajiri na wadau wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi.

Prof. Nombo amesema mkutano huo ni muhimu kama sehemu ya kutafuta suluhisho la pamoja kuhusu mahitaji ya ujuzi na ajira katika sekta mbalimbali nchini.
“Nia yetu mahsusi ni kuhakikisha tunazalisha nguvu kazi yenye ujuzi, umahiri na ubunifu unaokidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye ya soko la ajira, huku tukizingatia ushindani uliopo ndani ya nchi, kikanda na kimataifa,” amesema.

Amebainisha takwimu za kimataifa zinaonyesha kuwa asilimia 60 ya vijana duniani wako barani Afrika, hivyo kuna wajibu mkubwa kwa serikali na wadau kuhakikisha vijana wa Tanzania wanapata elimu na mafunzo yatakayowawezesha kushindana kimataifa.
Prof. Nombo amefafanua kuwa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 (toleo la 2023) imeweka mkazo katika kujenga mfumo wa elimu unaozingatia ujuzi, ubunifu na tija katika soko la ajira.

“Tanzania ipo katika hatua nzuri ya ukuaji wa sekta ya viwanda, lakini ukuaji huo hauwezi kufikiwa bila kuwa na watu wenye ujuzi. Tunahitaji ushirikiano wa karibu kati ya serikali, waajiri na wamiliki wa viwanda ili kuongeza tija,” amesisitiza.
Ameomba wamiliki wa viwanda na waajiri kufungua milango yao kwa wanafunzi wa vyuo vya ufundi stadi kupata uzoefu wa vitendo, pamoja na kuruhusu wataalamu kutoka viwandani kushiriki kufundisha katika vyuo vya VETA ili kuongeza ujuzi wa wanafunzi.
Aidha, Prof. Nombo amewataka wadau hao kuendelea kushirikiana na VETA katika kuendeleza programu ya wanagenzi ambayo imeonyesha mafanikio makubwa katika kuwajenga wahitimu wenye ufanisi katika sekta mbalimbali.

“Tunapojadili na kuimarisha ushirikiano huu, tuweke mbele maslahi mapana ya taifa. Tunaweza kuzalisha nguvu kazi yenye ubunifu wa hali ya juu itakayochochea maendeleo ya viwanda na uchumi wa Tanzania,” amesisitiza, huku akiahidi kuwa serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa uwekezaji na ukuaji wa viwanda.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Clotilda Ndezi, akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Prof. Sifuni Mchome, amesema mkutano huo unalenga kuimarisha ushirikiano kati ya watoa mafunzo, viwanda, waajiri na wadau wa maendeleo ya ujuzi.

“Tunatoa msukumo mkubwa kuhakikisha mafunzo ya ufundi stadi nchini yanakuwa ya vitendo zaidi na yanayoendana na mahitaji ya soko la ajira. Ili mwanafunzi awe na umahiri wa kweli, anapaswa kujifunza na kujaribu kwa vitendo kile anachofundishwa darasani,” amesema.
Amesisitiza kuwa mitihani na tathmini za wanafunzi zinapaswa kujikita zaidi kwenye vitendo ili kuzalisha wahitimu wanaoweza kufanya kazi kwa ufanisi pindi wanapoingia kazini.
“Viwanda ndivyo vyenye teknolojia na changamoto halisi za kiutendaji, hivyo tunawahimiza wamiliki wa viwanda kutoa nafasi za mafunzo kwa vitendo (field attachment na apprenticeship) kwa wanafunzi na walimu wa VETA,” ameongeza.
Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Suleiman Serera, amesema sekta ya viwanda ni injini ya uchumi na haiwezi kukua bila kuwa na rasilimali watu wenye ujuzi na umahiri.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, amesema serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka msukumo mkubwa katika kuboresha elimu ya ufundi stadi ili iwe shirikishi na inayoendana na mahitaji ya soko la ajira.
“Miaka mitano iliyopita tulikuwa na vyuo 37, lakini sasa tuna vyuo 80 vinavyofanya kazi, na vyuo vingine 65 viko hatua za kukabidhiwa. Hii inaonyesha dhamira ya serikali katika kuwekeza kwenye ujuzi wa Watanzania,” amesema.
