Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MRATIBU Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Wakili Onesmo Olengurumwa, amekosoa tamko la Chama cha Mawakili wa Serikali (PBA) lililopinga uamuzi wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) kuwataka wanachama wake kuandamana nchi nzima kulaani kukamatwa kwa Wakili Deogratius Mahinyila katika Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam.
Olengurumwa amesema hatua ya TLS ilikuwa sahihi kwani ililenga kuwalinda na kuwatetea mawakili wote nchini dhidi ya vitendo vya udhalilishaji au kuzuiwa kutekeleza majukumu yao ya kitaaluma.
“Uamuzi wa TLS ulikuwa wa kulinda heshima ya taaluma ya sheria na kuonesha mshikamano wa kitaaluma pale ambapo mwanachama anakumbwa na changamoto zinazodhoofisha uwezo wake wa kutekeleza majukumu yake kisheria,” alisema.
Ameongeza kuwa ni wajibu wa vyama vya wanasheria na taasisi za haki za binadamu kuhakikisha mazingira ya kazi za mawakili yanaheshimiwa bila hofu, vitisho au manyanyaso, kwani usalama wao ndio msingi wa haki na usawa mbele ya sheria.
Kwa mujibu wake, iwapo mawakili watakuwa huru na salama katika kutekeleza majukumu yao, wananchi nao hupata uhakika wa kulindwa na kuwakilishwa ipasavyo kwenye mahakama na vyombo vya utoaji haki.
Awali, PBA ilipinga msimamo wa TLS kwa maelezo kuwa maazimio yake yanakwenda kinyume na Katiba pamoja na Sheria ya Msaada wa Kisheria, ikisisitiza kuwa huduma hiyo si hiari bali ni wajibu wa kisheria.
Chama hicho kiliweka wazi kuwa kuzuia huduma za msaada wa kisheria ni hatua inayoweza kuchochea ubaguzi, kikibainisha pia kuwa mawakili, kwa nafasi yao kama maafisa wa mahakama, hawapaswi kuchukua hatua zinazoweza kuathiri upatikanaji wa haki kwa wananchi, hususan wenye kipato cha chini.
Aidha, PBA kimeitaka TLS kuhakikisha maamuzi na matamko yake yanazingatia weledi wa kisheria na maslahi mapana ya jamii, badala ya kuchukua hatua zinazoweza kufasiriwa kama za kiharakati.