Na Mwandishi Wetu
SERIKALI ya Austria kupitia Benki ya UniCredit imeahidi kuipatia fedha Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kiasi cha Euro Milioni 20 sawa na takribani Shilingi bilioni 60 kwa ajili ya Utekelezaji wa miradi ya kuzalisha umeme kwa kutumia jua na takataka.
Hayo yamesemwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Merl Solar Technologies GmbH, Mha. Hannnes Merl alipofanya mazungumzo na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mha. Felchesmi Mramba Septemba 17, 2025 pembeni ya Mkutano Mkuu wa 69 wa Shirika la Kimataifa la nguvu za Atomic unaoendela Jijini Vienna, Austria.

Ili kuanza utekelezaji wa miradi hiyo, Mhandisi Mramba ameikaribisha kampuni hiyo nchini Tanzania ili kukutana na wataalam na kuanza kufanya maandilizi stahiki ya miradi hiyo mipya ya kuzalisha umeme huku akiahidi kutoa ushirikiano katika kufanikisha Utekelezaji wa miradi hiyo.
Mha. Felchesmi Mramba ameeleza kuwa kampuni ya Merl imeshatekeleza miradi mbalimbali ya umeme wa jua nchini akisema “kampuni hii imetekeleza miradi ya umeme katika vijiji kumi (10) katika kipindi cha mwaka 2015 hadi 2017″.
Ametaja miradi hiyo kuwa ni ya makontena 14 ya kuzalisha umeme kwa kutumia nishati ya jua katika Wilaya za Kongwa mkoani Dodoma, Mlele mkoani Katavi, pamoja na Uyui mkoani Tabora ambapo mradi huo uligharimu kiasi cha shilingi bilioni 16.2.

Ameongeza kuwa miradi hiyo imewezesha kuzipatia umeme nyumba za makazi 812, nyumba za Ibada 27, Shule 6 na Vituo vya Afya 8.
Mha. Mramba ameishukuru Serikali ya Austria kwa kutekeleza miradi hiyo kwa ufanisi pamoja na nia ya Serikali ya Austria kuendeleza ushirikiano na Serikali ya Tanzania katika utekelezaji wa Mkakati Mahususi wa Nishati (National Energy Compact) unaolenga kupeleka umeme kwa watanzania wote ifikapo mwaka 2030 kupitia mpango wa misheni 300.
Kikao kati ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Kampuni ya Merl kimefanyika katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania Mjini Vienna nchini Austria na kuhudhuriwa na Balozi wa Tanzania na Mwakilishi wa Kudumu nchini Austria Balozi Naimi S. Aziz pamoja na Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mha. Innocent Luoga.