Na Mwandishi Wetu
Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Luhaga Mpina leo Septemba 11, 2025 ameshinda kesi ya kupinga kuzuiwa kurejesha fomu za uteuzi wa mgombea Urais aliyofunguliwa dhidi ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na mahakama kuamuru taratibu ziendelee zilipoishia.
Kesi hiyo namba 21692/2025, iliyofunguliwa na Bodi ya Wadhamini wa ACT Wazalendo pamoja na Lugaha Mpina, ikipinga uamuzi wa INEC kumuengua mgombea wao wa Urais, katika orodha ya wagombea.
Jopo la majaji watatu, Abdi Kagomba, Evaristo Longopa na John Kahyoza ndiyo waliokuwa wakisikiliza kesi hiyo. Majaji hao wamesema INEC ni Tume huru na haikupaswa kusikiliza maelekezo ya mtu au taasisi yoyote.


Mahakama imesema kitendo cha INEC kutopokea fomu za Mpina, ilimnyima haki ya kikatiba na ya kusikilizwa, hivyo kuamuru impe fursa mgombea huyo kuwasilisha fomu zake na mchakato uendelee ulipoishia.
INEC ilichukua uamuzi huo, kutokana na taarifa ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, aliyobainisha kuwa Mpina hakutimiza vigezo vya uanachama kwa mujibu wa kanuni za chama, pia kutokana na malalamiko ya kada wa chama hicho, Monalisa Ndala aliyedai kuwa mkutano mkuu uliompitisha Mpina haukufuata katiba.