Hizi ndizo hisia dhidi ya INEC, Msajili wa Vyama vya Siasa

KATIKA safu hii wiki iliyopita niliandika uchambuzi nikihoji, ‘INEC, Msajili wa Vyama wanaweza kutupa uchaguzi huru?’ Uchambuzi huo ulifanya ulinganifu wa vitu viwili, ufuasi wa mpira wa soka nchini na ule wa kisiasa. Nililinganisha nyanja hizo mbili, ambazo pengine baada ya imani za dini ndizo zinazovutia ufuasi mkubwa zaidi.

Msajili wa vyama vya siasa Jaji Francis S. Mutungi

Ulinganifu huo ulihoji ni kwa nini kwa mfano, ufuasi wa soka nchini uko juu sana kiasi cha kufanya viwanja vya michezo kufurika mashabiki. Au kuona mashabiki wakijitoa kwa hali na mali kuzibeba timu zao? Aidha, nilieleza wazi kwamba soka ulimwenguni kwa sasa ni moja ya burudani kubwa, lakini pia ni uchumi mkubwa. Nilieleza kwamba kwa mfano mtandao wa Soccer Worldwide unaeleza kuwa mapato ya soka kwa mwaka 2025 yanakadiriwa kufikia Dola za Marekani bilioni 59.1 duniani kote. Fedha hizo ni sawa na shilingi za Tanzania trilioni 153.66 kiasi kinachoweza kutosheleza bajeti ya taifa kwa miaka mitatu. Siasa kwa upande mwingine nilisema ni kila kitu. Ndiko maamuzi ya matumizi ya rasilimali yanafanyika. Ndiko hasa kilinge cha kuamua nini kifanyike kwenye nchi. Kwa maana hiyo, ilitarajiwa kwamba kila Mtanzania mwenye kujielewa hakika hawezi kupitwa na siasa.

Hivyo, ilitarajiwa hamasa kubwa na amsha amsha kubwa ionekane walau kwa mwaka wa uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani kama ilivyo mwaka huu. Isivyo bahati, hamasa na amsha amsha hiyo haipo. Swali langu likawa, kama soka inayosimamiwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) chini ya kanuni za ‘Fair Play’ imeweza kuhakikishia ulimwengu wa soka haki, uhalali wa ushindi unaoaminika, ni kwa jinsi gani taasisi muhimu hapa nchini, Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) inaweza kuwa chanzo cha kuwa na uchaguzi huru na haki? Au ni kwa jinsi gani Msajili wa Vyama vya Siasa naye anaweza kuwa na mkono wa kusaidia uchaguzi kuwa huru na haki, hivyo kusababisha hamasa na amsha amsha katika jamii juu ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025?

Baadhi ya wasomaji wa safu hii, wakiwamo walioandika mawazo yao  juu ya uchambuzi wangu na wale ambao tulizungumza ana kwa ana, walinilaumu kwamba niliwaacha njiani. Kwamba sikuonyesha ni kwa vipi INEC au Msajili wa Vyama vya Siasa wanaweza kusaidia kuwapo au kutokuwapo kwa uchaguzi huru na haki nchini. Kwa kifupi walisema kuwa nimekwepa kusema wazi wazi taasisi hizi mbili zinahusika vipi ama kuwapo kwa uchaguzi huru au kinyume chake. Yaani walitaka niseme tatizo ni nini?

Ninaheshimu na kuthamini sana mawazo ya wasomaji wangu. Nimepokea fikra zao tunduizi kwa moyo wa shukrani kubwa. Leo natamani nipige hatua moja mbele katika kufafanua niliyochambua wiki iliyopita.

Moja, wasomaji wangu wajizuia kusoma kwa nia ya kufanya ulinganifu wa siasa na soka. Kwamba kwa nini ukipita mitaani utasikia watu wengi, hasa vijana, wakisema hawataki kufuatilia siasa, ni nini hasa kinawakwaza? Je, kwa nini wanahamasika na soka, kiasi cha wengi wao kukubali kubeba gharama kubwa za ushabiki – kununua sare za timu wazipendazo; kusafiri masafa marefu kwenda kushangilia timu yao pendwa na kulipa gharama za viingilio. Kwa nini wako radhi kuingia gharama hizi? Pengine sababu kuu ni moja, walau wanaamini katika mchezo wa soka, kuna Fair Play. Kwenye siasa, hata pale wanapokuwa na matamanio ya mtu mwingine, uzoefu umeonyesha kwamba hapenyi. Kwa nini hapenyi ni kwa sababu pangine, FIFA ya siasa hapa kwetu ambayo kimsingi ni INEC na ikisaidiwa kwa karibu na Msajili wa Vyama vya Siasa, hawajasaidia sana kuwapo kwa uwanja sawa kwa watia nia wote.

Tunajua INEC itasimamia uchaguzi mkuu kwa mara ya kwanza mwaka huu kwa sababu ilianzishwa kwa sheria mwaka jana. Hata hivyo, makamishina wa INEC ni akina nani? Siyo wale wale waliokuwa wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)? Ambao mwaka 2020 walisimamia uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani ulioacha kilio nchini kote kwa jinsi ulivyoendeshwa?

Ni kweli kwa ujumla wake sheria ya INEC ina mambo mazuri; kwa mfano sheria inaitaja kuwa ni chombo huru kisichoingiliwa na yeyote; maamuzi yake ni ya mwisho; makamishina wake watapatikana kwa njia ya usaili kupitia Kamati ya Usaili kabla ya kuteuliwa na Rais pamoja na mambo mengine mazuri ambayo nafasi haitoshi kuorodhesha. Hata hivyo, uamuzi  wa kusonga mbele na watu ambao mpaka leo hawajawahi kueleza ilikuwaje mwaka 2020 kukawa na aina ya uchaguzi ule, na ni kwa kiwango gani hayatajirudia, inaibua hisia siyo nzuri? Kwa mfano, makamishina wa INEC hawatakiwi kufungamana na chama chochote cha siasa. Je, ni kweli mle ndani hawapo wanaofungamana na vyama vya siasa?

Niwaalike wasomaji wangu katika mjadala ambao umekuwako nchini kwa kitambo sasa juu ya marekebisho ya kisheria, kanuni na taratibu za uchaguzi. Ni kweli mwaka jana yalifanyika marekebisho na utungaji wa sheria mpya za kusimamia uchaguzi mkuu. Miongoni mwake ni sheria ya INEC ya mwaka 2024; Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2024 na Marekebisho ya Sheria ya Usajili wa Vyama vya Siasa ya mwaka 2024. Marekebisho yote haya yalifanyika mwaka jana. Isivyo bahati, baadhi ya watu waliokuwako katika ofisi hizo kabla ya marekebisho ni wale wale. Ipo hoja kwamba ni nini hicho kilikuwa kigumu cha kubadili kila kitu, kama kuteua watu wapya ili kuanza katika uwanja mpya ambao hauna anayehisiwa kuwa na waa kwa  yaliyojitokeza mwaka 2020?

Wakati tukiendelea kusubiri uteuzi wa mwaka huu kwa wabunge na watia nia urais, na jana Jumatano Agosti 27, 2025 ikiwa ni siku ya uteuzi kwa INEC, ni vema kuwa na imani kwamba huenda haki ikatendeka. Lakini, hadi kufikia jana katika mchakato mzima, zimekuwako hoja gani juu ya Fair Play na zimeshughulikiwa vipi?

INEC inasema kuwa watia nia wa kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makamu wa Rais katika uchaguzi wa mwaka huu ni kutoka vyama 18 vilivyokuwa vimewateua wagombea wao wa urais na umakamu kwenda kuchukua fomu hizo.

Orodha ya watia nia ambao walichukuwa fomu INEC ni Samia Suluhu Hassan na Dk. Emmanuel Nchimbi (CCM); Hassan Kisabya Almas na Hamisi Ally Hassan (NRA); Kunje Ngombale Mwiru na Shum Juma Abdalla (AAFP); Doyo Hassan Doyo na Chausiku Khatib Mohamed (NLD); Coster Jimmy Kibonde na Aziza Haji Suleiman (MAKINI); Twalib Ibrahim Kadege na Abdalla Mohd Khamisi (UPDP); na Georges Gabriel Bussungu na Ali Makame Issa (TADEA).

Wengine ni Mwajuma Noty Mirambo Mashavu Alawi Haji (UMD); Yustas Mbatina Rwamugira na Amana Suleiman Mzee (TLP); David Daud Mwaijojele na Masoud Ali Abdala (CCK); Salum Mwalimu na Devotha Mathew Minja (Chaumma); Abdul Juma Mluya na Sadoun Abrahman Khatib (DP); Majalio Paul Kyara na Satia Mussa Bebwa (SAU); Gombo Samandito Gombo na Husna Mohamed Abdalla (CUF); Wilson Elias Mulumbe na Shoka Khamis Juma (ADC); Saum Hussein Rashid na Juma Khamis Faki (UDP); Haji Ambar Khamis na Dkt. Eveline Wilbard Munisi (NCCR-MAGEUZI); na Luhaga Joelson Mpina na Fatma Abdulhabib Ferej (ACT – WAZALENDO). Tusubiri kwani subira huvuta kheri.

spot_img

Latest articles

TACTIC yaimarisha huduma za usafiri na usafirishaji Manispaa ya Sumbawanga

Na Mwandishi Wetu MRADI wa Uendelezaji Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC) unaelezwa kuimarisha huduma...

Mradi wa TACTICS waleta mageuzi ya miundombinu Morogoro

Na Mwandishi Wetu MRADI wa Uendelezaji Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC) unaelezwa kuboresha miundombinu...

Geofrey Timothy achukua fomu ya kugombea Ubunge Jimbo la Kawe

Na Mwandishi Wetu MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Kawe kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Geofrey...

UVCCM yazindua Mfumo wa Kijani Ilani Chatbot

Na Mwandishi Wetu MWENYEKITI wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM)...

More like this

TACTIC yaimarisha huduma za usafiri na usafirishaji Manispaa ya Sumbawanga

Na Mwandishi Wetu MRADI wa Uendelezaji Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC) unaelezwa kuimarisha huduma...

Mradi wa TACTICS waleta mageuzi ya miundombinu Morogoro

Na Mwandishi Wetu MRADI wa Uendelezaji Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC) unaelezwa kuboresha miundombinu...

Geofrey Timothy achukua fomu ya kugombea Ubunge Jimbo la Kawe

Na Mwandishi Wetu MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Kawe kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Geofrey...