Na Jesse Kwayu
JUMATATU wiki hii, yaani Agosti 4, 2025, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilihitimisha mchakato wa kura ya maoni kwa wanachama wake waliotia nia ya kupata ridhaa ya chama hicho kuwania ubunge katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu. Wajumbe wa ngazi ya jimbo, kata, matawi na nyumba kumikumi walikuwa kwenye kazi pevu ya kuwasilikiza watia nia wote waliokuwa wanaomba ridhaa ya chama hicho kuteuliwa kuwania ubunge mwaka huu. Kwa waliokuwa wanafuatilia mchakato huo tangu mwanzo wa uchukuaji wa fomu, watashuhudia kuwa haukuwa mchezo mwepesi.
Mchakato wa kutafuta tikiti ya kuwania ubunge na udiwani kupitia CCM mwaka huu umekuwa na mambo mengi ya kufikirisha. Chama hicho mapema mwaka huu kilifanya marekebisho ya mfumo wa upigaji kura za maoni kwa ngazi ya watia nia katika ngazi ya udiwani na ubunge. Marekebisho hayo, awali yalihusu kupanua wigo ndani ya chama juu ya idadi ya wajumbe wa kupiga kura za maoni. Yapo majimbo ambayo yalijikuta yakiwa na wajumbe zaidi ya 10,000.
CCM ilisema kwamba nia ya kufanya marekebisho hayo ilikuwa ni kupanua demokrasia na ushiriki wa wanachama wengi zaidi katika hatua ya kura ya maoni. Hii iliongeza wajumbe kiasi cha kufikirika kuwa itakuwa ni vigumu rushwa kutumika kama kichocheo cha mtu kuchaguliwa. Kupanuliwa kwa wigo huo, hapana shaka ulikuwa ni mwitikio wa uongozi wa CCM kujaribu kujibu malalamiko ya miaka mingi sasa kwamba wajumbe wanaoshiriki mchakato wa kupiga kura ya maoni, wamekuwa wakihongwa fedha nyingi na watia nia. Kwa maana hiyo, mchakato wa kutafuta nani hasa anaungwa mkono na idadi kubwa ya wanachama ndani ya chama hicho ukageuzwa kuwa ni kama ‘gulio’ kubwa la kuuza kura. Kwamba mwenye donge nono la kuwahonga wajumbe, ndiye alikuwa anapenya.
Kwa maana hiyo, kuongeza idadi ya wajumbe wa kuamua ni mtia nia yupi anafaa ulikuwa ni mkakati wa kuvunja ‘gulio’ la kura. Wapo watu tangu siku ya kwanza kabisa ya kufanyika kwa mabadiliko hayo, waliona kwamba dawa ya kutokomeza ununuaji wa kura, ilikuwa imepatikana. Ni kwa kiwango gani hatua hii imevunja na kuondoa kabisa utamaduni wa ‘gulio’ la kura, ni jambo ambalo haliwezi kupata majibu kwa haraka, ila tu itoshe tu kusema kuwa safari hii kazi ya ununuzi wa kura ilikuwa ngumu na mzito kuliko hapo kabla, hasa katika nafasi ya kuwania ubunge.
Hata hivyo, pamoja na ukweli kwamba CCM ilikuwa imekwisha kufanya mabadiliko ya katiba yake mapema mwaka huu, mwezi uliopita, yaani Julai, iliamua tena kufanya mabadiliko mengine madogo katika masuala ya kura ya maoni. Awali, mabadiliko ya katiba ya CCM yalikuwa yameruhusu kila mwanachama wake awe huru kuomba ridhaa hiyo, kwanza kwa kuchukuwa fomu na kwamba majina yote yangepelekwa mbele kutoka majimboni hadi ngazi ya Kamati Kuu, ambayo ingerejesha majina matatu tu kwa ajili ya kupigiwa kura kwenye majimbo. Taarifa iliyotolewa na chama hicho ilisema kwamba ilibidi kufanyika kwa mabadiliko madogo ya katiba ili sasa kuruhusu majina zaidi ya matatu kurejeshwa kwa wanachama kutoka Kamati Kuu ili yakapigiwe kura.
Hatua hii ya kufanya tena marekebisho hayo, ilielezwa kwamba ilikuwa katika nia ile ile ya kupanua wigo wa demokrasia ndani ya chama, na pia ilikuwa ni kutafuta jinsi ya kutambua, kuheshimu na kutoa fursa kwa wanachama wake ambao kwa mwaka huu walikuwa wamejitokeza kwa wingi zaidi kuchukuwa fomu kutafuta ridhaa ya chama hicho kuwateua. Kwa maana hiyo, marekebisho hayo madogo ya Julai mwaka huu, yalikuwa ni ya kuthibitisha kwamba CCM ni chama sikivu na ambacho wakati wote kinasikiliza maoni ya wanachama wake kulingana na uhitaji wa nyakati husika.
Utayari huu wa CCM ulinifikirisha. Ulinipa funzo kwamba hakuna kinachoshindikana kufanyika. Hata katika hali ambayo muda na hata rasilimali nyingine vinakuwa vimebana, bado kuna upenyo wa kufanya kitu. Kwamba CCM imeweza kufanya mkutano mkuu maalum kwa njia ya mtandao ili kukidhi kiu ya wanachama wake katika mchakato wa uchaguzi, siyo jambo dogo wala jepesi.
Katika kufikiri kwangu nikajiuliza, kama tumepiga hatua kiasi hiki; kwa usikivu huu; hivi ni nini hasa kinasababisha madai, kilio na maoni mengine yanayotolewa na wananchi nje ya mfumo wa CCM yasizingatiwe?
Kwa mfano, hakuna Mtanzania mwenye akili timamu asiyejua wazi nini kilifanyika katika chaguzi za serikali za mitaa mwaka 2019 na ule wa uchaguzi mkuu wa 2020. Kwamba kuna mambo ya msingi sana yanayoupa uchaguzi kuwa mchakato huru, wa haki na kuaminika, yalisiginwa mno. Wapo waliofikia hata hatua ya kusema chaguzi hizo, hazikuwa chaguzi, bali uchafuzi. Wajenga hoja hii wamekuwa wakitamani kufanyika kwa mabadiliko ya kisheria ya kuwezesha uchaguzi uwe huru, wa haki na wa kuaminika.
Katika mvutano huu wa hoja, wapo wanaosema kwamba mabadiliko makubwa ya mfumo wa uchaguzi nchini Tanzania yamefanyika, ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kwa kutungwa kwa sheria yake mahususi; pia kutungwa kwa sheria moja ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani pamoja na kufanyika kwa marekebisho makubwa ya sheria ya vyama vya siasa.
Katika muktadha huo, wajenga hoja kwamba mabadiliko makubwa yamefanyika, wanakwama au kukataa kutambua mambo mawili. Moja, kwamba pamoja na INEC kuundwa kwa sheria yake ya mwaka 2024 bado makamishina wa iliyokuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ndiyo wamefaulishwa kuwa makamishna wa INEC. Kwamba katika utekelezaji wa sheria ya INEC kwa maana ya kuanza kwa mchakato wa kupata makamisha wake kwa mujibu wa sheria yake, haukufanyika. Pili, utekelezaji wa sheria ya INEC ni wa vipande vipande, kama ambavyo pia INEC haikusimamia uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2024 ingawaje ni jukumu lake.
Nimesema hapo juu, tumeona kasi, nia na dhamira ya CCM katika kukidhi kiu ya wanachama wake katika kushiriki uchaguzi katika mchakato wa ndani ya chama. CCM imefanya vizuri sana. Hata muda ulipobana, ulitafutwa upenyo halali wa kikatiba kukidhi kiu ya wanachama wake. Ni halali kabisa kusema kwamba mwaka 2025 mchakato wa kura ya maoni ndani ya CCM ulikuwa wa kihistoria, niazime maneno ya kimombo ‘was very responsive’. Hii ni historia ambayo haijawahi kushuhudiwa labda tangu mfumo wa vyama vingi urejee nchini mwaka 1992.
Sasa katika mawazo haya chanya, katika usikivu huu, ni nini hasa kinakwamisha haya yanayolalamikiwa katika walau kilichoitwa ‘minimum reforms’ kufanyika ili mwaka huu kweli INEC ionekane ni chombo huru cha kusimamia uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani na siyo taasisi iliyosheheni makada wa chama tawala? Ni kwa nini CCM kwa mambo yake ya ndani ina kasi, ari na uthubutu wa kufanya mabadiliko, marekebisho ya katiba yake, kanuni na taratibu zake ili kwenda na wakati, lakini inapokuwa nje yake, serikali inayoiongoza imekuwa nzito mno kukubali mabadiliko hayo? Nani hasa anavuta wenzake shati katika kutekelezwa kwa mabadiliko ya dhati kwenye mfumo wa uchaguzi mkuu wa taifa letu.