Na Mwandishi Wetu, Mwanza
Jumla ya waandishi wa habari 31 kutoka mkoa wa Mwanza wamekutana Hoteli ya Lenana katika mafunzo ya siku moja kuhusu demokrasia na uandishi wa habari wakati wa uchaguzi, wakati taifa likielekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa Tanzania utakaofanyika Oktoba 2025.
Mafunzo hayo yaliandaliwa na Kampuni ya Media Brains kwa ushirikiano na Konrad Adenauer Stiftung (KAS), yakilenga kuwajengea uwezo waandishi wa habari kuhusu masuala ya kisheria, maadili ya taaluma, usalama wa waandishi wa habari, na usawa wa kijinsia kwa ajili ya kuhakikisha uandishi wa haki, sahihi na unaoelimisha jamii wakati wa uchaguzi.
Akiwasilisha mada katika mafunzo hayo, Absalom Kibanda ambaye ni Mkurugenzi Mwenza wa Media Brains, alizungumzia historia ya sheria za uchaguzi nchini , huku akiweka wazi mabadiliko kadhaa yaliyofanyika kwa kutungwa sheria mpya ambazo ni Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ya Mwaka 2024, Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2024 na mabadiliko yaliyofanywa katika Sheria ya Vyama vya Siasa.

Kibanda alisisitiza umuhimu wa waandishi wa habari kuzisoma na kuzielewa kwa undani sheria hizo akizitaja kuwa nyenzo muhimu za kuwawezesha waandishi wa habari kutekeleza majukumu yao ipasavyo ya kuuelimisha umma wakati wa mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
“Kama waandishi wa habari, uwezo wenu wa kuelewa mchakato wa uchaguzi na kuuliza maswali sahihi unategemea uelewa wenu wa sheria,” Kibanda alisisitiza. “Huwezi kuripoti kwa ufanisi kama huelewi sheria zinazotawala uchaguzi unaouandikia.”


Aidha, alitoa mtazamo wa kina kuhusu mageuzi ya hivi karibuni, kama vile kubadilishwa kwa jina la NEC kuwa INEC (Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi) pamoja na kuanzishwa kwa mchakato shindani wa uteuzi wa makamishna wa tume hiyo, licha ya mabadiliko hayo kuonekana kutokodhi kiu takiwa kwa wadau hasa vyama vya siasa vya upinzani.
Kadhalika baadhi washiriki wa mafunzo walionyesha wasiwasi kwamba uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika mwaka jana haukuonesha tofauti kubwa, kwani bado maafisa walioteuliwa kisiasa ndio waliendesha shughuli za uchaguzi.

Katika majadiliano ya pamoja, washiriki walibaini kuedelea kuwepo kwa upungufu katika mfumo wa uchaguzi wa Tanzania ukilinganishwa na majirani kama Kenya na nchi nyingine barani Afrika.
Upungufu huo ni pamoja , matokeo ya uchaguzi wa urais kutopingwa mahakamani hata kama kuna malalamiko ya ukiukwaji wa taratibu, marufuku dhidi ya wagombea binafsi katika nafasi zote, mvutano na ukosefu wa uwazi katika mipaka ya majukumu kati ya Tume ya Huru yay a Taifa ya Uchaguzi (INEC) na Msajili wa Vyama vya Siasa na ukosefu wa usawa wa kijinsia hasa wanawake kutopewa nafasi stahiki katika mifumo ya uchaguzi.
Washiriki walibainisha kuwa licha ya marekebisho ya sheria na kutungwa kwa sheria mpya kuwa hatua muhimu katika maboresho ya uchaguzi, bado unahitajikwa utashi wa kisiasa katika utekelezaji wa sheria hizo.
Kwa upande wake Jesse Kwayu ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Media Brains, aliwasilisha mada kuhusu nafasi ya vyombo vya habari katika uchaguzi mkuu, alisisitiza umuhimu wa kuzingatiwa kwa maadili ya uandishi wa habari na kuripoti kwa kuzingatia usawa wa kijinsia.

“Hatuwezi kuzungumzia demokrasia na kuwaacha wanawake nyuma,” alisema Kwayu. “Waandishi wa habari hawapaswi kuripoti tu ukweli, bali kuhakikisha kwamba sauti za wanawake, vijana, na makundi mengine yaliyotengwa zinasikika kwa haki na usawa.”
Washiriki walijadili masuala ya kijinsia katika kampeni, wakichambua jinsi vyombo vya habari vinavyopaswa kuwapa nafasi wagombea wanawake kuripoti masuala ya sera, sifa za uongozi, na vikwazo vya kimfumo vinavyowazuia wanawake kushiriki kikamilifu kwenye mchakato wa uchaguzi.
Kahalika katika mjadala huo, washiriki walizungumzia changamoto wanazokutana nazo, zikiwemo hofu ya usalama wao wakati wa uchaguzi, uelewa wa sheria na mashinikizo ya kitaaluma.

Peter Koch, Mwakilishi Mkazi wa Konrad Adenauer Stiftung, alifunga mafunzo hayo kwa kuwapongeza waandishi wa habari kwa kujitolea kwao na kusisitiza nafasi ya msingi ya vyombo vya habari katika mfumo wa utawala wa kidemokrasia.
“Uchaguzi huru, wa haki, na wa kuaminika unategemea uwepo wa vyombo vya habari vyenye taarifa sahihi na vinavyowajibika,” Koch alisema. “Tunaamini kazi yenu itasaidia kulinda uhalali wa taasisi za kidemokrasia nchini Tanzania.”