YAPO MATAMANIO YA UCHAGUZI WA 2019 KUJIRUDIA 2024?

KUNA uhusiano wowote kati ya mafanikio ya kiuchumi kwa nchi yoyote na kukua kwa mfumo wake wa kisiasa? Hili ni swali linaloonekana kuumiza vichwa vya wachambuzi wanaotafuta uhusiano chanya baina ya nyanja hizo kuu za maisha ya binadamu. Uchumi na siasa.

Katika maendeleo ya miaka ya hivi karibuni yanaonyesha kwamba uchumi wa Tanzania umepiga hatua kubwa. Kwa sasa Tanzania inatajwa kuwa katika ulimwengu wa nchi ya kipato cha ngazi ya kati kiwango cha chini (lower middle income). Taarifa hii ni kwa mujibu wa ripoti ya Benki ya Dunia ya mwaka 2024 – 2025 juu ya viwango vya vipato vya nchi zote duniani.

Tanzania tangu uhuru mwaka 1961 imekuwa ikitajwa kuwa ni nchi masikini ya kipato cha chini, ikiwa ni miongoni mwa nchi ambazo zimekuwa zikitajwa kwamba zinahitaji misaada ya aina mbalimbali, kama mitaji ya fedha, utaalamu, tekinolojia ili kujinasua kwenye mkwamo wa umasikini. Hata hivyo, kuanzia mwaka 2020 Tanzania ilianza kuonyesha dalili ya kujinasua kwenye mnyororo wa umasikini huo pale ilipotangazwa kwamba imejikongoja kutoka kundi la nchi masikini zaidi zenye kipato cha chini kabisa duniani.

Kwa mujibu wa ripoti ya Benki ya Dunia ya 2024 -2025 ya viwango vya vipato, Tanzania sasa ina pato la mtu la Dola za Marekani la 1,080 ikiwa imepanda kutoka pato la Dola za Marekani 704.62 kiwango ambacho ni wastani uliokuwa ukielezwa kutawala Tanzania kwa miongo kadhaa. Hatua hizi chanya za kiuchumi ni habari zinazoamsha matumaini kwa wananchi kwamba mipango ya kiuchumi na sera mbalimbali zinazotekelezwa zinaweza kupunguza umasikini wa taifa hili.

Uchumi unapostawi nchi hufunguka katika nyanja nyingi, hufunguka katika siasa na hata kijamii pia. Wakati tukishuhudia hatua hizi chanya za kiuchumi, tangu mwaka 2019 tumekuwa tukishuhudia hatua hasi katika uwanja wa kisiasa nchini.

Kwa mara ya kwanza tangu kurejea kwa mfumo wa vyama vingi nchini mwaka 1992 na kufanyika kwa uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi wa serikali za mitaa mwaka mwaka 1994, kisha zikafuata za mwaka ya 1999, mwaka 2004, mwaka 2009 na mwaka 2014 ni uchaguzi za wa 2019 Tanzania ilishuhudia mwelekeo mpya wa uchaguzi huo ambao ulirejesha nyuma hatua chanya zilizokuwa zimepigwa katika ushindani wa kisiasa. Uchaguzi huo ulionyesha kumomonyoka kwa mafanikio yaliyokuwa yamejengeka na kuimarika katika demokrasia ya vyama vingi.

Ni kwa mara ya kwanza uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2019 ulidhihirisha kwamba Watanzania wapo wa aina mbili, kwamba wagombea wa vyama vya upinzani kwa ujumla wao walionekana hawajui kujaza fomu za kugombea nafasi hizo. Asilimia kubwa ya wagombea hao walienguliwa kwa kuwa walishindwa kujaza fomu za kugombea. Wakati wagombea hao wakienguliwa kwa asilimia kubwa, wale waliosimama kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), chama tawala, wao walionekana kwamba walijaza fomu hizo sawasawa, hivyo kupitishwa na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi huo.

Hali hii ya mwaka 2019 iliibua malalamiko makubwa kutoka kwa wafuasi wa vyama vya upinzani. Hali hiyo ilibaki hivyo na matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka huo, ulionyesha kwamba Watanzania wanakuwa na uwezo wa kusoma na kujaza fomu za kugombea nafasi kuchaguliwa kutokana na nasaba na chama cha siasa wanachoshabikia. Kwamba wale wa CCM wanajua kusoma vema na kujaza fomu kwa usahihi, wakati wake wanaotokana na vyama vya upinzani kwa ujumla wao hawajui kusoma vema, hivyo hawawezi kujaza kwa usahihi fomu za kugombea nafasi hizo.

Hii ni rekodi iliyowekwa mwaka 2019. Kumekuwa na taarifa nyingi zikionyesha kukosoa jinsi uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2019 ulivyoendeshwa. Matokeo ya uchaguzi huo yalidhihirisha kwamba wakati taifa linapiga hatua kubwa kwenye eneo la kiuchumi kama ambavyo nchi ilipanda kutoka uchumi wa kipato cha chini hadi kipato cha kati, eneo la siasa Watanzania walikuwa wanarejea nyuma kwa kasi. Kwamba ule uwezo wa Watanzania wa kumudu kujaza fomu kama ilivyokuwa mwaka 1994, 1999, 2004, 2009 na 2014, ilipofika 2019 uliporomoka na kupotea kabisa kwa kuwa tu mtu ana nasaba na chama cha siasa cha upinzani.

‘Ugonjwa’ huu wa kuporomoka kwa uwezo wa kujaza fomu kwa watu wa itikadi ya vyama vya upinzani uliovamia nchi hii mwaka 2019 unaonekana kujirudia tena kwa njia ile ile mwaka huu wa 2024. Tayari vilio na malalamiko makubwa yamesikika nchini kote kwamba wagombea wa vyama vya upinzani wameenguliwa kugombea nafasi hizo kwa madai ya kwamba wameshindwa kujaza fomu za kuwania nafasi hizo.

Tafakari ya ‘ugonjwa huu mpya wa kisiasa’ inaibua maswali mengi ambayo hayana majibu. Kubwa la yote ni je, taifa letu limekinai mfumo wa vyama vingi? Je, kuna hofu ya kuendelea kulea mfumo wa vyama vingi nchini? Je, mfumo wa vyama vingi unaangaliwa kama hasara kwa taifa ambao hausaidii lolote kuchochea maendeleo na ustawi wa watu wake?

Kabla ya kutafakari hali hii, Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Emmanuel Nchimbi, Jumanne wiki hii aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kueleza wito wa Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan kwa mamlaka za kuendesha uchaguzi huo mwaka 2024 kupuuza makosa madogo madogo ya mapingamizi ambayo yamesababisha kuenguliwa kwa wagombea wengi. Alisema hatua hizo zitasaidia kulea demokrasia ya Tanzania ambayo kimsingi bado ni changa.

Wakati taifa likipitia wimbi hili, ni muhimu kutambua kwamba mfumo wa vyama vingi ni kichocheo kikubwa cha maendeleo. Mfumo imara wa vyama vingi unasaidia kuwafanya waliopewa ridhaa ya kuongoza kuwa macho katika kutekeleza wajibu wao sawasawa. Nchi nyingi ambazo mfumo wa vyama vingi umestawi, umejengewa sheria na mazingira rafiki kwa vyama vya siasa kufanya shughuli zake, umesaidia sana kukuza uwajibikaji na utawala bora.

Wakati nchi ilipokubali kuingia katika mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992, ilikwisha kujiendesha kwenye mfumo wa chama kimoja tangu mwaka 1965, kwa maana hiyo kwa takribani miongo mitatu taifa hili liliishi katika mfumo wa chama kimoja, lakini ilionekana ni vema kurejea kwenye mfumo wa vyama vingi.

Ni vigumu kuelewa kiongozi anayechaguliwa na wananchi anapata woga gani kushindana kisiasa katika kuwatumikia wananchi. Wiki mbili zilizopita katika safu hii niliuliza “Watawala wanawahofia wananchi katika uchaguzi?” Niligusia hali ya chaguzi katika nchi mbalimbali duniani, Afrika, Ulaya na Asia ambazo waliokuwako madarakani, wamefungashwa virago kwenye sanduku la kura kwa sababu wananchi hawakuridhishwa na utendaji wao katika kipindi walichokuwa madarakani.

Uchaguzi ni kipimo cha usahili cha wananchi dhidi ya walioomba ridhaa ya kuongoza na wakapewa, wanapimwa kati yao na waombaji wengine. Je, uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2024 kwa dalili na sura iliyokwisha kujitokeza inatoa fursa ya kweli kwa wananchi kufanya usahili wa haki juu ya wote wanaotafuta ridhaa ya kuongoza serikali katika ngazi ya awali kabisa ya madaraka ya dola?

Ni kwa kiwango gani Tanzania ambayo imekuwa kisiwa cha amani, imejitahidi kwa zaidi ya miongo mitatu kujenga mfumo wa demokrasia ya siasa ya vyama vingi, inaridhishwa na kinachoendelea nchini kwa sasa? Ni kwa kiwango gani yanayoendelea katika maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024 yataakisi uzingatiaji wa sheria, kanuni na miongozo ambayo inawapa wananchi fursa ya kugombea na kuchagua viongozi wao kwa haki na uhuru? Je, tunapiga hatua katika nyanja za kisiasa au tunarejesha taifa letu nyuma?

spot_img

Latest articles

Hivi vikosi kazi vimerejea kwa mlango wa nyuma?

KUNA kila dalili kwamba taifa letu kidogokidogo linakumbwa na hali ya kutokuaminiana. Hali hii...

Chondechonde Polisi msisababishe wananchi wakate tamaa

ALHAMISI iliyopita yaani Desemba 5, mwaka huu wa 2024 lilitokea tukio baya la kuhuzunisha...

Ufaransa yaipatia Tanzania Sh bilioni 323.4

Na Mwandishi Wetu Serikali ya Tanzania na Shirika la Maendeleo La Ufaransa (AFD) wamesaini mikataba...

TANZANIA YAWEKA REKODI MKUTANO WA WAHASIBU WAKUU AFRIKA

Na Mwandishi Wetu Tanzania imeweka rekodi ya Mkutano wa Pili wa Wahasibu Wakuu wa Serikali...

More like this

Hivi vikosi kazi vimerejea kwa mlango wa nyuma?

KUNA kila dalili kwamba taifa letu kidogokidogo linakumbwa na hali ya kutokuaminiana. Hali hii...

Chondechonde Polisi msisababishe wananchi wakate tamaa

ALHAMISI iliyopita yaani Desemba 5, mwaka huu wa 2024 lilitokea tukio baya la kuhuzunisha...

Ufaransa yaipatia Tanzania Sh bilioni 323.4

Na Mwandishi Wetu Serikali ya Tanzania na Shirika la Maendeleo La Ufaransa (AFD) wamesaini mikataba...