KUNA vitu Mungu alimkirimu binadamu bure ambavyo anavipata bila jasho. Kwa mfano hewa tunayovuta ni bure, katukirimu Mungu. Uwezo wa kuzungumza tumetunukiwa bure, hakuna anayetoka jasho ili azungumze. Mazungumzo yana maana sana katika uhusiano, katika jamii, tunaelezwa kwamba hata wanyama hayawani wanazungumza, wana lugha zao.
Duniani hapa mataifa yameparaganyika kwa sababu tu ya kushindwa kuzungumza. Kwa mfano kwa sasa hivi vita inayoendelea Mashariki ya Kati kati ya Israel na Hamas ambayo inadaiwa kuchochewa zaidi na tukio la Oktoba 7, mwaka jana ambalo Hamas walivamia Israel na kuua watu na kundoka na wengine mateka, ni kushindikana kwa mazungumzo ya kumaliza mzozo baina yao.
Ukisikiliza kinachoendelea Sudan kati ya vikosi vya Jeshi la Msaada wa Haraka (RSF) na Jeshi la Sudan vita ambavyo vimesababisha vifo vya maelfu na mamilioni kukimbilia ukimbizini, ni kushindikana kwa mazungumzo baina ya pande mbili zinazohasimiana.
Mazungumzo ni kitu chepesi, lakini kina umuhimu wa kipekee.
Jumatatu wiki hii Jiji la Dar es Salaam lilikuwa limepambwa na vikosi vya polisi wakiwa katika mavazi rasmi ya kukabiliana na vurugu. Magari maarufu kama ‘magari washa’, yalikuwa yamevinjani kila kona, tayari kukabiliana na kile kilichokuwa kimetangazwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) maandamano.
Wakati Chadema wakisema wataandamana, Polisi walisema maandamano hayo ni batili, kwamba taarifa zao za kiintelejensia zilitaarifu kwamba hayakuwa ya kheri bali shari. Chadema walisisitiza ni ya amani. Mwisho kila upande ukabaki na msimamo wake, kwamba ni ya amani na mwingine ni ya shari kwa hiyo ni marufuku.
Matokeo ya kauli za ‘maandamano ya amani’ na ‘maandamano ya shari’ Jumatatu wiki hii ndiyo yalihitimisha yote yaliyoshuhudiwa kwa viongozi kadhaa wa Chadema kukamatwa. Wapo pia waandishi wa habari waliokamatwa kwenye kadhia hiyo. Orodha imetolewa ya waliokamatwa wakituhumiwa kukaidi amri ya Polisi ya kuzuia maandamano yaliyokuwa yanaelezwa ni ya amani huku wengine wakisema ni ya shari.
Kuna swali la kujiuliza, ni kwa nini hatuzungumzi kama taifa kuhusu jambo lolote liwe gumu au jepesi kila unapoibuka utata? Ni kwa nini mazungumzo ambayo ni kitu cha bure, kisichohitaji fedha ziwe za ndani au nje, au mali ghafi au rasilimali yoyote kufanyika, hatuyataki ila tunataka kukomeshana kwa amri, maguvu na vitisho?
Kama kuna kitu kama taifa tulivuna kutokana na tukio la Jumatatu wiki hii ni doa. Doa hili halitupi taswira nzuri siyo ndani ya nchi wala nje, kwamba tumeshindwa kuonyesha sisi ni jamii ya watu wastaarabu wanaoweza kuendesha mambo yao kwa mazungumzo na yakaisha bila mtu yeyote kupata madhara yoyote.
Hakuna madhara yoyote siyo ya gharama ya kuweka vikosi vya polisi barabarani usiku na mchana, kuendesha magari kwa gharama kubwa, na wala hakungekuwa na madhara kwa wafuasi wa Chadema ambao sasa pamoja na viongozi wao wamekamatwa.
Demokrasia kwa kawaida ina gharama zake. Moja ni pamoja na kukubali kwamba kuna kauli kinzani zitatolewa kila mara. Kwamba alimradi mmekubaliana kwamba mtaendesha nchi kwa mfumo wa demokrasia ya vyama vingi, ni lazima kutambua wakati wote kwamba kauli kinzani, kauli kinyume, kauli za kupingana zitakuwako tu. Nasisitiza kauli. Siyo vitendo vya kihalifu. Katika kauli hizo, watu wanakuwa na haki ya kusimama na kusema, watu wanakuwa na haki ya kusema na kutembea kwa maandamano ya pamoja au hata ya mtu mmoja mmoja kwenda kueleza kwa kauli kwa nini hakubaliani na kitu fulani. Mambo haya ni haki ambayo tuliamua kuzirejea tena mwaka 1992 baada ya kuwa tumeyaharamisha tangu mwaka 1965 tulipofanya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa nchi ya chama kimoja cha siasa kisheria.
Ni bahati mbaya sana kwamba tangu mwaka 1992, mosi, hatujaweza kujifunza kwa dhati ya mioyo yetu kabisa juu ya utamaduni wa kuishi katika mfumo wa vyama vingi; pili, hatujakubali kwa dhati kwamba mfumo huu wa vyama vingi unaondoa ukiritimba wa fikra na haki kwa kikundi cha watu kwani kila mmoja ana uhuru wake kwa mujibu wa sheria. Ni haki.
Ndiyo maana tunaweza kupuuza mazungumzo ambayo hayana gharama katika kutatua tofauti zetu za kimtazamo na kimsimamo na badala yake kudhani kwamba nguvu, mabavu na shuruti zinaweza kusaidia kujenga zaidi.
Haiyumkiniki leo miaka 32 ndani ya mfumo wa vyama vingi, bado tunashindwa kuelewa njia kuu ya kuendesha mambo katika mfumo huo ni mazungumzo. Katika mazungumzo kila mmoja anasema apendalo, lakini mwisho wa siku kinachopatikana ni kile hekima na busara na sheria zinazoongoza nchi zitaonyesha ndicho kitu cha kufuata.
Ni lazima Tanzania kama taifa lijifunze kuishi kwa sheria, kanuni na taratibu ambazo ndizo tulizokubaliana zitatuongoza katika mfumo wa vyama vingi vya siasa. Tukubaliane kwamba nchi hii ni mali ya Watanzania wote.