Tulia alipoteza fursa ya kuokolewa uhai wa Kibao

INAWEZEKANA Agosti 27 2024 ilikuwa ni siku ambayo maisha ya Ally Mohamed Kibao yangeokolewa kama Bunge lingefanya kile alichokuwa ameomba Mbunge wa Nkasi Kaskazini (Chadema), Aida Khenani kujadiliwa bungeni hali ya kutanda kwa wimbi la kutekwa, kupotea na kuuawa kwa watu nchini.

Siku hiyo Bungeni Dodoma Khenani alitumia kanuni ya 54 ya Bunge inayompa mbunge fursa ya kupendekeza jambo lolote lijadiliwe Bungeni kwa kuwasilisha hoja, yaani kwa kutoa pendekezo lililokamilika ili lipate uamuzi wa Bunge. Kwa kutumia kanuni hiyo, alisema;

“Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na matukio ya utekaji, upoteaji na mauaji yanayoendelea kwa watoto, wanaharakati, viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa na makundi mbalimbali nchini. Mheshimiwa spika kwa kuwa jambo hili limekwisha kuzungumzwa na taasisi mbalimbali ambazo zimeshafanya tathmini; Tume ya Haki za Binadamu, TLS (Chama cha Wanasheria Tanganyika) pamoja na vyama vya siasa ikiwapo Chadema. Mheshimiwa Spika kwa kuwa jambo hili lina maslahi na linawaumiza Watanzania. Na Bunge liko kwa ajili ya hawa hawa Watanzania na Mheshimiiwa Spika kulingana umuhimu huu naomba nitoe hoja wabunge wenzangu waniunge mkono Bunge hili lijadili na kutoa maelekezo kwa serikali ili angalau Watanzania wapate haki yao ya kuishi kuliko hali ya wasiwasi inaoendelea sasa.”

Spika wa Bunge la Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dk. Tulia Ackson, hakutoa fursa ya Bunge kujadili hoja hiyo kwa kile alichosema hoja ya mbunge haikukidhi mashati ya kanuni hiyo ya 54 na pia kanuni ya 55.

Hata hivyo, Dk. Tulia alisema mambo ambayo alisema Khenani ni mazito, kwamba kuuawa kwa watu na kutekwa ni mambo mazito. Alisema binafsi (Tulia) hajasikia taasisi alizotaja mbunge zimesema nini, na hata kama angekuwa amesikia anaamini serikali ina utaratibu wa kufanyia kazi masuala hayo kwa kuwa ni sehemu ya majukumu yake.  Alisisitiza kuwa hawezi kupokea hoja hiyo kwa kuwa ni masuala ya uchunguzi, ambayo yanapaswa kupatikana kutoka vyanzo mahususi vya uchunguzi.

Siku mbili baadaye, yaani Agosti 29.2024 wakati wa kipindi cha maswali ya Papo Kwa Papo kwa Waziri Mkuu, Mbunge wa Viti Maalum Anatropia Theonest, alimuuliza swali Waziri Mkuu Majaliwa Majaliwa Kassim juu ya kauli ya serikali kuhusu ongezeko kubwa la utekaji, mauaji ya watoto na watu wengine kwa kuwa matukio hayo yanahusishwa na vyombo vya dola. Kabla ya Waziri Mkuu Majaliwa kujibu swali hilo, Spika Tulia alitoa maelezo ya ziada huku akijiuliza kama swali hilo ni la kisekta au la. Alitoa ufafanuzi mrefu kwamba watu wasifikie hatua ya kunyoosheana vidole kuhusu kupotea kwa watu, kwa kuwa inajenga hisia kwamba kuna watu hawajali, wakati kila mtu anajali na kila binadamu ana haki ya kuishi.

Hatimaye alimruhusu Waziri Mkuu Majaliwa kujibu swali hilo, lakini kwa kifupi. Kwa ujumla alisema vyombo vya ulinzi na usalama vina jukumu la kupokea taarifa za uvunjifu wa amani na kuzifanyia kazi kwa kufanya uchunguzi. Alisema uchunguzi ukikamilika hatua za kisheria huchukuliwa.

Suala la kutekwa, kuteswa na kuuawa kwa watu mbalimbali, hasa wanaharakati na wanasiasa, limetikisa kwa kitambo nchini. Agosti 9, 2024 TLS walitoa taarifa yenye orodha ya zaidi ya majina ya watu 80 ambao ama wamepotea, wametekwa, kuteswa au kuuawa. Agosti 22, 2024 Chadema katika kuunga mkono taarifa ya TLS wakaja na ndugu na jamaa wa watu waliotekwa, kuteswa au na kuuawa. Walishuhudia yaliyowapata ndugu zao.

Kwa hakika ni vigumu kusema vyombo vya dola, hususan Jeshi la Polisi lilichukua hatua gani, kwanza kama Waziri Mkuu Majaliwa alivyosema, lakini pia tangu hiyo Agosti 29, 2024 siyo tu vitendo vya utekaji na mauaji vimeendelea bali pia vimefanywa kwa kiburi kikubwa.

Kwa mfano, taarifa za kutekwa na kisha kuuawa kikatili kwa aliyekuwa mjumbe wa sekretarieti ya taifa ya Chadema, Ally Mohamed Kibao, ilieleza kwamba alishushwa kwenye basi la abiria la Tashrif eneo la Tegeta jijini Dar es Salaam, jioni akiwa safarini kwenda Tanga. Walimkamata wakamfunga pingu hiyo Septemba 6, 2024 kwa mtutu wa bunduki ambazo mashuhuda wanasema ni silaha zinazofanana na zinazotumiwa na vyombo vya ulinzi na usalama vya Tanzania. Pia, katika kufanikisha utekaji huo ambao uliishia kwenye mauaji ya kinyama kabisa ya Kibao, watekaji walikuwa na magari mawili aina ya Toyota Land Cruiser, moja lilizuia basi kwa mbele na jingine kwa nyuma, kisha wakaingia kwenye basi hilo na kuondoka na Kibao katika sura inayoashiria kwamba wanakamata labda jambazi sugu au gaidi. Kumbe ni raia mwema tu wa Tanzania ambaye kwa shuhuda mbalimbali zilizotolewa juu yake alikuwa ni mtu mwema kabisa katika jamii.

Spika Tulia amenukuliwa na kurekodiwa mara kadhaa akichochea vijana kujichukulia sheria mkononi kwa mtu yeyote anayemsema vibaya Rais au mbunge kwenye jimbo lake. Alikwenda mbali zaidi kwamba hata diwani au mwenyekiti wa serikali za mitaa kwa kuwa wote ni wa CCM kama kuna mtu anawasema vibaya basi ‘vijana hao wanyooke naye.’ Hakufafanua kunyooka ni nini, lakini katika mazingira ambayo alikuwa anazungumzia kauli hizo ni dhahiri alikuwa anahamasisha vijana hao kujichukulia sheria mkononi dhidi ya mtu anayewasema vibaya Rais, Mbunge, Diwani na Mwenyekiti wa Serikali za Mitaa.

Tulia ni mwanasheria, anafahamu nini maana ya utawala wa sheria. Tulia ni mkuu wa muhimili mojawapo wa dola, Bunge. Tulia ni Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani. Ukimsikiliza ni mtu mwerevu, anajua sheria anajua kutafsiri sheria na kanuni za Bunge vizuri tu, lakini ukimsikiliza vizuri zaidi, ni kiongozi anayelikaba pumzi Bunge.

Ni jambo la bahati mbaya sasa kwamba bunge la sasa kiuhalisia ni la chama kimoja. Ni bunge lililozaliwa kwenye uchaguzi wa mwaka 2020 ambao ulijaa kila aina ya ukiukaji wa haki na taratibu za uchaguzi. Ni bunge ambalo kwa habati mbaya sana limejikuta likijitafuta kuhusu uhalali wake wa uwakilishi wa wananchi.

Bunge ni chombo cha mijadala huru, ni chombo kinachoruhusu msigano wa mawazo, ni jukwaa la kujadili mambo mazito kuhusu nchi. Ndiko mahali serikali (utawala- executive) inapata kunyooshwa, kusimamiwa, kuelekezwa na kukumbushwa wajibu wake, lakini mbele ya Spika Tulia hata ile fursa ndogo inayopatikana ili kuiweka serikali katika mstari, anaitupia kapuni. Kazi yake kubwa ni kuikingia kifua, anafurahi kuilinda serikali kuliko kuwalinda wananchi waliowapeleka bungeni.

Katika mazingira haya, yawezekana kabisa kama angelichukulia kwa uzito unaostahili hoja ya Khenani na akachungulia kanuni ya 55 (3) inayosema: Hoja zifuatazo zinaweza kutolewa bila taarifa (d) kutaka ombi lililowasilishwa Bungeni lijadiliwe. Angeliweza kutumia kifungu hicho kwa kuwa hata kwa kauli yake binafsi alikiri kwamba jambo ambalo alikuwa ameliwasilisha Khenani ‘ni jambo zito’. Lakini pamoja na kukiri uzito huo, hakuona sababu ya kutaka serikali iwekwe kwenye mstari. Pengine ndiyo maana pia hata katika kuruhusu kujibiwa kwa swali la Anatropia, bado alijenga mazingira kama ya kumwelekeza Waziri Mkuu Majaliwa njia ya kutokea.

Pengine Tulia angechukulia kwa uzito unaostahili hoja ya Khenani ya Agosti 26, 2024 ambayo yalikuja kumkuta Kibao Septemba 6, 2024 zikiwa zimepita siku 11 tu baada ya serikali kupewa njia ya kutoroka wajibu bungeni, yasingetokea. Labda, serikali ingelikuwa imezinduka baada ya wabunge kujadili hoja husika na hivyo kusaidia kukabiliana na uharamia unaoendelea nchini kwa sasa.  Katika hili ni kama Tulia alipoteza fursa ya kusaidia ukomeshaji wa mauaji haya.

spot_img

Latest articles

Rasmi Kocha Yanga afungashiwa virago usiku

Na Mwandishi Wetu Uongozi wa Klabu ya Yanga umevunja mkataba na Kocha Mkuu, Romain Folz. ...

Mwanamke ashikiliwa  Polisi kwa  kumuua mume wake na kumfukia ndani ya nyumba yao

Na Mwandishi Wetu Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita linamshikilia mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina...

Padre aliyepotea apatikana akiwa hai

Na Mwandishi Wetu Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma limefanikiwa kumpata Padre Camillus Nikata wa Jimbo...

More like this

Rasmi Kocha Yanga afungashiwa virago usiku

Na Mwandishi Wetu Uongozi wa Klabu ya Yanga umevunja mkataba na Kocha Mkuu, Romain Folz. ...

Mwanamke ashikiliwa  Polisi kwa  kumuua mume wake na kumfukia ndani ya nyumba yao

Na Mwandishi Wetu Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita linamshikilia mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina...