Upi upepo unaoweza kufika Tanzania,wa Wiliam Ruto au Paul Kagame?

KUNA upepo wa aina mbili unavuma katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mmoja ni ule uliomzidishia furaha Rais Paul Kagame ambaye katika uchaguzi mkuu uliofanyika nchini kwake Jumapili iliyopita, ameibuka na ushindi wa kimbunga wa 99% na ushei. Kagame amepata idadi ya kura nyingi kuliko alizopata katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2017 ambao aliibuka na 98.8%. Safari hii amewaachia wapinzani wake ambao pia walikuwapo katika uchaguzi wa mwaka 2017 kura chini ya asilimia moja. Hawa ni Frank Habineza aliyepata 0.53% na Philippe Mapayimana 0.32%.

Habineza mwandishi wa habari wa zamani na Mpayimana, ni kama walikuwa wanamsindikiza mgombea mmoja tu katika uchaguzi huu ambao unampa Kagame muhula wa miaka mingine saba.

Wakati Kagame akitabasamu kwa matokeo hayo ya uchaguzi unaweza kuufananisha na wa Urusi ambako Vladimir Putin Machi mwaka huu katika uchauzi naye alikuwa na ushindi wa kimbunga wa 88%. Katika mfumo wa vyama vingi nchini Tanzania, Jakaya Kikwete mwaka 2005 alipata kura zaidi 80%, ulikuwa ni ushindi mkubwa.

Upepo wa pili unaovuma katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ni ule ambao kizazi cha Z (Gen-Z) kinamuhenyesha Rais wa Kenya, William Ruto. Upepo huu kwa wiki kadhaa sasa haujamkalia vizuri kabisa Ruto. Maelfu ya vijana wanajitokeza katika miji mikubwa ya nchi hiyo wakimshinikiza kuachia madaraka. Awali walikuwa wanamtaka aache kutia saini muswada wa fedha wa mwaka 2024 ambao walisema ulikuwa ni wa kuwaongezea mzigo na kuendeleza anasa za wakubwa serikalini, huku vijana wakitaabika bila ajira na hali mbaya ya uchumi.

Kimfanano, uhuru wa Wakenya katika kupambana na kupinga kile ambacho hawakubaliani nacho, unaweza kufananishwa na demokrasia halisi ya nchi za magharibi, hasa Marekani. Ruto kwa hulka ni mtu wa mapambano, lakini tangu vijana waanze kungia mtaani, amekuwa ni kiongozi tofauti sana na wa hapo kabla. Amekataa kusaini muswada wa fedha wa mwaka 2024, amevunja baraza la mawaziri, amemfuta kazi Mwanasheria Mkuu wa Serikali, amekubali kuachia ngazi kwa Inspeka Jenerali wa Polisi, amefuta mambo mengi ambayo alikuwa amepanga kufanywa na serikali yake, ikiwamo kufuta hata bajeti ya ofisi ya mkewe.

Ni kama Ruto amelainika. Pamoja na kulainika, vijana bado wanamng’ang’ania kooni. Wanataka kumng’oa!

Wanyarwanda wanaonyesha ‘wana imani’ na Kagame. Kagame amekuwa madarakani kwa kitambo sasa. Alianza kuonja madaraka kufuatia mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, ambayo yalihitimisha utawala wa Juvénal Habyarimana
Aliyeingia madarakani tangu Julai 1973 na kuishia 1994 baada ya kufa katika ajali ya ndege akiwa na mwenzake wa Burundi Cyprien Ntaryamira, ndege yao ilipotunguliwa wakitokea Dar es Salaam katika mazungumzo ya amani.

Ukiangalia utii na ukimya wa raia wa Rwanda, ukatazama matokeo ya uchaguzi wa sasa na kile kinachoendelea nchini Kenya, ni vigumu kusema kwamba nchi hizi zipo katika jumuiko moja la Afrika Mashariki. Lakini, pia ukipiga hatua moja mbele na kutafakari kuhusu Tanzania, unaweza kudhani labda, tunafanana na Rwanda. Nchi ya kutii mamlaka kwa gharama zozote. Ukifikiri zaidi, unaweza kudhani kwamba wale Gen-Z wa Kenya labda wameazimwa kwingineko, siyo raia wa Afrika Mashariki. Unaweza kuwaza vitu vingi sana. Ila mwisho wa siku, unapata ukinzani wa akili kwamba ni kwa kiwango gani nchi za Afrika kama ilivyo Rwanda na hata Tanzania, chaguzi zake kweli zinaakisi utashi wa umma?

Kwa mfano, ni kwa nini nchi nyingi za Afrika watawala wake wanang’ang’ana kuwa na mikono yao kwenye tume za uchaguzi? Ni kwa nini hazitaki tume huru wa uchaguzi? Ni kwa nini hazitaki katiba ambazo zinawawajibisha isipokuwa ambazo zinatoa nguvu kubwa ya madaraka kwa watawala kuamua watakavyo?

Mwaka 1989 dunia ilishuhudia ushindi wa kimbunga wa aliyekuwa Rais wa Romani, Nicolae Ceaușescu. Ushindi wake ulikuwa kama huu wa sasa wa Kagame, lakini miezi michache tu baada ya ushindi huo, alikutana na kile kinachofanana na Gen-Z ya Kenya ya sasa. Ulikuwa ni mwisho wa utawala wake wa kuanzia mwaka 1967.

Hakuna kitu cha maana kama ukweli. Ni kwa kiwango gani kwa mfano, watu wanaotafuta madaraka ya dola wana uhakika kwamba ushindi wanoupata ni wa kweli na halali katika mazingira sawa, huru ya ushindani usiokuwa na hila? Ni kwa nini kujilisha upepo na kusadiki kwamba kiongozi ana ridhaa ya kuongoza nchi wakati kimsingi anajua fika kwamba amebebwa na vyombo vya ulinzi na usalama?

Nakumbuka kuna uchaguzi mmoja nchini Zimbabwe, mkuu wa majeshi akijitokeza na kusema kwamba jeshi halikuwa tayari kumpigia saluti rais ambaye siyo Robert Mugabe, rais wa zamani wa Zimbabwe. Katika mazingira kama hayo, mtu anajiuliza kama nia ni kutaka kiongozi fulani ashinde tu yeye, kuna haja gani kwa mfano wa kufanya uchaguzi na kupoteza rasilimali nyingi kiasi hicho- fedha na muda wa watu? Kwa nini tu nchi nyingi za Afrika zisiseme turejee katika mifumo ya zamani ya uchifu?

Ingawa ushindi wa Kagame siyo somo la maana sana kwa Tanzania katika kuendesha siasa za vyama vingi, labda sisi kama taifa tunapaswa kujiuliza, hivi upepo unaovuma Kenya kwa sasa unaweza kuvamia Tanzania? Je, tuna mazingira yanayoshabihiana na Kenya ambayo yanaweza kustawisha kuvuma kwa kasi kwa upepo kama wa Kenya?

Ingawa sina majibu ya moja kwa moja, niseme tu, Ruto kabla ya Gen-Z kuingia barabarani, aliamini amedhibiti kila kitu katika nchi yake. Alikuwa na Bunge, Polisi, Jeshi na baraza lake la mawaziri, pia aliamini kwamba ni mjuzi sana wa siasa kwa sababu tu alishinda urais akiwa anapingwa na rais aliyekuwa anamaliza muda wake ambaye aliamua kumuunga mkono Raila Odinga.

Lakini, kitu ambacho Ruto alisahau, ni kwamba wananchi wa nchi yoyote, wanakawaida ya kuchoshwa na wizi wa mali ya umma, wanachoshwa na serikali zinazojiendesha kwa anasa kwa jasho la walipa kodi, wanachoshwa na mateso yasiyoisha ya hali ngumu ya maisha na wimbi la kukoseka kabisa kwa uhakika wa mkate kwa kila mwananchi. Hali inakuwa mbaya zaidi kama kundi kubwa la wananchi, hasa vijana, linazidi kutupwa kando kwenye meza ya kunufaika na keki ya taifa lao. Kama hakuna ajira hakuna tumaini lolote.

Ni wajibu wa viongozi wa Tanzania kujiuliza, hivi sababu za Gen-Z wa Kenya kuingia mitaani zinaonekana kwetu? Kuna dalili au mfanano wowote wa uendeshaji wa serikali ya Tazania na ile ya Ruto ambayo sasa inampa wakati mgumu kujua afanye nini kupata tena imani ya watu wake. Katika uchaguzi wa mwaka juzi, Ruto alipata kura milioni 7.17 sawa na asilimia 50.49, wakati mpinzani wake, Raila alipata kura milioni 6.9 sawa na asilimia 48.85. Ingawa unaweza kueleza kwamba ushindi huo ulikuwa ni mwembamba, kwa mwendo aliokuwa anakwenda nao na ahadi alizokuwa amewapa Wakenya, ni dhahiri isingekuwa rahisi mtu kubashiri leo kwamba ambao wangekuja kumpa shida kiongozi huyo siyo mpinzani wake wa kisiasa, Raila, bali ahadi zake mwenyewe alizozivakisha jina la ‘serikaki ya mahustler’. Je, sisi tuna ahadi ambazo zimeshindwa kutimizwa? Vipi bomu la ajira kwa vijana?

www.themediabrains.com

spot_img

Latest articles

Bei ya Petroli, dizeli zapanda

Na Mwandishi Wetu, Dodoma  MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji – EWURA,...

WHO yatangaza tarehe ya uchaguzi wa kupatikana mrithi wa Ndugulile

Na Mwandishi Wetu SHIRIKA la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa Mkurugenzi mpya wa Kanda...

Wajiteka na kudai pesa kutoka kwa wazazi wao

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam JESHI la Polisi Kanda Maalum Dar es salaam limefanikiwa...

Machifu watano watekwa Nyara Kenya na Al-Shabaab

MACHIFU watano wametekwa nyara siku ya Jumatatu na watu wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wa al-Shabaab...

More like this

Bei ya Petroli, dizeli zapanda

Na Mwandishi Wetu, Dodoma  MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji – EWURA,...

WHO yatangaza tarehe ya uchaguzi wa kupatikana mrithi wa Ndugulile

Na Mwandishi Wetu SHIRIKA la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa Mkurugenzi mpya wa Kanda...

Wajiteka na kudai pesa kutoka kwa wazazi wao

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam JESHI la Polisi Kanda Maalum Dar es salaam limefanikiwa...