Dimwa kashiba, lazima achafue hali ya hewa

themediabrains.com

KUNA mtu kachafua hali ya hewa huko Zanzibar. Huyu si mwingine bali Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Mohamed Said Dimwa, ambaye alisema kwamba wajumbe wa sekretarieti ya Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu Zanzibar, wamepitisha pendekezo la kuishauri Kamati Maalum ya NEC Zanzibar kuridhia kuongeza muda wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi wa kuongoza nchi kutoka miaka mitano hadi saba. Sababu kubwa inayosimika pendekezo hilo ni utendaji wa Rais Mwinyi tangu angie madarakani mwaka 2020 kwa kuwa amefanya mengi na kuingia katika uchaguzi mwakani ni sawa na kupoteza fedha bure.

Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Mohamed Said Dimwa.

“Wajumbe wa Sektetarieti tumejadili na kutathimini kwa kina juu ya utendaji wa Rais Dk. Mwinyi, tukajiridhisha kuwa hakuna mbadala wake na anastahiki aongoze nchi kwa kipindi cha miaka saba ili apate muda mzuri wa kufanya mapinduzi ya kimaendeleo katika nyanja za kiuchumi na kijamii. Maamuzi yetu yatafuata taratibu za kikatiba na kikanuni kwa kuyawasilisha katika vikao vya ngazi za juu ili vitoe baraka zake, ili hoja hii ikapitishwe katika Baraza la Wawakilishi Zanzibar. Ili yaendelee kufanyika mabadiliko ya baadhi ya vipengele vya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kwa lengo la kuhakikisha tunafanya Uchaguzi Mkuu wa dola kwa kila baada ya miaka saba,” aliwaambia vijana wa CCM wakati akifunga Mkutano wa Baraza Kuu la UVCCM Wilaya ya chama Dimami Zanzibar uliofanyika katika Ofisi za Wilaya hiyo Kiembesamaki.

Hata kabla ya kauli hiyo kupoa, baada ya kutolewa Jumapili ya Juni 23, 2024, tayari imekumbana na upinzani mkali. Ndani ya CCM kwenyewe, na hata ndani ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia idara ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, mapema wiki hii ilijitenga na mapendekeo hayo na kusisitiza kwamba Rais Dk. Hussein Mwinyi ni muumini wa kufuata katiba, sheria na taratibu za uchaguzi wa kila baada ya miaka mitano. Aidha, ametaka mjadala huo ufungwe. Kauli hiyo imo kwenye taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na ikulu ya Zanzibar.

Katika kupigilia msumari wa upinzani, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amosi Makalla naye akihojiwa na moja ya vituo vya luninga nchini amesema jambo hilo halipo. Pia amesisitiza kuwa hakuna kikao chochote cha chama kilichokaa kupokea au kujadili wazo hilo. “Kwa kifupi ni kwamba jambo hilo halipo.”

Kauli ya Dimwa anayejiita daktari, siyo jambo jipya katika siasa za Tanzania. Mwaka 2000 wakati aliyekuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Salmin Amour akifikia ukingoni mwa utawala, kulikuwa na juhudi zinazofanana na hizi. Zilenge kubadili katiba ili kumwezesha Salmin awanie kipindi cha tatu cha utawala huko Zanzibar. Hoja ya kutaka katiba ibadilishwe, iliwasilishwa katika Baraza la Wawakilishi na aliyekuwa Waziri wa Fedha, Mohamed Ramia Abdiwawa. Kwa bahati njema, hoja za wapambe wa Salmin waliokuwa wamepambana kufa kupona kuona kuwa kiongozi huyo almaarufu kama Komandoo anawania tena urais Zanzibar, haikuungwa mkono ndani ya CCM.

Wapo wabunge wa CCM walijiorodhesha na kupinga pendelezo lolote la kutaka kubadili katiba ya Zanzibar, ili kufanikisha njama za kumsaidia Salmin kusalia madarani na kuiwasislishwa kwenye chama chao. Hoja ya wapambe wa Salmin ilikuwa nyepesi tu kama ilivyo ya sasa, kwamba Komandoo alikuwa ndiye mtu pekee ambaye angeliweza kupambana na Maalim Seif Sharif Hamad ambaye alikuwa anawania nafasi hiyo kwa mara ya pili kupitia Chama cha Wananchi (CUF). Wapambe wa Komandoo walikwama na hali ilipokuwa imekuwa tete sana katika vikao vya CCM huko Dodoma, duru zilitaarifu kwamba Salmin aliwaruka wapambe wake akisisitiza kwamba hakuna kokote alikowahi kusema kwamba angewania tena urais wa Zanzibar mwaka 2000.

Juhudi hizi za kutamani na kusadiki kwamba kiongozi fulani ni lazima asalie madarakani kwa hali yoyote ili kwa kuwa eti, ndiye pekee anaweza kufanya mambo au jambo fulani, pia zilipata kuibuka kwa upande wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2020. Kauli ya ‘atake asitake’ ni rejeo muhimu katika muktadha huu.

Kauli iliyoibuliwa na aliyekuwa mbunge wa Nkasi (CCM), Ally Kessy kwamba Rais John Magufuli alazimishwe kuwania urais zaidi ya awamu mbili. Na kwa msisitizo akataka katiba ibadilishwe ili kumpa fursa hiyo, siyo tu ilionyesha mpango kabambe wa upambe wa kutaka kumfanya Rais Magufuli awe kiongozi wa kudumu, bali pia ilishitua wengi Spika wa Bunge wakati huo, Job Ndugai, alipomuomba Kessy aweke hoja yake kiporo. Kwamba waende kwanza kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, wakirejea bungeni, Magufuli ‘atake asitake’ watamfanya asalie madarakani. Kessy hakurejea bungeni, na Machi 2021 Mungu aliamua yake kuhusu Magufuli, na hata sasa Ndugai siyo spika tena. Hoja ikafa, ikaoza na kuzikwa.

Ni katika dhana hii ya kukataa au kupuuza kujenga taasisi imara za kuendesha nchi, ndiyo inasababisha kuibuka kwa tabia ya kujipendekeza kwa viongozi kiasi cha kujipachika majina ya ovyo kama ‘chawa’.

Jesse Kwayu.

Pengine ni kwa nini hoja hizi zimekuwa zikijirejewa mara kwa mara. Mwaka 2000, mwaka 2020 na sasa 2024? Chimbuko la hoja hizi ni taifa kushindwa kujenga taasisi za utawala. Badala yake, tunapenda sana kuendesha nchi kwa kumuangalia mtu. Kiongozi fulani. Bado hatujawa na mfumo wa kujenga taasisi za kuendesha nchi. Kila kitu kinaegemezwa kwenye utashi wa mtu mmoja, aghalab, mkuu wa dola.

Ukiwasikiliza viongozi wetu, mawaziri, wakuu wa taasisi za serikali zinazojitegemea, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri na kila mwenye mamlaka katika nchini hii, hakosi kufanya rejea kwa kiongozi mkuu wa dola kwa kila kitu.

Waziri wa Fedha akiwasilisha bajati ya serikali bungeni anasema ni ya kiongozi mkuu wa dola, ikijengwa barabara au daraja au reli au hospitali ikijengwa kwa ujumla kila fedha zikitolewa kwa ajili ya jambo lolote inatajwa kwamba ni fedha za mkuu wa dola.

Kwa bahati mbaya zaidi, hata wabunge ambao wana wajibu wa kuisimamia serikali, wakiunda muhimili mmoja wada unaowakilisha wananchi, nao wamejisalimisha katika dhana potofu ya kusadiki kila kitu ni cha mkuu wa dola. Ukiwasikiliza wabunge wakijenga hoja, unapata picha kama vila nchi yetu sasa ni ya kifalme. Kwamba wengine wote waliobaki ni watwana au vijakazi wa mkuu wa dola. Tunatamani uimla kama siyo udikteta!

Ni katika dhana hii ya kukataa au kupuuza kujenga taasisi imara za kuendesha nchi, ndiyo inasababisha kuibuka kwa tabia ya kujipendekeza kwa viongozi kiasi cha kujipachika majina ya ovyo kama ‘chawa’. Katika mfumo wa utawala wa namna hii, inakuwa ni vigumu kuwaza nje ya kiongozi aliyeko madarakani. Mfumo huu wa kukataa au kukwepa kujenga taasisi imara, ndiyo sababu kubwa ya wale walio karibu na kiongozi mkuu kutumia kila karata ili hali iliyoko iendelee kama ilivyo kwa kuwa inakuwa na manufaa binafsi kwao.

Mtu anaweza kujiuliza maswali magumu kwamba ‘chawa’ na wapambe wa kutaka usultani katika ofisi kuu za dola, wanapata wapi ujasiri huo, ilihali taifa letu kwa sasa lina mambo makubwa na mazito yanayohiataji muda wao na tafakari ya kina. Kwa mfano, katika changamoto kubwa ya ukosefu wa ajira kwa mamilioni ya vijana wanaotoka shuleni na vyuoni mwaka baada ya mwaka; hali ngumu ya maisha – bei ya bidhaa na huduma kuzidi kupaa mwezi baada ya mwezi na kila ya aina ya shinikizo ya maisha ya watu wetu, uchawa unasaidia vipi kutatua haya?

Ni vema ikaeleweka kwamba akina Mohamed Said Dimwa hakuna jambo jipya wanaleta leo lenye manufaa ya watu wetu, mbali ya kulinda na kutetea kibaba chao. Ni kauli kama zile za Mohamed Ramia Abdiwawa zama za Komandoo, ni kama ‘chokochoko’ ya kina Ally Kessy na Job Ndugai za ‘atake asitake’. Hakika mbinu hizi za ovyo za kulinda vibaba vya watu hazitafutika katika taifa hili kama tutaendelea na mfumo wa kujenga watu badala ya taasisi imara za kuendesha nchi.

spot_img

Latest articles

Hivi vikosi kazi vimerejea kwa mlango wa nyuma?

KUNA kila dalili kwamba taifa letu kidogokidogo linakumbwa na hali ya kutokuaminiana. Hali hii...

Chondechonde Polisi msisababishe wananchi wakate tamaa

ALHAMISI iliyopita yaani Desemba 5, mwaka huu wa 2024 lilitokea tukio baya la kuhuzunisha...

Ufaransa yaipatia Tanzania Sh bilioni 323.4

Na Mwandishi Wetu Serikali ya Tanzania na Shirika la Maendeleo La Ufaransa (AFD) wamesaini mikataba...

TANZANIA YAWEKA REKODI MKUTANO WA WAHASIBU WAKUU AFRIKA

Na Mwandishi Wetu Tanzania imeweka rekodi ya Mkutano wa Pili wa Wahasibu Wakuu wa Serikali...

More like this

Hivi vikosi kazi vimerejea kwa mlango wa nyuma?

KUNA kila dalili kwamba taifa letu kidogokidogo linakumbwa na hali ya kutokuaminiana. Hali hii...

Chondechonde Polisi msisababishe wananchi wakate tamaa

ALHAMISI iliyopita yaani Desemba 5, mwaka huu wa 2024 lilitokea tukio baya la kuhuzunisha...

Ufaransa yaipatia Tanzania Sh bilioni 323.4

Na Mwandishi Wetu Serikali ya Tanzania na Shirika la Maendeleo La Ufaransa (AFD) wamesaini mikataba...