WATALII HIFADHI ZA TAIFA WAFIKIA MILIONI 1.5

Na Tatu Mohamed 

IDADI ya watalii waliotembelea hifadhi za taifa nchini imeongezeka kutoka watalii 768,319 mwaka 2021/2022 hadi watalii 1,559,641 mwaka 2025/2026, ikiwa ni ongezeko la zaidi ya mara mbili ndani ya kipindi cha miaka mitano.

Ongezeko hilo ni miongoni mwa mafanikio yaliyobainishwa na Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Massina Mwishawa, wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari na waandishi wa habari katika kikao kazi kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Amesema mafanikio hayo yanatokana na mikakati mbalimbali inayotekelezwa na shirika hilo katika kuboresha huduma za utalii, kuongeza vivutio, kuimarisha miundombinu na kutumia teknolojia za kisasa katika shughuli za uhifadhi.

Takwimu zilizowasilishwa zinaonesha kuwa idadi ya watalii imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka, kutoka 768,319 mwaka 2021/2022 hadi 1,163,793 mwaka 2022/2023, kisha 1,280,145 mwaka 2023/2024 na kufikia 1,493,137 mwaka 2024/2025 kabla ya kufikia 1,559,641 mwaka 2025/2026.

“Hatua hii inaonesha ukuaji wa sekta ya utalii na umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika miundombinu na huduma zinazowezesha hifadhi za taifa kupokea wageni wengi zaidi,” amesema.

Ameongeza kuwa, katika eneo la uwekezaji wa malazi, TANAPA imeongeza uwezo wa vitanda vya malazi kutoka vitanda 5,755 mwaka 2021 hadi vitanda 12,014 mwaka 2025, hatua inayolenga kukidhi mahitaji ya watalii wanaotembelea hifadhi mbalimbali nchini.

Amesema uwekezaji huo umehusisha ujenzi na uboreshaji wa malazi katika maeneo mbalimbali, yakiwemo Loji, kambi za kudumu, kambi za muda na hosteli.

Aidha, amefafanua kuwa shirika hilo linaendelea kuimarisha usafiri na huduma za wageni kwa kukamilisha mpango wa kuingiza magari katika hifadhi sita, zikiwemo Tarangire kupitia Mamire, Ibanda-Kyerwa kupitia Kifurusa, Serengeti kupitia Machochwe, Nyerere kupitia Mtemere na Mikumi kupitia Kikwaraza na Doma.

“Katika kuhakikisha utalii unaendelea kukua, TANAPA imeweka mkakati wa miaka mitano unaolenga kuongeza idadi ya watalii na mapato kupitia uanzishaji wa aina mpya za utalii na kuboresha vivutio vilivyopo.

“Miongoni mwa mipango hiyo ni kuanzisha utalii wa farasi, utalii wa spot fishing, utalii wa anga na utalii wa kutazama mandhari kwa ndege maalumu (scenic flights), sambamba na kuimarisha utalii wa kitalii katika hifadhi za Serengeti, Ruaha, Mikumi, Nyerere na nyinginezo,” amesema.

Katika eneo la uhifadhi, amesema TANAPA pia imeweka mkazo katika matumizi ya teknolojia za kisasa, ikiwemo ndege zisizo na rubani (drones), mifumo ya GPS na vifaa vya mawasiliano ya satelaiti ili kuboresha doria, ufuatiliaji wa wanyamapori na kudhibiti vitendo vya ujangili.

“Pia tumepanga kuimarisha miundombinu ya barabara kwa kujenga barabara yenye urefu wa kilomita 6.69 kwa kiwango cha lami kutoka lango kuu la hifadhi hadi eneo la ndani ya hifadhi, hatua inayolenga kurahisisha usafiri na shughuli za uhifadhi,” amesema. 

Katika kuimarisha uhusiano kati ya hifadhi na jamii zinazozunguka maeneo hayo, amesema TANAPA imeendelea kutekeleza miradi ya maendeleo inayolenga kupunguza migogoro kati ya binadamu na wanyamapori.

“Tumejenga vituo sita vya askari kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za mwingiliano kati ya binadamu na wanyamapori, nyumba mbili za walinzi, zahanati tatu, nyumba ya mwalimu mmoja na bweni la wasichana katika shule ya sekondari.

“Pia, tumejenga madarasa mawili na kusambaza mizinga ya nyuki 2,590, huku likitoa mafunzo kwa askari wa vijiji wanaojitolea (VGS) 410 katika vijiji 40 vinavyozunguka Hifadhi za Taifa za Ruaha, Mikumi, Nyerere na Udzungwa,” amesema.

Amefafanua kuwa, hatua hizo zina lengo la kuwashirikisha wananchi katika shughuli za uhifadhi na kuwapatia fursa za kunufaika na uwepo wa hifadhi hizo.

Kwa upande mwingine, amesema TANAPA imeendelea kutumia michezo kama nyenzo ya kutangaza utalii wa Tanzania kupitia mashindano mbalimbali yanayofanyika ndani na karibu na hifadhi.

Ametaja mashindano hayo ni pamoja na Great Ruaha Marathon na Serengeti Marathon, ambayo yanalenga kuunganisha michezo na utalii pamoja na kuitangaza Tanzania kwa wageni kutoka ndani na nje ya nchi.

Katika matumizi ya teknolojia ya mawasiliano, amesema shirika hilo limeendelea kutumia majukwaa ya kidijitali kutangaza vivutio vyake. Miongoni mwa hatua hizo ni kuanzisha na kuendeleza maudhui ya podcast yanayohusu uhifadhi na utalii, ambayo kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa yamefikia zaidi ya watu milioni 120 katika mwaka 2025/2026.

Ameeleza kuwa, TANAPA imeweka mkakati wa kuendeleza utalii wa majini katika Ziwa Victoria kwa kuunganisha vivutio vya Hifadhi za Taifa Serengeti kupitia Ghuba ya Speke, Kisiwa cha Saanane, Kisiwa cha Rubondo na eneo la Bugiri-Chato.

Hata hivyo, Kamishna Mwishawa amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wadau wa habari, wawekezaji na jamii katika kuitangaza sekta ya utalii na kulinda urithi wa asili wa Tanzania kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Mwisho

spot_img

Latest articles

OTR na TAZAMA zajadili mwelekeo wa biashara

Na Mwandishi Wetu OFISI ya Msajili wa Hazina (OTR) na Kampuni ya Bomba la Mafuta...

MATENGENEZO YA BOMBA MPIJI YAKAMILIKA, DAWASA YAINGIA MTAANI

Na Mwandishi Wetu HUDUMA ya maji imeanza kurejea katika maeneo mbalimbali ya Dar es...

PIC yaitaka Benki ya Kilimo kupanua uwezo wa kuwafikia wakulima

Na Mwandishi Wetu KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma...

TANESCO YAJENGA NJIA MBADALA YA UMEME KUPUNGUZA CHANGAMOTO YA UMEME MBAGALA, KIGAMBONI, MKURANGA NA KIBITI

📌Ni katika kuboresha hali ya upatikanaji umeme kwenye maeneo yaliyoathirika 📌MD Twange awashukuru wateja...

More like this

OTR na TAZAMA zajadili mwelekeo wa biashara

Na Mwandishi Wetu OFISI ya Msajili wa Hazina (OTR) na Kampuni ya Bomba la Mafuta...

MATENGENEZO YA BOMBA MPIJI YAKAMILIKA, DAWASA YAINGIA MTAANI

Na Mwandishi Wetu HUDUMA ya maji imeanza kurejea katika maeneo mbalimbali ya Dar es...

PIC yaitaka Benki ya Kilimo kupanua uwezo wa kuwafikia wakulima

Na Mwandishi Wetu KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma...