Na Mwandishi Wetu
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, amesema Tanzania inahitaji rasilimali watu wenye afya bora, vijana wanaopata fursa na sekta binafsi inayowajibika ili kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Mhe. Hemed alisema hayo kwa niaba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, wakati wa Tamasha la Mbio za Hisani za CRDB Bank International Marathon lililofanyika katika Viwanja vya Posta Kijitonyama, Dar es Salaam.

Alisema tamasha hilo limekuwa na mchango mkubwa katika kuboresha afya za Watanzania kupitia kusaidia wananchi wenye uhitaji kupata huduma za matibabu, ambapo zaidi ya watoto 1,000 wamepatiwa matibabu ya moyo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), huku zaidi ya wanawake 450 wenye ujauzito hatarishi wakipatiwa huduma katika Hospitali ya CCBRT.
Kwa mujibu wa Mhe. Hemed, hatua hiyo imechangia kuokoa maisha ya wananchi ambao wangekabiliwa na madhara makubwa kutokana na changamoto za kiafya.

Alisema CRDB Bank International Marathon inaendelea kuunga mkono vipaumbele vya Serikali katika sekta ya afya kwa mwaka 2025/2026, hususan katika kuimarisha huduma za kinga, afya ya uzazi pamoja na huduma kwa mama na mtoto, hatua inayolenga kuchangia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.
Aidha, alisema sekta ya michezo ni muhimu katika kukuza uchumi, kuzalisha ajira, kuimarisha utalii na kuvutia uwekezaji, huku mashindano ya kimataifa yakitoa fursa ya kuitangaza Tanzania na kuongeza manufaa ya kiuchumi na kijamii.
Aliwataka wananchi kuendelea kuunga mkono juhudi za wadau mbalimbali zinazolenga kuboresha maisha ya watu wenye uhitaji na kuongeza ustawi wa jamii.

Sambamba na hilo, Mhe. Hemed aliipongeza CRDB Bank Foundation kwa kuwekeza katika maeneo yanayoendana na vipaumbele vya Serikali, akisema hatua hiyo ni mfano wa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
Pia aliwataka vijana na wanamichezo kuwa mabalozi wa amani na utulivu nchini, akisisitiza kuwa maendeleo hayawezi kupatikana bila kuwepo kwa amani.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya CRDB Bank Foundation, CPA Oswald Urassa, alisema Benki ya CRDB imejikita katika kutoa miongozo ya kisera kwa Menejimenti ili kuhakikisha taasisi hiyo inawafikia walengwa kupitia programu mbalimbali ambazo tayari zimenufaisha maelfu ya Watanzania.
CPA Urassa alisema CRDB ina mkakati wa kuwa kinara katika utoaji wa huduma za kifedha katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, huku ikiendelea kuimarisha mahusiano na nchi jirani kwa lengo la kupanua huduma, kukuza uchumi na kuimarisha huduma za kifedha.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank, Dkt. Abdulmajid Nsekela, alisema lengo la CRDB Bank International Marathon ni kubadili maisha ya Watanzania wanaokabiliwa na magonjwa mbalimbali, yakiwemo magonjwa ya moyo, saratani pamoja na changamoto za kiafya kwa wanawake wajawazito na watoto walio katika mazingira hatarishi.
Dkt. Nsekela alisema CRDB imejipanga kuendelea kutoa huduma kubwa zaidi kwa jamii, hususan vijana, wanawake na watoto, kwa kutambua kuwa uchumi imara hujengwa na watu wenye afya bora.
Alisema kupitia CRDB Bank International Marathon, watoto zaidi ya 400 tayari wamesaidiwa kupata huduma za upasuaji wa moyo, huku wanawake wenye ujauzito hatarishi wakisaidiwa kupata huduma na kujifungua salama.
Aliongeza kuwa CRDB itaendelea kupanua programu hiyo ili kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa kuwapatia fursa, elimu na kuwawezesha kutimiza malengo yao.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule, aliwataka vijana kutumia fursa zinazotolewa na CRDB Bank, akisema benki hiyo imeendelea kuwekeza katika kuwawezesha vijana, wanawake na jamii kwa ujumla kupitia mitaji, ubunifu na uwekezaji.
Mtambule pia aliwataka vijana kuwa mabalozi wa amani, uzalendo na mshikamano wa kitaifa ili kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa nchi salama kwa ajili ya maendeleo na uwekezaji.


