Vijana 3,967 waomba uwezeshaji kupitia Go Green na IMBEJU ya CRDB Bank Foundation

Na Mwandishi wetu

JUMLA ya vijana 3,967 kutoka maeneo mbalimbali nchini wamewasilisha maombi ya kupata uwezeshaji kupitia programu ya Go Green na IMBEJU inayotekelezwa na CRDB Bank Foundation, ikiwa ni ndani ya siku 30 tangu kufunguliwa kwa dirisha la maombi.

Programu hiyo ilizinduliwa Februari 12, 2026, ikiwa na lengo la kuhamasisha na kusaidia miradi ya vijana inayolenga kulinda mazingira na kukuza uchumi wa kijani.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 17, 2026 baada ya kufungwa kwa dirisha la maombi, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, TullyEsther Mwambapa, amesema hatua inayofuata ni tathmini ya kiufundi ya maombi hayo.

Ameeleza kuwa tathmini hiyo itafanywa na jopo la wataalamu kutoka taasisi mbalimbali ikiwemo CRDB Bank, COSTECH, ICTC pamoja na Wizara ya Maendeleo ya Vijana na Ofisi ya Makamu wa Rais inayosimamia mazingira.

Kwa mujibu wa TullyEster, tathmini hiyo itazingatia ubunifu wa wazo la biashara, uendelevu wake, uwezo wa kujitegemea pamoja na mchango wake katika uhifadhi wa mazingira, huku mchakato huo ukitarajiwa kukamilika ndani ya wiki moja.

“Tumepokea maombi kutoka sehemu mbalimbali nchini, jambo linaloonyesha kuwa dhana ya uchumi wa kijani inaeleweka na kukubalika kwa kasi miongoni mwa vijana. Kupitia programu hii, tunalenga kuchochea biashara bunifu zinazotatua changamoto za mazingira huku zikizalisha ajira na kukuza uchumi,” amesema TullyEster.

Ameongeza kuwa waombaji watakaofanikiwa kupita hatua ya awali ya mchujo watapatiwa mitaji kati ya Sh500,000 hadi Sh500 milioni kulingana na mahitaji na ukubwa wa miradi yao.

Amefafanua kuwa, Programu ya Go Green na IMBEJU inalenga kuwawezesha vijana wajasiriamali, wamiliki wa kampuni changa, wafanyabiashara wadogo, pamoja na wanafunzi wa vyuo vikuu wenye mawazo ya biashara yanayoweza kutekelezwa.

“Maeneo yanayopewa kipaumbele ni pamoja na kilimo kinachohimili mabadiliko ya tabianchi, uvuvi endelevu, matumizi ya nishati safi na jadidifu, teknolojia za maji na umwagiliaji, usimamizi wa taka, pamoja na ubunifu wa kidijitali unaolenga kulinda mazingira,” amesema.

Ameongeza kuwa, Takwimu za awali zinaonyesha kuwa asilimia 58 ya waombaji ni wanaume huku asilimia 42 wakiwa wanawake.”Maombi mengi yametoka Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Iringa, Morogoro, Arusha, Zanzibar, Pwani, Mara na Kilimanjaro,” amesema.

Amebainisha kuwa, baada ya mchujo wa awali, waombaji watakaofanikiwa wataitwa Dar es Salaam kwa ajili ya mafunzo maalum yatakayolenga kuboresha biashara zao pamoja na kuwaunganisha na wawekezaji, akiwemo Warioba Ventures.

Amesema hatua nyingine itahusisha uhakiki wa miradi kwa kutembelea biashara husika ili kuthibitisha uhalisia wake kabla ya kutangaza majina ya washindi watakaopata mitaji.

Kwa upande wa wanafunzi wa vyuo vikuu, amesema mawazo ya biashara yatakayochaguliwa yatapatiwa kati ya Sh500,000 hadi Sh10 milioni ili kusaidia kuyatekeleza na kutoa mchango katika kutatua changamoto za kijamii.

Programu ya Go Green na IMBEJU inatekelezwa kwa ushirikiano kati ya CRDB Bank Foundation na CRDB Bank kupitia programming ya Tanzania Agriculture Climate Adaptation Development Program (TACATDP), kwa ufadhili wa Green Climate Fund pamoja na FursaHub.

Programu hiyo ilizinduliwa rasmi Dodoma na Waziri wa Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, ambaye pia anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya kukabidhi mitaji kwa washindi.

spot_img

Latest articles

RC Kunenge aipongeza Dawasa, awapa jukumu madiwani

Na Mwandishi wetu MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amesema ushirikishwaji wananchi kwenye...

Serikali yatoa maelekezo nane kuimarisha kampuni ambazo ina umiliki hisa chache kuelekea Dira 2050

Na Mwandishi wetu, Arusha SERIKALI imetoa maelekezo nane ya kimkakati yanayolenga kuimarisha utendaji wa kampuni...

Uwekezaji wa Shilingi Bilioni 50 Kituo Cha Mpomvu waimarisha upatikanaji wa umeme Kanda ya Ziwa

📌 Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini yakagua Kituo cha Kupokea...

Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini yaipongeza Tanesco utekelezaji wa Mradi wa Umeme Jua Kishapu

📌 Watembelea mradi kuona ufanisi wake 📌 Shilingi bilioni 118 zatumika kutekeleza mradi 📌 Watoa rai...

More like this

RC Kunenge aipongeza Dawasa, awapa jukumu madiwani

Na Mwandishi wetu MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amesema ushirikishwaji wananchi kwenye...

Serikali yatoa maelekezo nane kuimarisha kampuni ambazo ina umiliki hisa chache kuelekea Dira 2050

Na Mwandishi wetu, Arusha SERIKALI imetoa maelekezo nane ya kimkakati yanayolenga kuimarisha utendaji wa kampuni...

Uwekezaji wa Shilingi Bilioni 50 Kituo Cha Mpomvu waimarisha upatikanaji wa umeme Kanda ya Ziwa

📌 Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini yakagua Kituo cha Kupokea...