Na Mwandishi wetu
BENKI ya CRDB imezindua kampeni yake mpya ya ‘Fainali ndio Mpango na TEMBOCARD VISA’, hatua inayolenga kuhamasisha matumizi ya malipo yasiyotumia fedha taslimu, kuongeza ubunifu katika huduma za kifedha, na kutoa zawadi kwa wateja wake.
Kampeni hii ni fursa ya kipekee kwa wateja wa Tembocard Visa, Tembo Prepaid, Tembo Credit, na Infinity Premier kushiriki katika droo za kushinda safari za kushuhudia fainali za Kombe la Dunia na vifaa vya kielektroniki kama Smart TV, hatua inayounganisha uchumi wa kifedha na burudani ya michezo.
Akizungumza kwenye uzinduzi leo Machi 13, 2026 jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Wateja Wadogo na wa Kati, Bonaventure Paul amesema kuwa kampeni hiyo inalenga kuhakikisha wateja wanapata urahisi wa kutumia kadi zao, kushiriki shughuli za kifedha kwa usalama, na kufurahia msisimko wa kimataifa wa michezo, huku ikichangia kukuza matumizi ya kidijitali nchini.

Kwa upande wake, Mkuu wa kitengo cha biashara za Kadi, Farid Seif amebainisha kuwa Washindi watapatikana kupitia droo tatu: droo ya kwanza tarehe 12 Aprili itatoa washindi wanne watakaosafiri Marekani kushuhudia fainali za Kombe la Dunia.
“Droo ya pili tarehe 12 Mei itahusisha washindi watatu safari za Canada kushuhudia mechi za awamu ya makundi, na droo ya mwisho tarehe 11 Juni itawazawadia washindi saba zawadi mbali mbali,”amesema.
Naye Meneja Mwakilishi (Country Manager) Visa, Tanzania, Burundi, Rwanda, Uganda,Victor Makere amesisitiza umuhimu wa kushirikisha wateja wote na kufuata utaratibu wa kushiriki , akiweka mkazo kwenye ushirikiano wa CRDB na Visa CRDB.
Pia imehakikisha wateja wapya wanaweza kujiunga kwa urahisi kupitia huduma za kidijitali kwenye matawi na mawakala zaidi ya 30 nchini, kupata kadi papo hapo, na kushiriki kampeni hiyo, hatua inayounganisha sekta ya kifedha na fursa za burudani ya michezo.


