Ngome ya Wanawake ACT Wazalendo yatangaza Machi kuwa Mwezi wa Maombolezo

Na Mwandishi Wetu

MWENYEKITI wa Ngome ya Wanawake ya ACT Wazalendo, Janeth Rithe, ametangaza kuwa wanawake wa chama hicho hawataadhimisha Siku ya Wanawake Duniani mwaka huu, bali watautumia mwezi Machi kama kipindi cha maombolezo na kumbukumbu ya waliopoteza maisha katika matukio ya Uchaguzi, Oktoba 29, 2025.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 26, 2026 Ritte amesema maelfu ya wanawake nchini bado wako katika maumivu na simanzi, hivyo hawaoni sababu ya kusherehekea wakati wengine wakiendelea kuomboleza.

“Kila mwaka Machi 8 huadhimishwa kama siku ya mafanikio ya mwanamke, lakini kwa wanawake wa ACT Wazalendo mwaka huu itakuwa tofauti kutokana na kumbukumbu nzito ya tukio la Oktoba 29, ambalo limeacha kovu lisilofutika katika maisha yetu,” amesema.

Amefafanua kuwa mbali na vifo vilivyotokea siku hiyo, kumekuwepo na mwendelezo wa vitendo vya utekaji, mateso na mauaji vinavyohusishwa na watu wanaodai haki na demokrasia, hali inayosababisha wananchi kuishi kwa hofu ndani ya nchi yao.

Kwa mujibu wa Janeth, katika kipindi chote cha mwezi Machi, wanawake hao watafanya shughuli saba zikiwemo ibada na maombi ya kitaifa Selous, kutembelea na kufariji yatima, kusaidia wazee, kufanya usafi na kutoa msaada katika vituo vya afya, kuchangia damu, pamoja na kuzuru familia zilizofiwa na makaburi ya waliopoteza maisha.

“Pia tutazindua mnara wa kumbukumbu ya waliopoteza maisha Oktoba 29, na kila mwaka tutaweka mashada ya maua na kuwasha mishumaa kwa heshima ya marehemu hao,” amesema.

Ameongeza kuwa watahitimisha mwezi huo kwa Hitma na Misa kubwa kitaifa, Bara na Zanzibar, kwa ajili ya kuwaombea wote waliopoteza maisha wakidai haki na demokrasia.

Amesema hatua hiyo inalenga kuonyesha mshikamano wa wanawake na kusisitiza umuhimu wa ulinzi wa maisha, haki na demokrasia nchini.

“Tunataka taifa litambue kwamba maumivu ya mama si jambo la kupuuzwa. Haki lazima itafutwe na ilindwe,” amesema.

Aidha ameeleza pia kutoridhishwa na mwenendo wa tume iliyoundwa kuchunguza tukio hilo, akidai kuwa bado haijatoa majibu yanayoridhisha kwa familia za waathirika.

Ametoa wito kwa Watanzania kushikamana kudai amani, haki na kurejeshwa kwa misingi ya demokrasia, akisisitiza kuwa machozi ya mama ni deni la taifa ambalo halipaswi kupuuzwa.

spot_img

Latest articles

Haikubaliki, hali hii ya D’Salaam inachefua

KATIKA siku za hivi karibuni kumekuwa na matamko ya operesheni mbalimbali za kurejesha uzingatiaji...

Mwanasheria Mkuu asisitiza mageuzi ya Sheria za Anga

Na Mwandishi Wetu MWANASHERIA Mkuu wa Serikali, Hamza Johari amesisitiza juu ya umuhimu wa...

Wananchi Peramiho, Shiwinga kupiga Kura kesho kuchagua Mbunge, Diwani

Na Mwandishi Wetu WAPIGA Kura 127,632 walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura...

MIF 2026 kujadili mikakati ya kufikia uchumi wa kati wa juu 2050

Na Mwandishi Wetu SERIKALI imesema Mkutano wa Jukwaa la Wakurugenzi wa Bodi na Watendaji...

More like this

Haikubaliki, hali hii ya D’Salaam inachefua

KATIKA siku za hivi karibuni kumekuwa na matamko ya operesheni mbalimbali za kurejesha uzingatiaji...

Mwanasheria Mkuu asisitiza mageuzi ya Sheria za Anga

Na Mwandishi Wetu MWANASHERIA Mkuu wa Serikali, Hamza Johari amesisitiza juu ya umuhimu wa...

Wananchi Peramiho, Shiwinga kupiga Kura kesho kuchagua Mbunge, Diwani

Na Mwandishi Wetu WAPIGA Kura 127,632 walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura...