Na Tatu Mohamed
MWAKILISHI wa kimataifa kutoka ActionAid International, Teresa Anderson, amesema ipo haja ya kuweka usawa na kuzingatia haki za jamii zilizo hatarini zaidi wakati wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Ameyasema hayo jana katika mafunzo yaliyofanyika kwa njia ya mtandao yaliyoandaliwa na Media for Environment, Science, Health and Agriculture (MESHA) kupitia programu ya Cross Border Science Café.

Mafunzo hayo yaliwakutanisha wanahabari kutoka nchi sita za Afrika ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Zimbabwe, Zambia na Malawi, kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kuandika habari za kina na zenye uwajibikaji katika masuala ya mazingira.
Teresa alisema uandishi wa habari kuhusu tabianchi unapaswa kuzingatia zaidi sauti za jamii zinazoathirika moja kwa moja.
Alifafanua kuwa mataifa mengi yanayoathirika zaidi na mabadiliko ya tabianchi yana mchango mdogo katika uharibifu wa mazingira.

Alisema nchi tajiri ndizo zinazoongoza kwa uchafuzi wa gesi joto, hivyo zinapaswa kuchukua hatua za haraka kupunguza uzalishaji huo pamoja na kutoa fedha za kusaidia nchi zinazoendelea kukabiliana na athari hizo.
Akiangazia masuala ya ufadhili wa masuala ya mabadiliko ya tabianchi, Teresa ambaye ni Mkuu wa Haki ya Tabianchi katika ActionAid International, alisema kiwango cha fedha kinachotolewa kupitia Mfuko wa Fedha kwa Ajili ya Ubadilishaji wa Tabianchi (FRLD) cha dola milioni 250 hakikidhi mahitaji halisi yanayofikia takribani dola bilioni 395 kwa mwaka.

Alisisitiza umuhimu wa mfuko huo kupanuliwa hadi angalau dola bilioni 400 kwa mwaka, uwe na uwezo wa kusambaza fedha kwa haraka, kutoa ruzuku moja kwa moja kwa jamii na kuwa madhubuti katika kusaidia juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wake, kiongozi wa Mkakati na Masuala ya Kiufundi kutoka African Centre for Health, Climate and Gender Justice Alliance (ACHCGA), Imali Ngusale, alisema ushirikiano na vyombo vya habari ni njia muhimu ya kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
“Waandishi wa habari ni watu muhimu sana katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, hivyo ni muhimu kuendelea kuripoti na kujifunza mara kwa mara kuhusu masuala haya,” alisema.

Mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uandishi wa habari za sayansi, afya, kilimo na mazingira barani Afrika, kwa lengo la kuchochea uwajibikaji na mabadiliko endelevu katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.


