Waraka kwa Waziri Paul Christian Makonda

Katika dunia tunayoishi sasa michezo ni sekta inayoshikilia uchumi mkubwa. Wanamichezo wengi wamekuwa mabilionea kwa sababu tu ya michezo. Kwa mfano mchezo wa soka, umegeuka kuwa nguzo kubwa ya uchumi siyo wa mchezaji mmoja mmoja tu, bali hata kwa mataifa wanakotoka.

Kwa Tanzania, ukiacha imani za dini – Ukristo na Uislam, ambazo ndizo zenye wafuasi wengi zaidi, soka inafuatia kwa ufuasi baada ya dini hizo kuu mbili nchini. Ni jambo la bahati kubwa kuona kwamba soka inawaunganisha Watanzania kwa karibu zaidi kama ambavyo pia wanaunganishwa na imani zao za kidini. Hata ufuasi wa vyama vya siasa kwa Tanzania haufui dafu dhidi ya ufuasi wa soka.

Jambo la kujiuliza ni kwa kiwango gani kama taifa tunatambua fursa ambazo ziko kwenye michezo kwa ujumla wake?

Nianze kueleza kwa ufupi sana mchango wa walau wachezaji watano wakubwa wa soka kwa jamii zao. Sadio Mané huyu anatoka Senegal. Mapato yake yanakisiwa kuwa ni Dola za Marekani milioni 80. Katika mapato hayo, amejenga hopitali ya kisasa yenye vifaa vyote kwa gharama ya Dola za Marekani 500,000. Hospitali hii ameijenga kijijini Bambali alikozaliwa katika mkoa wa Sédhiou, karibu na mpaka wa Gambia. Kijiji hiki kina wakazi 2,000. Kabla ya hapo hakukuwa na hospitali ya kisasa. Mane pia amejenga shule kijijini kwake na miradi mingine mingi ambayo imebadili kabisa maisha ya jamii yake na Wasenegali kwa ujumla.

Mane hulipa posho ya Dola za Marekani 70 kwa mamia ya kaya- hapa ni kama TASAF yao, analipia ada wanafunzi kwa mamia. Yote haya yanatokana na mapato ya mpira wa kulipwa anaocheza.

Kuna Cristiano Ronaldo raia wa Ureno, anakadiriwa kuwa na utajiri wa Dola bilioni moja kutokana na kucheza mpira. Ronaldo amekuwa akitoa misaada ya huduma afya kwa watoto na misaada ya majanga. Kwa mfano, taarifa zinasema kuwa mwaka 2015 alitoa Dola za Marekani bilioni 1.5 za msaada kwa Gaza, aligharimia matibabu ya saratani kwa watoto nchini Ureno na Uhispania. Alipiga mnada tuzo zake za Ballon d’Or ili kufadhili mashirika ya misaada.

Yuko mtaalamu Lionel Messi raia wa Argentina, huyu anakisiwa kuwa na utajiri wa Dola za Marekani bilioni 1.3, chanzo chake ni soka la kulipwa. Michango yake ya kibinadamu ni mingi.

Kupitia taasisi ya Leo Messi, anajikita katika misaada ya afya na elimu ya watoto. Amejenga

na kusaidia hospitali za watoto huko Argentina na Uhispania; amefadhili vifaa vya tiba na matibabu ya saratani kwa watoto; amesaidia katika miradi ya elimu Amerika ya Kusini na Afrika.

Katika orodha hii yuko Didier Drogba raia wa Ivory Coast. Mapato yake ya soka yanakadiriwa kuwa Dola za Marekani milioni 100. Amewekeza katika misaada ya ujenzi wa amani na mshikamano wa taifa lao, hasa kutokana na kukumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa wanasiasa kugombea madaraka. Amejenga hospitali Abidjan na amefadhili kwa muda mrefu  miradi ya afya na elimu kupitia taasisi yake.

Pia yuko Marcus Rashford raia wa Uingereza. Anakadiriwa kuwa na mapato ya soka ya Dola za Marekani milioni 70. Amechangia katika misaada ya chakula kwa watoto na umaskini wa chakula nchini Uingereza. Kampeni yake ilisababisha serikali ya Uingereza kuongeza chakula cha bure shuleni wakati wa UVIKO-19; pia ilifadhili mipango ya chakula kwa watoto maskini; na alikusanya mamilioni ya Pauni kwa ajili ya benki za chakula.

Orodha ya wachezaji wa namna hii ni ndefu sana. Suala la kujiuliza ni kama Tanzania ina ufuasi wa soka wa kiwango hicho, hivi ni kwa kiwango gani tunaitazama kama uchumi, kama muhimili muhimu wa kukwamua watu wetu na taifa lao – kama fursa?

Ukiangalia mpira unaochezwa na klabu za ligi kuu nchini, unaweza kushawishika kuamini kwamba kama taifa tumepiga hatua kwenye soka, lakini ukija kuitazama timu ya taifa, Taifa Stars, unakumbuka kwamba kumbe viwango vyetu bado sana. Hapa ndipo ilipo siri, vilabu vikubwa vimesajili wachezaji wengi wazuri kutoka nje. Wa kwetu wazuri ni wachache sana. Sababu yake, hatuna uwekezaji wa ndani.

Hatuna uwekezaji wa kuibua vipaji, kuvikuza na kuvilea mpaka vitupe matunda mazuri. Hatuna wa kwetu. Utawasikia tu Mbwana Ally Samatta na Thomas Ulimwengu. Hao tu, na sasa wamezeeka hakuna wengine.

Tuna changamoto kubwa kama taifa la kugeuza ufuasi huu wa soka kuwa fursa ya kuinua vijana wetu kiuchumi. Tunahitaji uwekezaji wa kweli katika soka. Tunahitaji kujenga akademi za soka za maana, akademi zinazoweza kuzaa matunda. Tunahitaji kutupia jicho kwenye soka kuibua vipaji, kuviendeleza na kuvilea. Hatuwezi kusubiri kulipa zawadi ya kila goli linalofungwa tu, pamoja na kwamba ni ishara njema, hiyo haitoshi kujenga soka endelevu nchini.

Hali ni hiyo hiyo kwenye riadha. Wakati Kenya na Ethiopia zikitamba kote duniani kwa wanariadha bora wa masafa marefu, sisi pamoja na kuwa na aina ya kijiografia na hali ya hewa inayofanafa na nchi hizo ambazo sote tupo kwenye Bonde la Ufa, na wanariadha wao wakitoka katika ukanda huo, sisi hatuna wanariadha wa viwango vyao. Hatuwekezi, hatujitumi kutambua kwamba ipo fursa kubwa hapo.

Mambo haya yanahitaji utashi imara wa kisiasa, yanahitaji uwekezaji mkubwa na ufuatiliaji, yanahitaji kujitambua, na yanahitaji kujua kwamba eneo hilo ni moja ya fursa muhimu ya ajira na kuinua uchumi.

Yote haya yako chini ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Hii ni wizara ambayo amekabidhiwa Waziri Paul Christian Makonda kuiongoza. Akiwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Makonda aliandaa maonyesho ya magari aina ya Land Rover – Land Rover Festival iliyofanyika Arusha Oktoba 12–14, 2024, takribani magari zaidi ya 1,000 ya chapa ya Land Rover yalikusanyika, msafara ukiwa na urefu wa takriban kilomita 12, na tukio hilo lilijaribu kuvunja rekodi ya dunia ya msafara mrefu wa magari ya aina hiyo. Lilikuwa ni tukio kubwa.

Binafsi kwa moto kama ule wa Land Rover Festival- ningetamani kazi kuu ya Waziri Makonda iwe ni kugeuza ufuasi wa soka Tanzania uwe fursa, tuzalishe vipaji, viende kusakata soka nje. Tupate akina Samatta na Ulimwengu wengi. Warejeshe nguvu kubwa ya pesa nchini kama magwiji wengine wa mpira duniani. Hili ndilo ombi langu kwa Waziri Paul Christian Makonda. Hii ndiyo alama ninayotamani atuachie.

spot_img

Latest articles

ETDCO yaahidi kukamilisha Mradi wa Umeme katika vitongoji 372 Ruvuma kwa wakati

Na Mwandishi Wetu KAMPUNI ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji...

Wadau sekta ya Hali ya Hewa wajadili utabiri wa Masika 2026

Na Mwandishi Wetu WADAU kutoka sekta mbalimbali nchini wamekutana kujadili utabiri wa msimu wa...

WMA yafunga Mtambo wa kisasa unaohakiki Dira za Maji Dodoma

Na Mwandishi Wetu WAKALA wa Vipimo (WMA) umesimika mtambo wa kisasa wa kidijitali wa...

Benki ya CRDB yaja na ‘Benki Kimpango Wako’ yaahidi huduma bora zaidi mwaka 2026

Na Mwandishi wetu BENKI ya CRDB imezindua kampeni yake ya mwaka 2026 inayoitwa ‘Benki Kimpango...

More like this

ETDCO yaahidi kukamilisha Mradi wa Umeme katika vitongoji 372 Ruvuma kwa wakati

Na Mwandishi Wetu KAMPUNI ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji...

Wadau sekta ya Hali ya Hewa wajadili utabiri wa Masika 2026

Na Mwandishi Wetu WADAU kutoka sekta mbalimbali nchini wamekutana kujadili utabiri wa msimu wa...

WMA yafunga Mtambo wa kisasa unaohakiki Dira za Maji Dodoma

Na Mwandishi Wetu WAKALA wa Vipimo (WMA) umesimika mtambo wa kisasa wa kidijitali wa...