Tume ya Jaji Chande ijitafakari upya

KATIKA dunia tunayoishi sasa suala la uwazi katika kuendesha mambo limekuwa miongoni mwa nguzo kuu za kusaidia kupata mafanikio na uwajibikaji. Misingi ya kuendesha mifumo, hasa katika utawala uliojengwa kwenye demokrasia, uwazi hautajwi tu kama moja ya vitu muhimu vya kuzingatiwa katika utendaji kazi wa kila siku, bali hugeuka kuwa jambo la lazima lisilokuwa na mbadala wake. Vinginevyo, kukosekana kwa uwazi hutoa fursa ya majungu, uongo, kutokuwajibika, lakini kikubwa zaidi kupoteza kuaminika.

Kwa maana hiyo, uwazi huimarisha imani, uwajibikaji na ufanisi katika utendaji. Katika uendeshaji wa taasisi au mifumo iliyobuniwa na binadamu, uwazi ukikosekana hufungua milango ya kutokuaminiana, kukosekana kwa uhalali, kupotea kwa uwajibikaji, kushuka kwa weledi na ubora wa maamuzi na thamani ya kazi kwa ujumla wake.

Mazingira yanayoepuka uwazi aghalabu huzaa ulegevu na hata kuporomoka kwa maadili na uadilifu katika mwenendo mzima wa utumishi, iwe ni kwa sekta ya umma au hata binafsi.

Nimesukumwa kuzungumzia uwazi leo kwa sababu kuu moja. Kwamba wiki iliyopita Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Oktoba 29, 2025 ambayo inaongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman, iliripotiwa kuwa ilibadilisha utaratibu wake wa kazi iliyokuwa imeutumia kwa kitambo wa kuruhusu waandishi wa habari kusikiliza ushahidi/maelezo/taarifa za wananchi walizokuwa wanatoa mbele ya Tume hiyo. Kwamba sasa hawataruhusiwa kusikiliza moja kwa moja maelezo hayo, badala yake watapewa taarifa na Tume.

Taarifa ambazo ziliripotiwa na vyombo vya habari ilisema kuwa uamuzi wa Tume unalenga kulinda faragha ya mashahidi wanaofika mbele yake kutoa taarifa/ushahidi/maelezo. Hali hii ilijulikana Jumapili ya Januari 24, 2025 siku Tume hiyo ilipokuwa kwenye ukumbi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, kusikiliza ushahidi wa watu walioathiriwa na matukio ya Oktoba 29, 2025.

Tume hii imekuwa kazini tangu Desemba mwaka jana ilipoundwa na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania na ilipewa miezi mitatu kukamilisha kazi ya uchunguzi wa matukio ya Oktoba 29, 2025. Hadidu kuu za Tume hiyo ni kubaini chanzo halisi cha matukio ya wakati wa uchaguzi Oktoba 29, 2025 na baada; kuchunguza lengo la walioratibu na kushiriki matukio hayo; kuchunguza madhara yaliyotokea; kuchunguza mazingira ya hatua zilizochukuliwa na serikali na vyombo vyake; kupendekeza maeneo yanayohitaji kuimarishwa kuongeza uwajibikaji wa viongozi na raia katika kulinda amani nchini, utawala bora na haki za binadamu na mwisho kuchunguza jambo jingine lolote ambalo Tume itaona linaendana na majukumu yake.

Ingawa Tume ina haki ya kuona na kuamua njia ya kufanya kazi yake, kwa maana hiyo hata kuzuia waandishi kusikiliza na kuripoti taarifa zinazofika mbele yake kutoka kwa mashahidi mbalimbali, uamuzi wa namna hiyo yafaa upimwe kwa uangalifu mkubwa ili kusaidia kile kilichoelezwa hapo juu – faida ya uwazi katika kuendesha mifumo na taasisi.

Naomba kurejea nyuma kidogo. Kuanzia miaka ya mwanzo ya 2000 hadi 2015 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilijijengea utaratibu wa kuendesha vikao vyake kwa uwazi. Yaani Bunge live. Bunge lilikuwa likiendeshwa mubashara. Ilipofika 2016 kwa sababu ambazo watawala wanazijua, waliamua kubadili mfumo wa kuendesha Bunge na kuingia katika ‘giza’. Bunge live ikapigwa marufuku.

Hakuna raia wa Tanzania ambaye alikuwa anajisumbua kufuatilia shughuli za Bunge asiyejua faida ambazo taifa lilipata kwa Bunge kuwa live. Hakuna asiyekumbuka mijadala ya moto iliyokuwa inaibuka Bungeni, hakuna asiyekumbuka kiwango cha uwajibikaji cha serikali kwa Bunge. Hakuna kipimo chochote kinachoweza kupinga ukweli kwamba ile Bunge kuwa live, ilihamasisha mambo makuu matatu. Mosi, ufuatiliaji wa karibu wa wananchi kwa Bunge lao; pili umakini wa wabunge katika wajibu wa uwakilishi katika kuisimamia na kuiwajibisha serikali na tatu, utayari wa serikali kutekeleza mambo yake kwa weledi, uwazi na ufanisi uliotarajiwa na wananchi.

Kwa maana hiyo, faida ya uwazi ilisaida sana kulifanya Bunge kuwa chombo cha wananchi kinachotekeleza wajibu wake sawasawa. Kwa mantiki hiyo, uwazi uliimarisha siyo tu uwezo wa Bunge bali pia uliiweka serikali kwenye mstari sahihi wa utendaji na uwajibikaji kwa umma. Kinyume cha hali hii ni dhahiri – Bunge dhaifu!

Inawezekana Tume ya Jaji Chande imetafakari kwa kina sababu za kuondoa uwazi huu katika kusikiliza maelezo/taarifa/ushahidi wa waliokumbwa na madhila ya matukio ya Oktoba 29, 2025. Inawezekana. Hata hivyo, tafakari ya kina inapotazama hadidu za rejea za Tume, inapotafakari hali ya wananchi ya kukata tamaa kutokana na mwenendo wa muda mrefu sasa wa vyombo vya mabavu dhidi ya raia, hatua ya kuamua kufanya mikutano yake sirini, pengine haitakuwa na faida kama ingelikuwa kinyume chake.

Ni vema ikakumbukwa, kazi ya Tume ya Jaji Chande ni mojawapo ya hatua muhimu na ya msingi sana ya kutafuta uponyaji wa taifa kwa haya ambayo yalishuhudiwa wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025. Ni kazi ambayo inafaa ianze kujenga imani kwa wananchi kwamba ni kweli kuna hatua zinakwenda kuchukuliwa kutibu taifa.  

Tume nyingi za kutafuta tiba kwa taifa zimekuwa zikiendesha mambo yake kwa uwazi. Kwa mfano, ndivyo ilivyofanya Tume ya Jaji Francis Nyalali ya kupata maoni ya wananchi kama Tanzania iwe nchi ya mfumo wa chama kimoja au vingi. Tume hii ilikuwa na uzito mkubwa wa kushauri hatima ya mfumo wa kisiasa nchini Tanzania. Ilikuwa imebeba dhima ya kuamua mwelekeo wa kisiasa wa nchi ambayo ilikuwa imekita mizizi katika mfumo wa siasa ya chama kimoja tena chini ya itikadi ya Ujamaa ambayo haki nyingi za kiraia zilikuwa zimekamatwa na chama pekee cha kisiasa kilichokuwako wakati huo.

Kila nikitafakari, ninashawishika kuamini kwamba uamuzi wa Tume wa kusikiliza ‘gizani’ maelezo/taarifa/ushahidi wa waathirika wa matukio ya Oktoba 29, 2025 na baada yake, hautaisaida si tu Tume yenyewe, bali pia na serikali na wananchi. Hatua ambayo taifa ilipo sasa inatakiwa mwelekeo mpya, na huo hauwezi kukwepa uwazi kwa kila kitu kinachokwenda kutendeka ili kujenga imani ya wananchi. Zama za kutenda vitu ‘gizani’ haziwezi kutibu majeraha. Haziwezi kuondoa kushukiana na kutuhumiana vibaya. Naiomba na kuishauri Tume ya Jaji Chande ifikirie upya uamuzi wake wa kufungia waandishi wa habari nje. Waandishi wa habari wana wajibu wa kusaidia nchi kuandika historia mpya. Historia ya kujiponya.

spot_img

Latest articles

Tanesco yafanya ukaguzi wa Mita kitaalamu kubaini ukweli malalamiko ya umeme kuisha haraka yagundua mita zipo sawa

📌 Ni kufuatia malalamiko ya baadhi ya wateja kwenye mitandao ya kijamii na vyombo...

Vijana Dar wakutana kusherehekea kumbukizi ya kuzaliwa Rais Samia, wasifu mchango wake kwa maendeleo ya vijana

Na Mwandishi Wetu VIJANA Jijini Dar es Salaam wameungana kusherehekea siku ya kumbukizi ya...

Twiga, Tanga Cement wapewa saa 48 kujisalimisha

Na Mwandishi Wetu SERIKALI kupitia Wizara ya Madini imezipa Kampuni za Twiga Cement na...

Watendaji wa Uchaguzi watakiwa kutekeleza majukumu kwa weledi

Na. Mwandishi Wetu, Iringa WATENDAJI wa uchaguzi wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na weledi...

More like this

Tanesco yafanya ukaguzi wa Mita kitaalamu kubaini ukweli malalamiko ya umeme kuisha haraka yagundua mita zipo sawa

📌 Ni kufuatia malalamiko ya baadhi ya wateja kwenye mitandao ya kijamii na vyombo...

Vijana Dar wakutana kusherehekea kumbukizi ya kuzaliwa Rais Samia, wasifu mchango wake kwa maendeleo ya vijana

Na Mwandishi Wetu VIJANA Jijini Dar es Salaam wameungana kusherehekea siku ya kumbukizi ya...

Twiga, Tanga Cement wapewa saa 48 kujisalimisha

Na Mwandishi Wetu SERIKALI kupitia Wizara ya Madini imezipa Kampuni za Twiga Cement na...